Mfuko wa Nishati safi ya kupikia (CookFund) Tanzania imetoa ruzuku
yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.2 kwa kampuni 16 zinazojishughulisha
na utoaji wa huduma za uuzaji wa nishati safi ya kupikia nchini kwa
lengo la kuzisaidia kutoa huduma hizo kwa gharama nafuu na zenye ubora
unaowanufaisha wateja wa kipato cha chini nchini Tanzania.
Wanufaika
hao 16 ni matokeo ya mwito wa kwanza wa maombi ya ufadhili yaliyotolewa
mnamo Septemba 2022 kupitia program hiyo inayofadhiliwa na Umoja wa
Ulaya (EU) ukilenga katika maeneo ya teknolojia safi ya kupikia hususani
gesi ya ‘mitungi’ yaani Liquified Petroleum (LPG), majiko ya umeme
(EPC) ,majiko ya mkaa banifu (ICS) mkaa tofali utokanao na vumbi la
makaa ya mawe (briquettes) na nishati ya mafuta itokanayo na mabaki ya
mimea (bioethanol)
Hafla fupi ya kukabidhi hundi za fedha kwa
wanufaika hao ilifanyika jijini Dar es Salaam katikati ya wiki hii
ikiongozwa na Waziri wa Nishati January Makamba sambamba na Balozi wa
Umoja wa Ulaya Manfredo Fanti, na Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji
wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) Tanzania Peter Malika ambaye mfuko wake ndio
unaratibu program ya CookFund.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo
Waziri Makamba aliwasisitiza wanufaika wa ruzuku hiyo kuhakikisha
wanazitumia fedha hizo kulingana na malengo ya mpango huo ili matokeo
mazuri ya mpango huo yaweze kuwafikia Watanzania wengi.
“Ni
vyema mkafahamu kuwa huu si mkopo bali ni ruzuku ambayo mnaipata moja
kwa moja kwa jina la nchi yetu.Hivyo ni vyema mkahakikisha Watanzania
wananufaika kweli kupitia mpango huu kwa kuwafikishia bidhaa zenu za
nishati kwa bei nafuu ili waweze kuondokana na matumizi ya nishati chafu
ambazo si rafiki kwa mazingira,’’ alisema
Akizungumzia zaidi
programu ya CookFund Waziri Makamba alisema ni moja ya suluhu la msingi
kwa nchi katika kupambana na matumizi ya nishati chafu kwa sababu
inawahakikishia wananchi upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu.
Kwa
upande wake Balozi Manfred Fanti aliwataka wafanyabiashara walionufaika
na ruzuku hiyo kuonyesha kwamba wanaweza kuuza bidhaa zao za nishati ya
kupikia kwa bei nafuu na kwa wateja wengi wapya kupitia msaada wa
kifedha walioupata kupitia mpango huo
"Umoja wa Ulaya (EU)
unatarajia ruzuku hizi zitasaidia watumiaji wapya wa nishati ya kupikia
hapa nchini kuweza kupata vifaa vyote vinavyohusika na mfumo mzima wa
zana za kupikia kwa bei nafuu na zaidi tuendelea kuhamasisha watanzania
wengi zaidi waendelee kuachana na mbinu za kupikia ambazo zinachafua na
kuharibu mazingira".
"Tunatumai kushuhudia matokeo ya
kuridhisha katika siku zijazo na kupungua kwa familia zinazotumia
nishati ya kuni au mkaa kwa kupikia." Alisema.
Akitoa shukurani
zake kwa Serikali ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, Bw. Peter Malika
alisema kwa kuzingatia athari kubwa ya matumizi ya nishati itokanayo na
mimea katika suala zima la mapishi nchini, ipo haja ya msingi ya
kuongeza uwekezaji katika mnyororo wa thamani kwenye nishati safi ya
kupikia ili kuharakisha mabadiliko kuelekea kwenye matumizi ya nishati
safi ya kupikia.
“Kwa kuwa hii ni awamu ya kwanza ya maombi
yaliyoidhinishwa ambayo yanahusisha wanufaika 16 ambao kwa jumla
watahudumia kaya 191,336 katika maeneo yao na kutoa ajira 191 katika
kipindi cha miaka mitatu, tunatarajia kuzindua mwito mpya wa mapendekezo
mwezi huu kwa hivyo kuendelea awamu nyingine ya ruzuku kwa kama hizi,’’
alibainisha.
CookFund ni programu ya miaka mitatu
inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) chini ya Mpango wa mkakati
jumuishi wa kutumia nishati safi ya kupikia nchini na Mfuko wa 11 wa
Maendeleo ya Ulaya (EDF), unaolenga kuchangia dhamira ya Tanzania ya
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuongeza sehemu ya idadi ya
watu na upatikanaji endelevu wa ufumbuzi wa kupikia.
UNCDF ndiye
taasisi msimamizi na mtekelezaji wa program ya CookFund. Mpango huu
unalenga kushughulikia "upungufu wa mitaji" kwa upande wa watendaji wa
sekta binafsi na changamoto ya kumudu gharama kwa watumiaji wa mwisho
kwenye kaya.
Programu ya CookFund inachangia vipaumbele vya
kimkakati vya Mfumo wa Ushirikiano wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania
kwa kusaidia upatikanaji bora wa nishati safi na teknolojia, usimamizi
endelevu wa maliasili na kuongeza kasi ya kazi zenye heshima katika
sekta rasmi.
Waziri wa Nishati January Makamba (kushoto) akizungumza na wageni waalikwa wakati hafla fupi ya kukabidhi hundi kwa kampuni 16 za nishati safi ya kupikia zilizonufaika na ruzuku kutoka Mpango wa Tanzania CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya ukilenga kusaidia kampuni hizo kutoa huduma zao kwa bei nafuu na zenye ubora unaowanufaisha wateja wa kipato cha chini katika maeneo ya vijijini na mijini kote nchini.
Balozi wa Umoja wa Ulaya Manfredo Fanti Makamba (kushoto) akizungumza na wageni waalikwa wakati hafla fupi ya kukabidhi hundi kwa kampuni 16 za nishati safi ya kupikia zilizonufaika na ruzuku kutoka Mpango wa Tanzania CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya ukilenga kusaidia kampuni hizo kutoa huduma zao kwa bei nafuu na zenye ubora unaowanufaisha wateja wa kipato cha chini katika maeneo ya vijijini na mijini kote nchini.
Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) Tanzania Peter Malika ambaye mfuko wake ndio unaratibu program ya CookFund akizungumza na wageni waalikwa wakati hafla fupi ya kukabidhi hundi kwa kampuni 16 za nishati safi ya kupikia zilizonufaika na ruzuku kutoka Mpango wa Tanzania CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya ukilenga kusaidia kampuni hizo kutoa huduma zao kwa bei nafuu na zenye ubora unaowanufaisha wateja wa kipato cha chini katika maeneo ya vijijini na mijini kote nchini.
Waziri wa Nishati January Makamba (wa tatu kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya fedha kwa wawakilishi wa kampuni mbalimbali za nishati safi ya kupikia zilizonufaika na ruzuku kutoka Mpango wa Tanzania CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya ukilenga kusaidia kampuni hizo kutoa huduma hizo kwa bei nafuu na zenye ubora unaowanufaisha wateja wa kipato cha chini katika maeneo ya vijijini na mijini kote nchini. Wanaoshuhudia ni pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya Manfredo Fanti (Katikati), Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) Tanzania Peter Malika (wa pili kulia) na wadau wengine muhimu wa mpango huo.
Baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia hafla hiyo.
Waziri wa Nishati January
Makamba (katikati mstari wa nyuma) akiwa kwenye picha ya pamoja na wageni
waalikwa pamoja na wadau muhimu wa Mpango wa Tanzania CookFund wakati wa hafla
fupi ya kukabidhi mfano wa hundi ya fedha
kwa wawakilishi wa kampuni mbalimbali za nishati safi ya kupikia
zilizonufaika na ruzuku kutoka Mpango wa Tanzania CookFund unaofadhiliwa na
Umoja wa Ulaya ukilenga kusaidia kampuni hizo kutoa huduma hizo kwa bei nafuu
na zenye ubora unaowanufaisha wateja wa kipato cha chini katika maeneo ya
vijijini na mijini kote nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...