
MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar apongeza Serikali kwa Kuzindua mradi wa miundombinu tafiti utakaochakata mazao ya uchumi wa Buluu Zanzibar.
Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo Aprili 11, 2023 wakati akizindua Kituo cha Miundombinu wezeshi ya Kitafiti inayolenga kuimarisha uzalishaji na uchakataji wa mazao bahari kupitia uchumi wa buluu katika Chuo Kikuu cha Zanzibar- SUZA kilichopo kampasi ya Nkrumah eneo la Maruhubi - Unguja
"Natoa pongezi zangu za dhati kwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Hussein Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa juhudi zao kubwa wanazoendelea kuzichukua katika kutanua wigo wa elimu hapa nchini" alisema.
"Nachukua nafasi hii kuushukuru Uongozi wa Wizara ya elimu kupitia Chuo cha Taifa Zanzibar- SUZA kwa kushirikiana na COSTECH kwa kunipa heshima ya mwaliko wa kuwa mgeni rasmi, kadhalika
Aidha, Mhe. Hemed amefafanua kuwa kuwa Serikali zote mbili (2) ya awamu ya Sita na Serikali ya Awamu ya nane zinaelewa umuhimu wa kuimarisha uchumi wa buluu na inatambua umuhimu wa tafiti na zimejikita kuwajengea uwezo na ujuzi wataalamu ili utumike kuratibu maendeleo ya utafiti
"Niwashukuru sana ndugu zangu wa COSTECH kwa kuendelea kuunga mkono juhudi hizi hasa kwa upande wa Zanzibar, haya mliyofanya mmeendana na adhima ya Serikali ya Awamu ya Nane inayolenga kupeleka nguvu katika uchumi wa buluu tunashukuru sana na tunaombeni muendelee kutoa mashirikiano na kushajihisha pamoja na kuongeza ubunifu kwa watumiaji wakubwa wa mifumo hii" alisema mhe. Hemed
Alihitimisha kwa kutoa wito wa kuondokana changamoto ya tafiti kuishia kwenye makaratasi na maktaba zinazokosa miundombinu ya usambazaji wa matokeo ya tafiti na kuelekeza Kituo hiki kipya kijikite kuongeza tija kwa wanachi pamoja na kuwajengea uwezo wavuvi na vijana wanaosomea fani hizi hapa nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu na Amali Zanzibar, Mhe. Ali Abdugulam alisema mwelekeo wa serikali ya Zanzibar ni uchumi wa buluu hivyo wanatafiti wanatakiwa kufanya tafiti za kutosha zinazolenga pia kutunza mazingira.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu amesema Tume ilipokea maandiko 75 yaliyoshindanishwa na mradi huu wa Chuo cha Taifa Zanzibar (SUZA) ilifadhiliwa kiasi cha TZS Millioni 400 ili kujenga miundombinu wezeshi ya kitafiti inayochocheo utengenezaji wa Sera za Serikali za uchumi wa buluu kwa maendeleo ya haraka.
Dkt. Nungu ameongeza kuwa COSTECH kwa kipindi cha Miaka minne (4) iliyopita imeshatoa kiasi cha TZS Bilioni 1.7 kugharamia uratibu miradi kimkakati ya kibunifu na kitafiti Zanzibar ili matokeo yake yatumike kuishauri Serikali kwa kuongozwa na Utafiti.
Vilevile, Makamu Mkuu SUZA, Prof. Moh’d Makame amesema kupitia mradi huu Serikali itakusanya wataalamu wa tafiti mbalimbali ili kutathimini hatua za maendeleo zinazochukuliwa kupitia sera ya uchumi wa buluu.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Kituo cha Kipya cha Utafiti, Dkt. Mary Mtumwa Khatib alisema kupitia Kituo hiki kitapunguza changamoto za wavuvi kupitia ujenzi wa miundombinu ya utafiti, maabara ya ubora wa maji na chakula cha samaki kwa kutumia uhawilishaji wa Teknolojia ya uzalishaji vifaranga wa viumbe hai wa baharini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...