Na Mwandishi wetu Dar es Salaam
Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha shilingi bilioni 400 zitumike kuboresha na kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini ili sekta ya tehama itoe mchango stahiki kwa taifa.
Akizungumza pembezoni mwa Jukwaa la Tano la Uvubunifu na Teknolojia, Naibu Waziri Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew alisema hatua hiyo ina maana kubwa katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano ili kuchochea ubunifu kwa lengo la kujenga uchumi endelevu na wenye ushindani duniani.
Dhima ya jukwaa hilo ilikuwa ni ‘Sera ya ubunifu --- Mtazamo wa mbele na jumuishi wa uundaji sera katika enzi ya kidigitali’.
“Serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini. Hii ni pamoja na upatikanaji wa huduma muhimu ya mawasiliano. Na ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake ametenga zaidi ya shilingi bilioni 400 ili kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano inaboreshwa,” alisema Mhandisi Mathew
Alisema majukwaa kama hayo yanasaidia kubaini changamoto mbalimbali zinazokwamisha ustawi wa sekta hiyo. Aidha yanasaidia kukusanya mapendekezo yenye lengo la kuboresha sekta ya tehama na kuibua fursa zilizomo katika sekta hiyo hapa nchini ili Tanzania iwe na nafasi stahiki katika ulimwengu wa kidigitali.
“Sisi kama serikali tumeyapokea mapendekezo na tutayafanyia kazi kwa lengo la kufikia azma ya Dk. Samia ya kuvutia uwekezaji hapa nchini,” alisema Mhandisi Mathew
Alibainisha kuwa serikali itatengeneza sera ambayo itaweka mkazo katika kujenga mfumo wa kukuza uchumi wa kidigitali na uchumi huo uendeshwe na huduma za kitehama. Alisema tayari miundombinu ya Tanzania imekaa vizuri lakini lengo ni kuwa na mifumo ambayo itasaidia wananchi kupata huduma bila vikwazo vya aina yoyote.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk. Moses Mwasaga, alisema kupitia majukwaa kama hayo wataalamu wanaweza kujadili changamoto na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kutengeneza sera ambayo itakuwa rafiki katika kutatua changamoto zinazoibuka mara kwa mara katika sekta hiyo kwani sekta yenyewe nayo inabadilika kila wakati.
“Kupitia majukwaa kama haya tunaweza kujadili changamoto na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kutengeneza sera ambayo itakuwa rafiki katika kutatua changamoto zinazoibuka katika sekta hii; sekta hii inabadilika kila wakati hivyo kuna haja ya kutengeneza sera itakayokwenda sambamba na kasi hii,” alisema Dkt. Mwasaga
Aliisifu Benki ya CRDB kwa kuzindua programu wezeshi kwa wajasiriamali vijana na wanawake wenye biashara na mawazo bunifu kwa kuwapa mitaji itakayowasaidia kukuza biashara zao katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya tehama. Programu hiyo inaitwa imbeju.
“Benki hiyo mbali ya kuwapa mitaji wabunifu imekuwa ikiwajengea uwezo kwa kuwapa mafunzo yatakayopelekea Tanzania kuwa mshindani kwenye soko la ndani na nje ya nchi kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora unaohitajika,” alisema Dk. Mwasaga
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara Tanzania (TNBC), Dk. Godwill Wanga, alisema kuwa Rais Samia anataka teknolojia ichangie kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania. “Kwa hiyo tunategemea sana wabunifu wadogo katika kutekeleza hilo ili kukuza na kuendeleza sekta hii hapa nchini,” alisema Dk. Wanga
Alisema serikali ina nia athabiti ya kuwasaidia wadau wa sekta ya tehama na akawahimiza kuendelea kufanya ubunifu. “Serikali iko tayari kuwasaidia ili kuhakikisha sekta hii inakuwa hapa nchini na kutoa mchango chanya katika kukuza pato la taifa,” alisisitiza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...