MKUU wa Mkoa wa Singida, Juma Homera ameipongeza taasisi ya kusaidia Sekta binafsi ya Kilimo (PASS Trust )juu ya kuja na mpango wa kukuza uchumi kupitia ajenda ya ukuaji wa Kijani Shirikishi hivyo ni njia bora ya kuchochea Kilimo endelevu.
Akizungumza hivi karibuni Mkoani humo katika mkutano wa mashauriano na wadau mbalimbali wa Sekta ya kilimo ya kuhamasisha uzalishaji unaozingatia ukuaji wa Kijani Shirikishi,alisema ukuaji huo wa Kijani Shirikishi utachochea na kukuza uchumi kupitia ajenda za Kilimo.
"Naipongeza PASS Trust kwa ubunifu na kuanzisha ajenda ya Ukuaji wa Kijani Shirikishi ambayo kwa hakika inachochea maendeleo endelevu ya kiuchumi ambayo yanaenda sambamba na utunzaji wa mazingira na kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo”,
Homera aliongeza kuwa kupitia ajenda hiyo itawawezesha wakulima kujihusisha kikamilifu na kilimo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Trust, Yohane Ibrahim Kaduma alisema, “PASS Trust ina mchango mkubwa katika kuchochea na kuwezesha ukuaji wa kilimo nchini Tanzania huku tukitoa kipaumbele kwa vijana na wanawake ambapo tunawapa dhamana ya mikopo na huduma za maendeleo ya biashara ili kufikia malengo yao”.
Aliongeza kuwa PASS Trust pia ilianzisha kampuni tanzu ya PASS Leasing ambayo inatoa zana zote za kilimo kutoka kwa wauzaji mbalimbali washirika nchini Tanzania.Akifafanua kuhusu ushirikishwaji wa wadau wengine wa kilimo katika kikao hicho, Mkurugenzi Kaduma aliongeza
“Tunaamini katika ushirikiano na mashirika mengine yanayohudumia sekta ya kilimo, ndiyo maana tumewaalika wadau wengine wa sekta hiyo kwa ajili ya kujadili na kubainisha njia mbalimbali zinazoweza kusaidia sekta ya kilimo kupitia ajenda ya Ukuaji wa Kijani Shirikishi ambayo inalenga kuhimiza ukuaji wa kilimo kwa kujali uhifadhi wa mazingira asilia.
Serikali ya Denmark inafadhili PASS Trust ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na maendeleo ya biashara kwa wafanyabiashara wa kilimo nchini Tanzania,
Imesaidia kwa kiasi kikubwa wakulima wengi ambao wamegawanyika katika makundi matatu, ambayo ni watu binafsi, vikundi na makampuni yanayojihusisha na kilimo kupitia huduma za vifaa na misaada ya kifedha kwa ajili ya kukuza kilimobiashara.
PASS inatoa huduma katika mikoa yote nchini Tanzania yenye ofisi za kanda katika mikoa sita ambayo ni Kanda ya nyanda za juu kusini (Mbeya) kanda ya kati na mashariki(Singida) kanda ya magharibi(Tabora),Kanda ya Kusini (Ruvuma),Kanda ya Kaskazini(Arusha),Kanda ya ziwa (Mwanza) na Ofisi kuu Dar es Salam.PASS pia inapatikana kwa urahisi katika mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, YouTube, Twitter na kupitia Tovuti yenye jina la PASS Trust.
Kwa maelezo zaidi inapatikana pia kwa namba ya huduma kwa wateja kwa namba ya bure 0800750037.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...