Na Mwaandishi Wetu Lindi
WAKULIMA Mkoani Lindi wamejipanga kufanya kilimo biashara kupitia zao la Mihogo Mkoani humu ili kujiinua kutoka katika kujiinua kiuchumi na kumaliza kabisa upungufu wa chakula kwenye familia zao.
Hatua hiyo imekuja baada ya wakulima hao kugundua uwepo wa mbegu bora za Mihogo ambazo zimezalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) kituo cha Naliendele Mkoani Mtwara.
Wakizungumza na waandishi wa habari Mkoani hapa, wakulima hao wamesema licha ya uwepo wa mbegu bora pia wamejifunza kanuni bora za kilimo hicho cha biashara.
"Kuna mbegu bora zaidi ya nane ambazo nimeziona kupitia shamba darasa la TARI Naliendele hapa kwenye kata yetu, mbegu ni nzuri sana, zinafaa kwenye kilimo biashara," amesema Bendita Mkanga Mkulima wa Kata ya Kiwalala ,Wilaya ya Mtama Mkoani Lindi.
Mkanga ambaye kwa muda mrefu amesema amekuwa akitumia mbegu za asili kufanya kilimo cha kaweida sasa anajipanga kufanya Kilimo biashara ili kujiinua kiuchumi na kujiongezea zaidi chakula kwenye familia yake.
"Mimi ni mkulima wa Mihogo ambaye nilikuwa natumia mbegu tu za kienyeji ambazo hazinipi manufaa katika kilimo, lakini leo nimekuja kwenye shamba darasa ambapo tumevuna Mihogo ambayo imepandwa kutumia mbegu bora na imepandwa kitaalamu, nimeiona na nimejifunza na sasa naenda kubadili na kufanya kilimo nipate manufaa zaidi," amesema.
Mkanga pamoja na wakulima wengine Mkoani Lindi wamekuwa wakitumia mbegu za asili kufanya kilimo cha Mihogo kwa ajili ya kupata chakula tu ambacho pia hakitoshelezi.
"Nilikuwa nalima Mihogo kwa ajili ya kupata chakula cha familia yangu tu, kwake sababu tunatumia mbegu za asili ambazo hazizai sana, zinakuwa na magonjwa mengi na lazima tulime kwa msimu tu, kitu ambacho hakitupi manufaa yoyote zaidi ya chakula tena ambacho wakati mwingine hakitoshelezi familia," amesema Aziza Nungu Mkulima wa Wilaya ya Mtama.
Amesema elimu ambayo amepata kupitia shamba darasa la Mihogo iloyopandwa kutumia mbegu bora, ameona tofauti kubwa kati ya mbegu za asili na mbegu mpya za TARI na sasa anabadili fikra kufanya kilimo biashara ili apate manufaa zaidi.
"Hizi mbegu za TARI ni nzuri sana, zinazaa sana, kwanza nzito, ujazo mwingi, mirefu. Kwenye shina moja unakuta mizizi (Mihogo) mingi ambayo kwa shina moja ninaweza kula na familia kwa siku tatu mpaka nne tofauti na mbegu za asili," amesema.
Amesema kilimo cha Mihogo kutumia mbegu za asili haziwapi faida kwa sababu ya kutozaa kwa wingi, magonjwa na ukame.
"Mbegu za asili hazizai sana unakuta shina moja lina mizizi miwili au mitatu tu na kama unataka kula unakuta unang'oa mashina matatu mpaka nne ndiyo unapata chakula cha siku moja tu lakini hizi mbegu bora shina moja unaweza kula na familia siku mbili mpaka tatu, ndiyo ubora wake zaidi," amesema.
Mtafiti wa Mazao ya Mihogo na Jamii ya Viazi kutoka TARI Naliendele Festo Masisila amesema Taasisi hiyo imetafiti na kuzalisha mbegu bora zaidi ya nane kwa Kanda ya Kusini ili kukuza kilimo cha zao la Mihogo nchini.
Amesema mbegu hizo zina sifa nyingi za manufaa kwa wakulima ikiwemo kuzaa kwa wakati, zinazaa kwa kiwango kikubwa, kuhimili magonjwa pamoja na ukame.
"Mbegu hizi zina sifa nyingi lakini kwa uchache, moja zinazaa kwa wakati, ndani ya miezi tisa mpaka 12 zinakuwa zimeshakomaa vizuri kabisa kwa ajili ya matumizi ya aina yoyote," amesema.
Amesema mbegu hizo bora zinazaa tani 10 na zaidi kwenye hekari moja ikilinganishw na mbegu za asili ambazo zinazaa kuanzia tani 3 kwenye hekari moja.
Masisila amesema Mbegu hizo bora zinaweza kupandwa wakati wowote badala ya kusubiria msimu kwa sababu zinahimili ukame.
Amesema licha ya kuwa na teknolojia mpya ya mbegu, teknolojia nyingine ni kupanda kwa awamu, mkulima anaweza kupanda mara tatu mpaka mara nne Kwa msimu mmoja.
"Anaweza (Mkulima) kupanda kwa mfano mwezi wa 11 ambapo mvua za kwanza zinaanza, mwezi wa 12 mwishoni, mwezi wa Kwanza na wa pili na mwezi wa tatue bado anaendelea kupanda na akavuna mazao mfululuzo bila kutegemea msimu," amesema.
Aina ya mbegu bora ambazo zinafanya vizuri ni TARICASS 1, TARICASS 2, Kiroba, Chereko, Kipusa.
Mtafiti wa Mazao ya Jamii ya Mihogo na Viazi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) kituo cha Naliendele aking'oa Mihogo katika shamba la Majaribio Kata ya Kiwalala Wilaya ya Mtama Mkoani Mtwara.
Mkulima wa Mihogo kijiji cha Maumbika Kata ya Kiwalala, Mtama Mkoani Lindi Azizi Nungu (Kulia) akiangalia Mihogo aina ya mbegu bora ambayo imevunwa kutika Shamba Darasa la TARI Naliendele kijiji cha Maumbika
Mtafiti Msaidizi wa Kilimo kutoka TARI Naliendele Dwasi Gambo (Katikakati) akifurahia ujazo (uzito) wa Mihogo aina ya mbegu bora katika shamba darasa Kijiji cha Maumbika Mtama
Mihogo aina ya mbegu bora ya TARICASS
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...