Na.Mwandishi Wetu-DODOMA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof. Adolf Mkenda ametoa wito kwa watahiniwa wanaoanza mitihani kuzingatia masharti na taratibu zote za mitihani. 

Waziri Mkenda ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akitoa salamu za kheri kwa watahiniwa hao ambapo amesema kutozingatia taratibu hizo kunaweza kupelekea kufutiwa matokeo.

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaojihusisha na wizi na udanganyifu wa mitihani na kuwataka walimu, wasimamizi, wazazi na walezi kwa pamoja kuhimiza watahiniwa kufuata masharti na taratibu za mitihani zilizowekwa.

"Tutakosea sana tukifumbia macho suala la wizi na udanganyifu wa mitihani, kufumbia macho au kunyamaza hakuondoi tatizo, kutokukemea na kutochukua hatua dhidi ya wizi na udanganyifu kunalea tatizo hili na kulikuza,"amesisitiza Prof. Mkenda

Amesema udanganyifu unaleta madhara ikiwemo kunaondoa haki kwa watahiniwa, kudidimiza weledi kwenye taifa na kuharibu malezi ya watoto kwa kuwafundisha udanganyifu

"Pamoja na kwamba wizi na udanganyifu wa mitihani hapa nchini ni mdogo sana ni wazi tusipoziba ufa tutajenga ukuta,"amesema Prof. Mkenda

Ameongeza "Tunao maofisa wa Serikali ambao wapo mahabusu wakikabiliwa na mashtaka ya wizi na udanyanyifu wa mitihani, zipo shule chache ambazo zimefutwa kama vituo vya mitihani kwa sababu ya wizi na udanganyifu wa mitihani kama itatulazimu tutachukua hatua kali zaidi ikiwa ni pamoja na kufuta usajiliwa shule zinazoratibu udanganyifu wa mitihani,"amesisitiza Prof. Mkenda

Prof. Mkenda ametumia nafasi hiyo kuwaomba watanzania wote kusimama pamoja na kukemea wizi na udanganyifu wa mitihani na endapo kutakuwa na dalili ya wizi au udanganyifu wa mitihani kutoa taarifa kupitia namba ya simu ya mkononi 0759 360 000 au barua pepe esnecta@necta.go.tz

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...