• Yatoa msaada kwa taasisi za elimu ya juu ili kukuza fasihi ya kiswahili
SAFAL Group, ambayo ni kampuni mama ya makampuni yake tanzu ya Alaf Tanzania na Mabati Rollings Mills ya nchini Kenya, imetimiza ahadi yake kwa kuchapisha kazi za washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika.

Mbali na zawadi ya dola 5000 zilizotolewa na Safal Group, ambazo kila mshindi wa kwanza katika kipengele cha Riwaya na Ushairi alipata kama zawadi na zawadi ya dola 2500 ambazo zilikwenda kwa washindi wa pili wa kila kitengo, kampuni hiyo huchapisha kazi za washindi kila mwaka kama njia ya kukuza fasihi ndani ya ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Meneja Unadi wa Alaf Tanzania, Salwa Omari, alisema nakala 2000 za kazi za washindi zilichapishwa na zitasambazwa kwa taasisi mbalimbali za elimu ya juu ili kukuza fasihi na kujenga utamaduni wa kusoma miongoni mwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya elimu ya juu.

Ameyasema hayo wakati alipokuwa akikabidhi vitabu 200 kati ya 2000 kwa maktaba ya Chuo Kikuu Dar es Salaam na kuongeza kuwa watatoa msaada kwa taasisi nyingine za elimu pia.

Omari amesema ALAF Limited inatambua thamani ya Kiswahili kama sehemu muhimu ya utambulisho wa Tanzania, huku wakiamini kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina mchango mkubwa katika kuendeleza masomo ya kitaaluma na utafiti wa Kiswahili.

Amesema wamechapisha nakala 500 kwa kila mshindi kati ya washindi wane wa tuzo za mwaka 2022 na wametoa nakala 50 za kila mtunzi kwa UDSM peke yake.

Watunzi hao pamoja na machapisho yao ni pamoja na, Halfani Sudy- Kirusi kipya, Idrissa Haji Abdalla- Kilio cha Mwanamke, John Wanyonyi- Safari ya Matumaini na Lucas Lubango-Bweni ya Wasichana.

Ameendelea kusema kuwa Safal Group imejitolea kutangaza na kukuza fasihi hapa nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla na ndiyo sababu halisi iliyoipelekea kampuni hiyo kufadhili hafla hiyo kila mwaka sambamba na Kituo cha Mafunzo ya utamaduni wa Kiafrika kilichoko katika Chuo Kikuu cha Cornell kilichoko nchini Marekani na taasisi ya wakfu wa Ngugi wa Thiong’o (Ngugi wa Thiong’o Foundation). “Mchango huu unalenga kuimarisha uhusiano wetu na kuchangia katika uboreshaji wa kitaaluma na kitamaduni wa tasnia ya Kiswahili,” alisema

Vitabu hivyo vilichapishwa na kampuni ya Mkuki na Nyota, ambayo ni moja ya makampuni maarufu ya uchapishaji nchini na ndio mchapishaji maalumu wa kazi za washindi wa tuzo hizo.

Akizungumza baada ya kupokea vitabu hivyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam-Utafiti Prof. Nelson Boniface alitoa shukrani kwa uongozi wa makampuni ya Alaf Tanzania na Mabati Rolling Mills kwa kuandaa tuzo hizo kila mwaka, jambo ambalo walisema linatoa fursa kwa watu mbalimbali wakiwemo wanafunzi kujisomea na kujifunza kupitia kazi zinazochapishwa na zitakazochapishwa.

“Tuzo hizi pia zitawawezesha washindi mapato wanapata mapato kutokana kazi zao nzuri walizofanya; tuzo hizi pia zinawapa ari wanafunzi ya kuzalisha maudhui mengi ambayo pia yatatumiwa na umma,” alisema.

Ametoa wito kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam kutumia vyema vitabu walivyokabidhiwa ili kuimarisha ujuzi wao wa fasihi na ili waweze waje kuwa waandishi wazuri hapo baadaye.

Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ilianzishwa mwaka wa 2014 na Dkt. Lizzy Attree na Dkt. Mukoma wa Ngugi kwa lengo la kutambua kazi za uandishi wa lugha mbalimbali za Kiafrika na pia kuhimiza tafsiri ya lugha hizo kutoka lugha moja ya kiafrika kwenda lugha nyingine Barani Afrika.
Meneja Mradi wa Kampuni ya Alaf Tanzania, Salwa Omari (wa nne kushoto) akikabidhi msaada wa vitabu 200 ambayo ni machapisho ya miswada ya washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika 2022 kwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam- Utafiti, Prof. Nelson Boniface kama msaada kwa maktaba ya chuo. Wengine kutoka kushoto ni Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dr. Mussa Hans, mmoja wa waandishi wa vitabu Hafidh Kido, mwakilishi wa maktaba ya UDSM Magreth Bwathondi, Mkurugenzi TATAKI Prof. Shani Omari Mchepange na Afisa Uhusiano wa Alaf, Theresia Mmasy.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...