Na. Dennis Gondwe, DODOMA

KAMATI ya Usalama ya Wilaya ya Dodoma imewahakikisha wananchi wa Mtaa wa Kizota Relini kuwa hakuna tukio lolote la uvunjifu wa amani litakaloruhusiwa kutokea katika eneo hilo kufuatia mgogoro wa ardhi uliodumu zaidi ya miaka 10.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Wilaya ya Dodoma, Godwin Gondwe alipokuwa akiongea na waandishi wa habari baada ya kikao cha ndani na viongozi wa wananchi wa eneo la Muhuji katika Mtaa wa Kizota Relini jijini hapa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Gondwe ambae ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma alisema “niwahakikishie wananchi wa eneo la Muhuji katika Mtaa wa Kizota Relini kuwa kuna usalama wa kutosha katika eneo hilo. Hakuna mwananchi atakayesumbuliwa kwa namna yoyote. Dodoma ni salama na ina amani na waandishi wa habari mnafahamu serikali ipo macho na haitakubali kuona mtu yeyote anayewakosesha amani wananchi”.

Akiongelea utatuzi wa mgogoro wa ardhi katika eneo hilo, alisema kuwa uongozi wa wilaya na halmashauri una jukumu la kutatua migogoro ya ardhi. “Leo tupo hapa kwa ajili ya kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 10. Tumekutana na makundi yote yanayohusika na mgogoro huu. 

Tumetengeneza timu ya wananchi watano waliopendekezwa na wananchi wenyewe ili kuweza kuutatua. Tumekaa hapa na Mstahiki Meya Prof. Davis Mwamfupe na Mkurugenzi wa Jiji John Kayombo. Tumetoa siku saba kufuatilia historia ya mgogoro huu na kuutatua. 

Kundi la kwanza tutakutana nalo kesho saa 2 asubuhi na kundi la pili tutakutana nalo saa 5 asubuhi. Jiji la Dodoma hatutaki kuzalisha migogoro ya ardhi, muelekeo wa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais ni kumaliza migogoro ya ardhi Dodoma.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Makazi katika eneo la Muhuji, Simba Shaban alisema “nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwaona ninyi na kuwateua kuja kumsaidia ndani ya Wilaya ya Dodoma. Niwapongeze kwa moyo wa utashi na ubinadamu wa kutusikiliza”.

Wananchi wa eneo la Muhuji katika Mtaa wa Kizota Relini walikumbwa na taharuki baada ya kuona askari wakitekeleza majukumu yao ya kulinda amani katika eneo hilo kufuatilia mgogoro wa ardhi uliodumu zaidi ya miaka.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...