*Asema wanaopinga wamenunuliwa, wana maslahi binafsi
*Asema wanaonufaika na mfumo uliopo sasa hawawezi kukubali
*Asisitiza yuko tayari kujibu kipengele baada ya kipengele
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MBUNGE wa Jimbo la Ukonga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Jerry Silaa ameishauri Serikali kuharakisha uwekezaji wa DP World katika Bandari ya Dar es Salaam ili wananchi waone manufaa yake.
Aidha amesema wanaopinga na kupotosha kuhusu uwekezaji huo wana maslahi binafsi na wamenunuliwa na ajenda yao kubwa ni kumtoa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye reli ya kuendelea kuleta maendeleo ya wananchi.
Pamoja na hayo ametoa rai kwa wananchi kuendelea kusikiliza mijadala inayoendelea kuhusu uwekezaji wa DP World lakini akiwatahadharisha kuwa makini na wapotoshaji ambao nia yao ni kukwamisha uwekezaji katika bandari hiyo kwani wananufaika na mfumo uliopo sasa.
Akizungumza leo Julai 12,2023 Jerry Silaa amesema ameamua kujitokeza kwa mara nyingine kuzungumzia suala hilo kwasababu ameona kuna upotoshaji mkubwa ambao unaendelea kufanywa na baadhi ya watoa maoni wenye ajenda zao binafsi.
“Nitoe rai kwa Serikali kuharakisha mchakato wa uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam kwani kwa jinsi ambavyo mjadala unakwenda hautaisha.Tunataka uwekezaji uanze ili wananchi waone kwa macho yale ambayo tunayazungumza , kama kontena waone ambavyo zinatumia muda mfupi kukaa bandarini, kama meli inakuja waone ambavyo kontena zinapakuliwa kwa haraka.”
Amefafanua uwekezaji umelenga kuboresha utendaji wa bandari ambao kwa sasa haukukidhi viwango na hivyo kusababisha meli zinapokuja zinaka kuanzia siku tano, 10 hadi 15 na kila inavyokaa kuna fedha ambayo mwenye mzigo analipa kuanzia Sh.milioni 60,000 mpaka Sh.milioni 90,000.
Hata hivyo amesema kuna biashara za watu bandarini ambao hawawezi kufurahia uwekezaji unaotaka kufanywa na Serikali na hao ndio wamekuwa wakieneza upotoshaji ili kukwamisha.
Amesisitiza kwamba kushusha kontena inachukua siku tatu hadi nne, kushusha kichere siku sita hadi 10, kutoa mzigo ni saa 12 na katika urasimu wote huo wapo watu wananufaika.
“Kutokana na mifumo ya bandari iliyopo hivi sasa kutokukidhi mahitaji akitokea mtu anayehitaji mzigo upeleke Congo kwa kupitia bandari ya Dar es Salaam ni rahisi kujua meli itatoka lini China na kufika Dar es Salaam lakini kuhusu majibu ya mzigo wake utatoka lini hakutakuwa na majibu.”
Pia amesema katika mchakato wa uwekezaji huo wapo washindani ambao nao wanaona kabisa bandari ya Dar es Salaam ikiboreshwa wao hatakuwa na nafasi hivyo huenda nao wako nyuma kukwamisha.
“Kupitia uwekezaji huo urasimu huo utaisha, kuanzia muda wa meli kusubiri, kushusha mizigo, na hadi kutoa mizigo hali ambayo itavutia wafanyabiashara kutumia bandari zetu ambapo kwa sasa wanakimbilia bandari nyingine za nchi jirani zisizo na urasimu.
“Narudia tena kutoa mwito kwa Serikali kwenda kwa kasi katika utekelezaji wa mkataba huo ili watanzania wajionee kwa macho faida zake, “amesema na kuongeza amepitia vipengele vyote vya IGA hakuna matundu yoyote na kama kuna mtu ana hoja basi aoneshe mahali ambako ana mashaka nako ili ajibiwe.
Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa asitokee mtu yoyote akasema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia inakurupuka katika kuingia mikataba.
“Serikali iko makini na hata mkataba wa awali wa mahusiano kati ya Tanzania na Dubai unaozungumzia uwekezaji bandari ya Dar es Salaam umepitiwa kipengele kwa kipengele.,”
Ameongeza kwenye mjadala wa suala hilo hata wanasheria wanazitumia taaluma vibaya kwani hakuna hata mmoja ambaye anajikita katika vipengele vya kisheria vya mkataba huo baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai Zaidi ya kufoka na kugonga meza kutokana na maslahi yaliyokuwa nyuma yao.
Hata hivyo amesema kilichoiingiwa baina ya nchi hizo mbili si mkataba wa utekelezaji bali ni hatua ya awali na yeye kama mwanasheria aliyepata nafasi ya kuupitia vizuri haoni kama kuna makosa ya kisheria.
“Mkataba unatoa fursa iwapo mwekezaji atahitaji kufanya jambo lolote atatakiwa kuwasilisha maombi Serikali.Wenye wasiwasi na usalama , ukweli suala la usalama wa bandari liko kwa mujibu wa sheria za nchi na ndio maana kuna polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
“Je bandari itabinafsishwa ,jibu ni hapana hakuna mahali kokote ambako kunaeleza kwamba mkataba huo unakwenda kubinafsisha bandari,Bandari ya Dar es Salaam itaendelea kuwa chini ya Usimamizi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na sio vinginevyo kama baadhi ya watu wnavyopotosha.
“Suala la mapato na forodha yote yapo chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Serikali inafanya uwekezaji kwa kuwa hali iliyopo bandarini na haikidhi viwango vya kimataifa,”amesema.
Ametumia nafasi hiyo kueleza sio mara ya kwanza Serikali kutoa nafasi kwa sekta binafsi kutekeleza baadhi ya mambo ndio maana hata uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuna kampuni binafsi kama Swisport ambayo inatoa huduma na wala hakuna anayehoji.
“Tunakumbuka ambavyo wakati Serikali inataka kubinafsisha Benki ya NMB lakini leo wote tunashuhudia faida zake, hivi karibuni Serikali imepokea gawio la Sh.bilioni 45.5 na wote tunafurahia.
“Uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam umezingatia mahitaji ya kiuchumi lakini hata maelekezo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ukurasa wa 92 ibara ya 59 na ibara ya 9b na Ibara 14 unaihimiza Serikali kushirikiana na sekta binafsi katika uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Pamoja na hayo amesema katika kujadili suala hilo watu wanapaswa kujikita katika kujibu hoja kipengele kwa kipengele badala ya kushambulia watu na kuendelea kupotosha ukweli wa jambo hilo aidha kwa kutojua au kwa makusudi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...