Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MICHUANO ya Kimwanga CUP iliyoanza Machi mwaka huu kwa timu 20 za kata ta Makurumla jijini Dar es Salaam kuchuana katika hatua ya makundi hadi fainali imekamilika rasmi huku timu ya soka ya Mingle FC kutoka Mtaa wa Kilimahewa kuibuka kidedea katika fainali ya michuano hiyo baada ya kuichabanga timu ya Ting Wayland 2-0.
Katika fainali ya michuano hiyo iliyoteka hisia za mashabiki lukuki wa soka katika Kata ya Makurumla pamoja na kata jirani zilizopo katika jimbo la Ubungo mbali ya kujitokeza mamia ya wananchi kushuhudia mtanange wa timu hizo zilizotinga fainali, mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Abass Mtemvu.
Wengine waliohudhuria fainali za mashindano hayo ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo Profesa Kitila Mkumbo, viongozi wa ngazi mbalibali wa chama na Serikali katika Wilaya ya Ubungo na Mkoa wa Dar es Salaam huku Kata ya Makurumla wakiongozwa na Diwani wa Kata hiyo Bakari Kimwanga ambaye ndiye aliyeandaa mashindano hayo.
Mchezo wa fainali ya mashindano ya Kimwanga CUP, ulitanguliwa na mchezo wa Rede ulioandaliwa na Diwani wa Viti Maalum, Hawa Abdulrahman ambapo mshindi katika fainali hizo naye alinyakua ng'ombe na wa pili mbuzi, ambapo michezo hoyo ilifanyika katika Uwanja Bubu ulioko Mtaa wa Kwa Jongo Kata ya Makurumla ambapo wananchi wameshuhudia ushindani mkali kutoka kwa timu hizo ambazo ziliingia fainali huku kila mmoja akiwa na ndoto ya kutaka kuchukua Ng’ombe.
Lakini hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika Mingle FC wakaibuka washindi na hivyo kukabidhiwa zawadi zao kama ambavyo ziliahidiwa na Diwani Kimwanga.
Akizungumza kwenye fainali hizo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Abass Mtemvu amesema kupitia mashindano ya Kimwanga CUP wao kama Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Dar es Salaam wamejiridhisha kazi inakwenda vizuri huku akihamasisha madiwani wengine kuiga mfano huo na kwamba mashindano hayo yawe chachu kwa madiwani ambao hawajaanzisha sasa waanzishe mashindano kama njia ya kukutana na watu na kuwa karibu nao.
Aidha amesema uwepo wa mashindano hayo yanakwenda kuakisi kile alichokisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alipowaalika Yanga Ikulu kuwapongeza baada ya kufika fainali ya michuano mikubwa katika Bara la Afrika.
“Rais Dk.Samia alisema amekuwa akifuatilia mashindano ya mpira mtaani yakiwemo ya Ndondo CUP pamoja na mashindano mengine ya aina hiyo yenye kuibua vipipaji. Kwa hiyo kwa Mkoa wa Dar es Salaam nami nimekuja kusimamia kauli ya Rais Samia na naona kazi ni nzuri,”amesema Mtemvu huku akitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwatumikia Watanzania sambambamba na kuboresha huduma za wananchi.
Pia ametumia nafasi hiyo kueleza michezo ni fursa na ni ajira kwani yanapokuwepo mashindano kama hayo kunafanya vijana kupata ajira kwasababu wanapocheza kwenye timu za mtaani hulipwa, hivyo hupunguza vijana kkushiriki kwenye vitendo cha kihalifu.
Kwa upande wake Mbunge wa Ubungo Profesa Kitila Mkumbo amesema mashindano ya Kimwanga CUP yeye kama mbunge wa jimbo hilo ni wajibu wake kusaidia na kuwa karibu huku akifafanua aliyazindua Machi mwaka huu na jana yamefika tamati kwa washindi kukabidhiwa zawadi.
“Baada ya kukamilika kwa michuano ya Kimwanga CUP sasa tunakwenda kujiandaa na mashindano ya Jimbo CUP yanayotarajia kuanza Agosti mwaka huu , mshindi wa kwanza na wapili wa Kimwanga Cup hao wamepata nafasi ya kwenda moja kwa moja mashindano ya Jimbo Cup yatakayokuwa chini ya uratibu wa ofisi ya Mbunge.
“Naamini kupitia mashindano ya Kimwanga Cup naona kuna mambo mengi ya kufanya hata katika kusaidia vijana na wananchi wa maeneo mbalimbali.Nitumie nafasi hii kumpongeza Diwani wa Kata ya Makurumla Bakari Kimwanga kwa kuanzisha Kimwanga Cup lakini pia Diwani wa Viti maalum wa kata hii Hawa Abdulrahman kwa kuanzisha mashindano ya Rede CUP na mshindi kupata ng’ombe kama ilivyo kwa timu za mchezo wa soka,”amesema Profesa Mkumbo.
Awali Diwani wa Kata ya Makurumla Bakari Kimwanga amemshukuru Mungu kwa mashindano hayo kufika hatua ya fainali na kukabidhi zawadi kama alivyoahidi na tangu kuanza kwa michuano hiyo wamepita kwenye milima na mabonde na kila ilipojitokeza changamoto waliitatua kwa wakati.
“Niliahidi kutoa zawadi ya ng’ombe kwa mshindi wa kwanza wa michauno hii ya Kimwanga Cup na leo nimekabidhi, niliahidi kutoa Mbuzi kwa mshindi wa pili nimetekeleza na hivyo kwangu nachukua kama chachu na changamoto zilizojitokeza tutakwenda kuzitafutia ufumbuzi ili kwenye mashindano yajayo yawe bora zaidi .
“Niwashukuru Watanzania na hasa wananchi wa Kata ya Makurumla kwa kuwa name bega kwa bega kuhakikisha kwamba mashindano haya hasa vijana wanakuwa karibu katika kuhakikisha wanashiriki kutumiza ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha sekta ya michezo pamoja na kuwa karibu na jamii nyakati zote,”amesema Kimwanga
Aidha amesema baada ya kumaliza michuano hiyo anaangalia utaratibu wa kuja na michuano mengine ikiwezekana anaweza kuja na Netball na lengo ni kuendelea kuhamasisha michezo hasa kwa jamii ya wana Makurumla kwa ujumla.
Nahodha wa timu ya Mingle FC akiwa amenyanyua kombe baada ya kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya timu ya Ting Wayland katika michuano ya fainali ya Kimwanga Cup iliyochezwa katika wa Uwanja wa Bubu uliopo Kata ya Makurumla jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Abass Mtemvu akikabidhi kikombe kwa nahodha wa timu ya Mingle FC baada ya kuibuka washindi wa fainal za Kimwanga Cup.Pia Mtemvu amekabidhi kitita cha Sh.100, 000 iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Ubungo Profesa Kitila Mkumbo( wa pili kushoto) Wa kwanza kushoto ni Diwani wa Kata ya Makurumla Bakari Kimwanga aliyeandaa mashindano hayoMwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Abass Mtemvu( katikati) akisalimiana na wachezaji wa Ting Wayland kabla ya kuanza kwa mchezo wa faina ya Kimwanga Cup iliyofanyika Uwanja wa Bububu katika Kata ya MakurumlaWachezaji wa timu ya Mingle FC wakiingia uwanjani kumenyana na timu ya Ting Wayland kwenye mchezo wa fainali ya Kimwanga Cup
Shamrashamra mbalimbali zikiendelea wakati wa mchezo wa fainali ya Kimwanga Cup iliyofanyika Uwanja wa Bubu uliopo Kata ya Makurumla jijini Dar es Salaam
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...