Na Mwandishi Wetu
MTALAAM wa magonjwa ya mama na uzazi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili(MUHAS)
Profesa Andrea Pembe amesema elimu ya Afya ya Uzazi inatakiwa itolewa mapema kwa vijana nchini ili kuondokana na tatizo la utoaji mimba usio salama.
Akizungumza hivi karibuni na vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam, Prof. Pembe amesema elimu hiyo inatakiwa kutolewa kabla ya watu hawajaanza kushiriki tendo la ndoa ili hata wakipata mimba wawe wanapata taarifa sahihi na kuepuka mimba za ujanani.
Amesema kwa sasa vijana wengi wanaanza kufanya tendo la kujamiiana wakiwa na umri mdogo kuanzia miaka 9 hadi 12 na wanavunja ungo mapema tofauti na zamani ambapo ilikuwa miaka 14 hadi 15 lakini kwa sasa imeshuka.
Amesema wakiwa na umri huo wanatakiwa wameshaanza kupewa elimu itakayowezesha kujua nini kinaweza kutokea kama wataendelea kujamiana na wavunja ungo mapema hali ya kimwili inabadilika kwa mabinti pamoja na vijana kwani wengine wanakuwa na hamu hivyo lazima wafundishwe namna ya wao kujizuia matamanio yao ya mwili.
Aidha, amesema elimu hiyo isiishie hapo tu kwa sababu inayohusu afya ya uzazi ambayo ni pana na ina vitu ni vingi na vyote walipaswa kuvifahamu ili waweze kupambana na afya zao za kila siku.
Pia, amesema suala la utoaji mimba usio salama umekuwa na madhara makubwa hasa kwa mama ambaye ametoa mimba ikiwemo kupoteza maisha kwa kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua,kuambukizwa kwa bakiteria na kupelekea mwili wake na viongo mbalimbali kushindwa kufanya kazi.
"Katika masuala ambayo utoaji mimba unaweza kuleta madhara ya muda mrefu ni pamoja na mama huyo kutopata mtoto baada ya muda mrefu kutokana na mirija yake ya uzazi kuweza kuwa imeziba na ujauzito kutofika katika nyumba ya uzazi lakini pia kutokana na utoaji wa mimba ulivyofanyika inaweza kusababisha ukuta wa nyuma wa mfuko wa uzazi kugandamana popote na mama huyo kupoteza afya yake ya hedhi hivyo kutokupata mimba tena baadae.
“Kwa ujumla katika Taifa letu la Tanzania suala nzima la utoaji mimba likojuu kama nchi nyingi za ukanda huu wa mashariki na kati ya Afrika na kuna jumla kama akina mama 36 kati ya 1000 wanakuwa wametoa mimba,” amesema Prof. Pembe.
Hivyo, amewataka mabinti pamoja na akina mama kuacha kutumia dawa pasipo kufata ushauri kwa madaktari kwa sababu zipo baadhi ya dawa ni hatari na kupelekea mfuko wa uzazi kujikunyata.
Serikali yabainisha mikakati ya kupambana na changamoto ya utoaji wa mimba usio salama
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel Juni 2023 akiwa Bungeni alibainisha juhudi zinazofanywa na Wizara ya Afya katika mapambano dhidi ya changamoto ya utoaji mimba usio salama ikiwemo, kutoa elimu juu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike ambao wapo chini ya umri wa kuzaa.
Ameendelea kusema, Wizara kupitia vitengo vyake imeendelea kutoa elimu kwa klabu za vijana na vijana balehe kutojihusisha na ngono zembe (abstinence) ili kuepuka kupata mimba zisizotarajiwa ambazo hupelekea kuongezeka vitendo vya utoaji mimba usio salama.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Wizara inaendelea kusimamia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma bila malipo ili kuwawezesha wanawake na wanaume kuzuia mimba zisizotarajiwa.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, ametoa wito kwa jamii kuhakikisha mimba zote zinapatikana kwa mpango ili kuondokana na changamoto ya utoaji mimba usio salama unaoweza kuathiri afya za wajawazito.
Pia, amewataka wajawazito kuhudhuria katika kliniki za uzazi wa mpango ili waweze kupatiwa elimu ya Afya ya Uzazi ikiwemo jinsi ya kuepukana na mimba zisizotarajiwa ili kuondokana na uavyaji wa mimba usio salama.
Masuala ya Afya ya Uzazi katika Mkataba wa Maputo
Tanzania ilikubali kusaini Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu – Mkataba wa Nyongeza wa Haki za Wanawake Barani Afrika maarufu kwa jina la MKATABA WA MAPUTO uliotungwa kuwa sehemu ya nyongeza ya Mkataba wa Haki za Binadamu na Watu wa Mwaka 1981.
IBARA YA 14 (2c) YA MKATABA WA MAPUTO
Kuna mengi ndani ya mkataba huo ambayo Tanzania imeyachukua na kuyatumia lakini kuna moja ambalo halijachukuliwa kwa ukubwa kama inavyotakiwa, suala hilo lipo katika IBARA YA 14 (2c).
Kipengele hicho kinahusu masuala ya afya ya uzazi hasa katika kutoa mwanya kwa Mwanamke kutolewa/kutoa mimba pale anapokabiliana na mazingira kadhaa ambayo yanaweza kuwa hatarishi kwake.
IBARA YA 14 YA MKATABA WA MAPUTO (2c) inatoa uwanja mpana wa kulinda haki ya afya ya uzazi kwa Wanawake, ambayo inataka Marekebisho ya sheria kuruhusu utoaji mimba kwa njia salama hasa kwa mimba zilizopatikana kama matokeo ya Ubakaji, Shambulio la kingono na Maharimu sio tu utaboresha afya ya mwili na akili miongoni mwa akina mama, lakini pia itapunguza vifo vya kina mama vitokanavyo na uzazi. Utoaji mimba usio salama unachangia kwa asilimia 19 ya vifo vitokanavyo na Uzazi, ambavyo kwa Tanzania takwimu zinaonyesha kuwa wanawake 556 hufariki kati ya vizazi hai 100,000 (TDHS, 2015-16)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...