Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) unatarajia kuzindua mpango wa usajili wa watoto wote chini ya umri wa miaka mitano bure utakaofanyika katika Uwanja wa Mayunga mkoani Kagera hapo kesho,

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi amesema mpango huo utakaozinduliwa na Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt Damas Ndumbaro unatarajia kusajili watoto laki nne na kumi na nane elfu na mia mbili na arubaini na sita (418,246) mkoani Kagera pekee.

“Mpango huu unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi sambamba na kutolewa katika vituo vyote vya tiba vinavyotoa huduma ya afya ya mama na mtoto sambamba na ofisi za watendaji kata hivyo nitoe rai kwa wakazi kujitokeza kwa wingi,,” alisisitiza Bw. Kanyusi.

Alisema maandalizi yote uzinduzi wa mpango huo yamekamilika na kutakuwa na vituo vya usajili vipatavyo mia tano na ishirini na tatu (523) ambapo kila kituo kitakuwa na wasajili wasiopungua wawili (2) waliopatiwa mafunzo maalum ya usajili na utambuzi ili kuwezesha kutimiza majukumu yao kikamilifu.

Alisema utekelezaji wa mpango huo unafanywa na RITA kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ikimo serikali ya Canada, Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) na kampuni ya simu ya TIGO ili kuhakikisha watoto wote nchini wanasajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa bure.

Bw. Kanyusi alisema mpango huo utatekelezwa katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itakuwa kusajili na kutoa vyeti kwa bakaya watoto ambao walikuwa hawajasajiliwa na hawana vyeti vya kuzaliwa na awamu ya pili itakuwa ni kusimika mfumo madhubuti ambao utawezesha kusajili na kutoa vyeti kwa watoto wote watakao zaliwa baada ya mpango huu kuzinduliwa.

“Utekelezaji wa mpango huu ni jitihada za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa watoto wote wanaozaliwa wapata vyeti vya kuzaliwa bila kikwazo chochote,” alisema.

Bw. Kanyusi alisisitiza kuwa huduma hiyo itatolewa bure kwa watoto wote chini ya umri wa miaka mitano nakuamazisha watu wengi wajitokeze zaidi ili kunufaikan na mpango huo wa usajili na kupewa vyeti bure.

“Utekelezaji wa mpango huo unaofanyika katika mikoa 23 ya Tanzania Bara na umeonesha mafanikio makubwa kwa kusajili na kuwapa vyeti vya kuzaliwa zaidi ya watoto milioni nane na laki tatu (8,300,000),” alisema.

RITA ambayo ipo mstari wa mbele kuhamasisha na kuzitangaza huduma zake mbali ya kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa inatoa huduma nyingine nyingi katika maeneo ya vizazi, ndoa, vifo na udhamini.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Frank Kanyusi, akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki kuhusu uzinduzi wa mpango wa usajili wa Watoto wote chini ya umri wa miaka mitano bure utakaofanyika katika Uwanja wa Mayunga mkoani Kagera kesho(Jumanne).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...