Na. Jacob Kasiri - Ibuguziwa Ruaha.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Veronica Kessy amesema Great Ruaha Marathon iliyofanyika mwishoni mwa wiki hii ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha ni chachu ya kuhifadhi mto Ruaha Mkuu ambao ni muhimu kwa ikolojia ya hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa Tanzania pia, ni kuhamasisha utalii wa ndani na nje ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Akiwa katika eneo la Ibuguziwa lililopo katika daraja la "The Great Ruaha River" ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha, Mhe. Kessy alisema, "lengo la mbio hizi ni kutoa elimu ya kuhifadhi mto "The Great Ruaha" na ndio maana mbio zetu zimeanzia hapa darajani ili muone ni kwa kiasi gani maji yanavyopungua katika mto huu na mnaporudi katika maeneo yenu mkawe mabalozi wazuri wa kuusemea ili kupunguza athari zinazoweza kusababisha kukauka kwa mto huu ambao ni tegemeo kwa taifa.

Aidha, kupitia mbio hizi pia, lengo letu ni kutangaza utalii ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje wanaotembelea hifadhi na hatimaye kuongeza watalii na mapato yatokanayo na watalii hao ukizingatia Hifadhi ya Taifa Ruaha inavivutio vingi na vya kipekee kwa hiyo vikitangazwa kwa njia kama hii ya Great Ruaha Marathon itavutia watalii wengi na wawekezaji wa miundombinu ya utalii, aliongeza Mhe. Kessy.

Hata hivyo, Mhe. Kessy alisema, "jambo hili tulilolifanya leo ni katika kuunga mkono jitihada kubwa za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizoziasisi za kutangaza utalii kupitia Falamu ya The Royal Tour. Hivyo nasi tumeona ni vema tuhamasishe utalii wa ndani, kwa bahati nzuri mbio hizi zimeshirikisha watalii wengi wa nje pia".

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Godwell Meng’ataki, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha alisema, "nimefurahi sana kuanzishwa kwa utalii wa Marathon ya utunzaji na uhifadhi wa Mto Ruaha uliopo hapa nyuma yetu, huu ni ujumbe muhimu sana kuufikisha kwa watanzania na wote wanaopenda uhifadhi. Mto huu umekuwa na changamoto nyingi zinazosababisha utalii wetu usiende vizuri katika hifadhi hii hasa unapokuwa umekauka".

Lakini pia tutambue kuwa mto huu ni muhimu katika taifa letu kwa ajili ya kuzalisha umeme, kilimo, ufugaji, uvuvi na utalii wa Ruaha pia unategemea mto huu, hivyo nichuke fursa ya mbio hizi kutoa ujumbe hasa kwa Nyanda za Juu Kusini na maeneo yote ya vyanzo vya maji yanayoingia mto Ruaha Mkuu kuvitunza kwa sababu mto huu una maslahi mapana kwa nchi, alisisitiza Kamishna Meing’ataki.

Pia, tumetumia mbio hizi kwa ajili ya kutalii ni matumaini yangu baada ya shamrashara za kuhitimisha mbio hizi naamini kuna watu watabaki hapa kwa ajili ya kutalii, kuona hifadhi na kufurahia vivutio vyetu, kama tunavyojua kuna utalii wa kukaa kwenye magari, utalii wa Puto, kutembea kwa miguu usiku na mchana ukiongozwa na waongoza watalii wetu mahiri na wabobezi katika kada hii ya utalii, aliongeza Kamishna huyo.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Hotel ya Kitalii ya Mabata Makali Eward Athanas, aliishukuru serikali na TANAPA kwa kukubali mbio hizo zifanyike katika Hifadhi ya Taifa Ruaha, pia amewaasa wadau wa utalii kuwekeza katika miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi na nje. Alisema kuwa kutokana na wingi wa wageni waliojitokeza kukimbia hoteli yao imejaa na wageni wengine kukosa malazi ndani ya hifadhi kulikopelekea baadhi ya wageni hao kurudi kwenda kulala mjini Iringa.

Mbio hizo za Great Ruaha Marathon zilizohusisha umbali wa kilometa 42, 21, 10 na 5 zimehudhuriwa na wanariadha 250 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania kama vile, Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Njombe na mwenyeji Iringa pia imeshirikisha watalii wanariadha kutoka nje ya Tanzania.






 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...