Tanzania na Cuba zimekubaliana kushirikiana na kuimarisha misingi ya kisiasa, ujengaji wa uwezo kwa wanasiasa vijana, sekta za elimu, afya, utalii, biashara na uwekezaji
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) alipokutana na kuzungumza na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne Vera katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
“Tanzania imekuwa ikishirikiana na Cuba kwa muda mrefu na ushirikiano baina ya mataifa haya umekuwa imara tangu ulipooasisiwa na viongozi wakuu wa Mataifa hayo Hayati Fidel Castro na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,” alisema Balozi Mbarouk.
Balozi Mbarouk ameongeza kuwa kwa sasa Cuba imeonesha dhamira ya kushirikiana Tanzania katika kuimarisha misingi ya siasa, kuwajengea uwezo wanasiasa vijana pamoja na sekta nyingine kama vile elimu, afya, na utalii pamoja na kuimarisha ushirikiano kwenye sekta ya biashara na uwekezaji
Kwa upande wake Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne Vera amesema kwamba Cuba inajivunia kuwa na uhusiano imara na Tanzania kwa takribani miaka 60.
Cuba itaendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha misingi ya kisiasa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili. “Wakati umefika sasa kwa serikali zetu mbili (Cuba na Tanzania) kuimarisha ushirikiano wake kisiasa na kuhakikisha kuwa mataifa yetu yanakuwa na misingi imara ya kisiasa, kijamii, na kiuchumi pia kwa manufaa ya pande zote mbili,” alisema Balozi Vera.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akizungumza na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne Vera walipokutana kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne Vera pamoja na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wa Cuba
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...