Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesema hakuna mwombaji wa udahili kwa masomo ya Shahada mwaka 2023/24 ambaye atalazimishwa kujithibitisha katika chuo asichokihitaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 29, 2023 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Tume ya vyuo vikuu nchini, Profesa Charles Kihampa amesema kila mtu ataenda kwenye chuo anachotaka endapo ataweza kuhimili ushindani wa chuo husika.
Pia amesema kwamba endapo kuna mwombaji atakwama katika hatua zozote wakati wa udahili au uthibitisho, wawasiliane na tume kwa kupiga simu au kuandika barua pepe.
"Uthibitisho ufanyike kupitia akaunti za kielektroniki ambazo muombaji alifungua kwa vyuo husika haufanyiki kwa simu wala kwa fomu maalum bali kuingia kwenye akaunti ambayo waliomba kudahiliwa," amesema
Pia amesema taasisi za elimu ya juu zihakikishe waombaji wanaruhusiwa kuingia kwenye mfumo sambamba na kuwakumbusha namba za siri ili kujithibitisha wao wenyewe kupitia akaunti zao.
Profesa Kihampa amesema waombaji ambao wanataka kubadili uthibitisho waingie katika akaunti zao za chuo na kufuta uthibitisho wa awali na kujithibitisha kwenye chuo kingine kule anakotaka.
"Wapo ambao wamejithibitisha kwenye chuo X lakini baadae wamebadili mawazo na kutaka chuo Y, basi watumie ujumbe wa kwenye simu afute uthibitisho wake na aende kujithibitisha katika chuo anachotaka," amesema.
Pia amesema kwa wanafunzi wanaotaka kubadili udahili wao pia wana fursa ya kufuta maombi ya awali na kutuma upya maombi yao kwa dirisha la pili.
Amefafanua mwenendo wa udahili katika vyuo hivyo unaendelea vizuri na kwamba wadau, wanafunzi na wazazi wale ambao hawakupata fursa wanatuma maombi yao na wengine wanaojithibitisha kupitia mfumo.
"Waombaji 23,387 sawa na asilimia 55 wamethibitisha kwenye chuo kimoja wapo na waombaji 43,213 walidahiliwa kwa zaidi ya chuo kimoja hivyo tunaamini mpaka Septemba watakuwa wamejithibitisha katika chuo kimoja wapo,"
Amesisitiza "Kwenye kipindi hiki kuna watu ambao sio waaminifu wanaoweza kujitambulisha kama maofisa udahili wa chuo fulani. Vyuo vyote vijitangaze kuelezea mawasiliano yao sahihi."
Amewataka waombaji wa udahili ambao wanapata mafunzo katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutokuwa na wasiwasi kwani wote watapata fursa ya kujithibitisha kabla ya mwaka wa masomo 2023/24 kuanza.
Kuhusu udahili, amesema dirisha la pili limefunguliwa Agosti 28 mwaka huu na tayari vyuo vimetangaza waliopata udahili na kwamba hadi Septemba 6, mwaka huu zoezi la udahili kwa wanaoomba na wale wanaojithibitisha kwa waliopata udahili zaidi ya chuo kimoja.
Amesema mwaka huu kuna madirisha matatu, la pili litakapokamilika vyuo vitakamilisha hadi Septemba 20 watatangaza awamu ya pili na uthibitisho utaendelea na kuanzia Septemba 25 na 26 watafungua dirisha la tatu na la mwisho kwa kalenda ya sasa.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, akizungumza na waandishi wa habari namna mwenendo wa udahili wa shahada ya kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu unavyoendelea kwa mwaka wa masomo wa 202/2024 jijini Dar es Salaam leo Agosti 29,2023
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...