Utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ndio kunakowavutia wananchi na wapinzani kujiunga kwa wingi na Chama Chama Cha Mapinduzi ili kuzidi kukiunga mkono chama hicho.
Akikabdhi kadi za CCM kwa wanachama wapya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amewataka viongozi na watendaji wote wa CCM kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri ya kukiimarisha chama, kuwaweka wanachama pamoja na kuachana na makundi ndani ya chama ambapo kufanya hivyo kutasaidia idadi ya wanachama kuongezeka na CCM kupata ushindi katika ngazi zote ifikapo mwaka 2025.
Mhe Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema sifa kuu ya kiongozi bora ni kusimamia haki na usawa kwa anaowaongoza sambamba na kutatua changamoto zinazojitokeza majimboni mwao.
Aidha ameeleza kuwa Amani na utulivu ndio nguzo kubwa ya maendeleo nchini ambapo katiba ya CCM imemtaka kila mwana CCM na mtanzania kusimamia jambo hilo.
Amesisistiza suala la kulipa ada kwa wanachama ni la lazima na wasisubiri hadi wakati wa uchaguzi ndio wakalipia ada ama kulipiwa na viongozi wao wa majimbo kwani kufanya hivyo ni kuzorotesha utendaji kazi wa chama.
Mhe. Makamu amesema lazima Viongozi wa CCM wakiimarishe Chama kwa kuwaelelza wanachama juu ya umuhimu wa kulipa ada, mahusiano mema na umoja na mshikamano ndani ya chama.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Amewataka viongozi kuwasimamia vijana waliofikisha umri wa miaka 18 kusajiliwa na kupatiwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kitakachowasaidia katika shughuli mbali mbali ikiwa ni pamoja na kujiandikosha katika daftari la kupigia kura.
Ameahidi kuwa Serikali zote mbili chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussen Ali Mwinyi zimejiwekea utaratibu wa kupokea maoni na ushauri kutoka kwa wananchi pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuahidi kuwa Serikali zitasimamia changamoto hizo ili wananchi waishi bila ya usumbufu wowote.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Sufiani Khamis amemuahidi Mhe. Hemed kuwa majimbo yote ya Zanzibar yatachukuliwa na Chama Cha Mapinduzi pasipo wapinzani kuchukua hata jimbo moja.
Nae mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Kichama Talib Ali Talib amesema nguvu ya upinzani ni ndogo sana katika Majimbo ya Jang'ombe na Malindi na ndio mana katika Jimbo la Jang'ombe hakuna bendera hata moja ya chama cha upinzani inayopepea na haitapepea kamwe.
Kwa upande wao viongozi wa Majimbo ya Jang'ombe na Malindi wamesema katika kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo miradi mbali mbali ya maendeleo imetekelezwa na mengine inaendelea kutekelezwa jambo ambalo linakifanya chama cha Mapinduzi kuzidi kukubalika hadi na wapinzani ambao kwa wingi wameshajiunga na CCM.
Wamesema hadi sasa tayari asilimia kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM umeshatekelezwa hivyo ni dhahiri kuwa Chama Cha Mapinduzi kitachukua ushindi mkubwa ifikapo mwaka 2025.
Nao wananchi wa majimbo hayo wampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa mapenzi yake kwa wazanzibari kwa kuwasogezea huduma mbali mbali karibu na maeneo yao hatua ambayo inawazidishia Imani kwa Chama Cha Mapinduzi.
Katika ziara yake hiyo ya kukiimarisha Chama na Jumuiya zake Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametembelea Jimbo la Jang’ombe na Jimbo la Malindi na amekagua miradi mbali mbali ya uwekezji, ameweka mawe ya msingi na kumeshiriki katika ujenzi wa maskani zinazojengwa katika Majimbo hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...