Mkutano wa Jukwaa la mifumo ya chakula barani Afrika umekuwa na matokeo chanya kwa upande wa program ya “Jenga kesho iliyo njema” (BBT) mara baada ya benki ya CRDB kwa kushirikiana na Mfuko wa kimataifa wa kuhifadhi mazingira (GCF) kutoa kiasi cha Dola milioni 50 zitakazotumika katika utekelezaji wa program hiyo.

Hayo yamebainika wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mpango  wa kuwezesha wavuvi nchini inayoratibiwa na benki ya CRDB tukio lililofanyika Septemba 08, 2023 ambapo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha vijana hao wanapata mtaji mara baada ya kumaliza mafunzo yao  kwa vitendo.

“Hii inamaanisha kuwa hawa wajasiriamali tunaowatengeneza kwa upande wa sekta za Mifugo na Uvuvi sasa wamepata uhakika kabisa wa kupata mikopo yao na kwa kuwa tayari wana maandiko mazuri ya biashara wataingia moja kwa moja kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hizo mbili” Amesema Mhe. Ulega.

Aidha Mhe. Ulega ametoa wito kwa benki hiyo kugeukia  upande wa tasnia ya ufugaji wa samaki ambako ameweka wazi kuwa anaamini kuna faida kubwa sana endapo wafugaji hao watawezeshwa rasilimali fedha na zana mbalimbali za kisasa za kufanyia shughuli hiyo.

““Wavuvi ni jamii iliyoonekana kuwa masikini  kuliko jamii yoyote na kwa muda mrefu wamekuwa na kipato cha chini sana lakini walichokuwa wanakosa ni namna ya kupata tija katika mnyororo wa thamani wa shughuli zao za uvuvi na mimi wakati wote nimekuwa nikiamini mnayo suluhu ya kuwaondoa wavuvi na wafugaji hawa kwenye hali hiyo kwa sababu ninaamini kabisa Mifugo na Uvuvi ni Utajiri” Ameongeza Mhe. Ulega.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB Bw. AbdulMajid Nsekela amesema kuwa mikopo yenye masharti nafuu itawapa fursa vijana hao kujipanga kwani ina muda mrefu zaidi wa matazamio kuliko aina nyingine zote za mikopo inayotolewa na benki hiyo.

“Vijana watapata muda usiopungua miaka 3 ya matazamio mara baada ya kuchukua mikopo hii hivyo tunaamini kipindi hicho kinatosha kwa wao kufanya shughuli zao na kuanza kupata faida itakayowawezesha kuanza kuirejesha” Amebainisha Bw. Nsekela.

Mpango wa mikopo kwa wavuvi uliozinduliwa leo utawanufaisha wavuvi waliopo kwenye vyanzo vyote vya maji ya asili kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar ambapo vikundi vya vijana na wanawake watapatiwa mafunzo yatakayowawezesha kuainisha aina ya zana wanazotaka kukopeshwa.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...