Na Mwandishi Wetu,


Benki ya Exim kupitia mkakati wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaojulikana kwa jina la “Exim Cares” imeshirikiana na asasi ya Asma Mwinyi Foundation katika kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa kijiji cha Tumbatu Unguja, visiwani Zanzibar ikiwa ni azma ya benki hiyo kurejesha kwa jamii.

Mradi wa maji huo ambao umefadhiliwa kikamilifu na benki ya Exim utanufaisha zaidi ya kaya 5000 ni utekelezaji wa Lengo la sita la Maendeleo Endelevu (SDG 6) linalolenga kuhakikisha upatikanaji wa vyanzo vya maji salama na usafi wa mazingira kwa wote.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika kata ya Tumbatu, Kijiji cha Kichakani visiwani Zanzibar mapema wiki hii, Meneja Masoko wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza alisema mradi huo mpya wa maji unalenga kukabiliana na hitaji kubwa la upatikanaji wa maji katika eneo hilo.

D’souza alisema mradi huo unadhihirisha azma ya benki hiyo kuendelea kuchangia miradi endelevu kupitia mkakati kabambe wa Exim Care wenye lengo la kuchochea ubunifu na kuongeza athari chanya kwa kijamii ambako benki yake inafanya kazi.

"Benki ya Exim imejitolea kujenga mustakabali wenye usawa zaidi, uthabiti na endelevu kwa jamii. Tunaamini kuwa maji ni uhai. Pia tunaamini kuwa maji safi ni muhimu kwa afya bora ndiyo maana hatukufikiria mara ya pili kushirikiana na asasi ya Asma Mwinyi Foundation ili kuhakikisha watu wa Tumbatu wanapata maji safi na salama,” D’souza alisema.

Alibainisha kuwa mradi wa maji unaofadhiliwa na benki hiyo unaonyesha dhamira ya benki hiyo katika kuleta maendeleo endelevu huku akibainisha kuwa utaleta mabadiliko makubwa kwa jamii hasa wanawake ambao siku za nyuma hawakuwa na chaguo ila kusafiri umbali mrefu kutafuta maji.

“Mradi huu utakuwa ahueni kubwa hasa kwa wanawake wanaosafiri umbali mrefu kutafuta maji. Sasa watakuwa na muda zaidi wa kushiriki katika shughuli zaidi za kuzalisha kipato zaidi kwa vile maji sasa yanapatikana kwa urahisi,” Kauthar alisema.

Kwa upande wake Sheikh wa Kijiji cha Tumbatu Omar Haji Sheha katika hafla hiyo aliipongeza Benki ya Exim na asasi ya Asma Mwinyi kwa kuanzisha mradi huo wa maji na kuongeza kuwa eneo lake lilikuwa na uhitaji mkubwa wa maji safi na salama kwa miaka mingi.

“Nachukua fursa hii kuwapongeza Benki ya Exim, wafadhili wa mradi huu pamoja na asasi ya Asa Mwinyi Foundation kwa kuanzisha mradi huu. Kiukweli umekuja wakati muafaka kwani kwa miaka mingi tumekuwa tukikabiliwa na changamoto ya maji safi na salama kwa ajili ya kunywa na kwa matumizi ya majumbani,” alisisitiza.

Aliwataka wanakijiji cha Tumbatu kutunza vizuri miundombinu ya mradi huo ili kuhakikisha mradi huo unaendelea kwa vizazi vijavyo.

Mwenyekiti wa asasi ya Asma Mwinyi Foundation Asma Ali Hassan Mwinyi wakati wa hafla hiyo alitoa shukurani kwa Benki ya Exim kwa kushirikiana na yake katika utekelezaji wa mradi wa maji.

“Dhamira yetu ya kuwapa fursa wakazi wa kijiji cha Tumbatu imetimia leo baada ya uzinduzi wa mradi huu wa maji. Hili lisingewezekana bila msaada wa washirika wetu Benki ya Exim,” alisema.

Meneja Masoko wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza (wa pili kushoto) na Mwenyekiti wa asisi ya Asma Mwinyi Foundation, Asma Ali Hassan Mwinyi (wa pili kulia) wakimsaidia mkazi wa Tumbatu kubeba ndoo ya maji wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama unaofadhiliwa na Benki ya Exim ambao utanufaisha zaidi ya kaya 5,000 katika kijiji cha Tumbatu Unguja, visiwani Zanzibar.
Meneja Masoko wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza (wa pili kushoto) na Mwenyekiti wa asisi ya Asma Mwinyi Foundation, Asma Ali Hassan Mwinyi (wa pili kulia) wakifungua bomba la maji kuashiria uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama unaofadhiliwa na Benki ya Exim ambao utanufaisha zaidi ya kaya 5,000 katika kijiji cha Tumbatu Unguja, visiwani Zanzibar.


Meneja Masoko wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza (wa tatu, mstari wa pili) na Mwenyekiti wa asisi ya Asma Mwinyi Foundation, Asma Ali Hassan Mwinyi (katikati mstari wa pili) katika picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa mradi wa maji safi na salama unaofadhiliwa na Benki ya Exim ambao utanufaisha zaidi ya kaya 5,000 katika kijiji cha Tumbatu Unguja, visiwani Zanzibar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...