Mkuu wa wilaya ya Temeke mheshimiwa Mobhare Matinyi alipokea vifaa vya kufanyia usafi kutoka kwa mmoja wa wadau wa Mazingira kutoka taasisi ya TIRIMA kuunga mkono zoezi la wiki ya usafi lililozinduliwa leo katika kata ya Kurasini.Katikati ni Mkurugenzi wa manispaa ya Temeke ndugu Elihuruma Mabelya

Mkuu wa wilaya ya Temeke mheshimiwa Mobhare Matinyi (katikati waliokaa)akiwa pamoja na wawakilishi  wa Chama cha TEJA(Temeke Jogging Association) mara baada ya zoezi la uzinduzi wa wiki ya usafi lililofanyika kata ya Kurasini leo.Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Elihuruma Mabelya na kulia ni Diwani wa kata ya Kurasini Mhe.Arnold Peter

Baadhi ya wananchi na wadau wa usafi walojitokeza katika uzinduzi wa wiki ya usafi wilayani Temeke iliyozinduliwa leo na mkuu wa wilaya hiyo Mhe.Mobhare Matinyi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani itakayoadhimishwa Septemba 16,2023.


Na Khadija Kalili , Michuzi Tv

MKUU wa Wilaya ya Temeke Mhe. Mobhare Matinyi, amewataka wananchi kuweka juhudi katika usafi na utunzaji wa mazingira ili kuokoa fedha nyingi zinazotumika kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa na uchafu badala ya fedha kupelekwa kwenye miradi mingine ya maendeleo.

DC Matinyi amesema hayo leo Septemba 11, 2023 wakati akizindua wiki ya usafi kuelekea kilele cha Siku ya Usafi Duniani itakayoadhimishwa September 16 mwaka huu.

Mhe. Matinyi amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kufanya usafi  kwenye  miundombinu iliyochafuliwa na wananchi kwa makusudi wakati fedha hizo zingekwenda kusaidia sehemu nyingine muhimu kama afya, elimu na kadhalika. 

"Mfano mmoja ni mfereji mkubwa wa Kiwanda  cha Serengeti unaopita katika Kata ya Keko, uliojengwa kwa Tshs. Bil.18 bila kujumlisha fedha za kuwafidia watu waliobomolewa maeneo yao, Manispaa imetumia milioni 15 kuuzibua na kuusafisha wakati fedha hizo zingeweza kununulia mahitaji hospitalini badala yake tunalipia kijiko kiingie kutoa takataka nje hii inasikitisha sana" amesema.

Hali kadhalika ametoa wito kwa wananchi wa Temeke  kuhakikisha wanapendezesha mandhari ya Temeke na amewataka   wajasiriamali kuondoka barabarani  walikozagaa na kwenda kwenye maeneo rasmi yaliyopangwa kufanya biashara zao. 

Uzinduzi huo umefanyika katika Kata ya Kurasini kwenye eneo la Mama na Baba Lishe TRH na kushuhudiwa na Katibu Tawala wa Wilaya Nicodemus Tambo , Mstahiki Meya Abdallah Mtinika, Naibu Meya Arnold Peter ambaye pia ndiye Diwani wa Kata ya Kurasini, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Elihuruma Mabelya pamoja na Wakuu wa vitengo na Idara wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.

Aidha wadau mbalimbali wa usafi na Kampuni na Taasisi kadhaa nao waliungana na wananchi kufanya usafi na baadaye kupata stafutahi kutoka kwa Mama na Baba Lishe hao waliohimizwa kujali usafi.

Mwisho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...