Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza leo Septemba 3, 2023, jijini Dar es Salaam wakati wa kuwasilisha maazimio 21 ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mtaa 2024 na uchaguzi Mkuu  2025. Kushoto ni Mkurugenzi wa TCD,  Bernadetha Kafuko.
Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza leo Septemba 3, 2023, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TCD, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema maazimio hayo yamejikita haswa kwenye mabadiliko ya katiba na sheria.
 Mkurugenzi wa TCD,  Bernadetha Kafuko katikati akizungumza leo Septemba 3, 2023, jijini Dar es Salaam wakati wa kuwasilisha maazimio 21 ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mtaa 2024 na uchaguzi Mkuu  2025.


Baadhi ya wawakilishi wa vyama vya siasa nchini wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari wa kuwasilisha maazimio ya TCD.

Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
KITUO cha Demokrasia Tanzania(TCD) kimetoa maazimio 21 yenye lengo la kukuza Demokrasia nchini na kuhakikisha kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025 unakuwa wa amani, huru na haki.

Akizungumza leo Septemba 3, 2023, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TCD, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema maazimio hayo yamejikita haswa kwenye mabadiliko ya katiba na sheria.

Pia amesema maazimio hayo yamejikita katika Ushirikishwaji wa makundi maalumu katika siasa, demokrasia ndani ya vyama vya siasa, elimu ya uraia, haki na Uhuru katika mifumo ya kidemokrasia.

Maazimio hayo ni matokeo ya mkutano wa siku mbili juu ya hali ya Demokrasia nchini Tanzania kuelekea Uchaguzi wa serikali za Mtaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam Agosti 22 na 23, 2023.

Maazimio ni hayo ni yafuatayo;
1. Kuhusu swala la katiba: Mchakato wa kupata katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi ukwamuliwe na hatimaye tupate Katiba yenye misingi imara ya demokrasia.

2. Hata hivyo Mkutano umebaini kuwa serikali imechelewa kuanzisha mchakato wa kukamilisha upatikanaji wa katiba mpya. Inaweza isiwezekane kukamilisha zoezi la kupata Katiba mpya kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025. Hivyo basi tunahitaji haraka iwezekanavyo mabadiliko madogo ya Katiba ya sasa ili yaruhusu uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi na marekebisho mengine ya kikatiba ya kuwezesha uchaguzi huru na haki na ushiriki mpana wa demokrasia.

3. Mabadiliko madogo ya Katiba yanayohitajika yanakaribiana na yale Rais wa awamu ya nne Dr Jakaya Mrisho Kikwete alikubaliana na Viongozi wa TCD mwaka 2014 Mjini Dodoma. Makubaliano hayo yalizingatia kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya hautakamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, hivyo basi katiba ya 1977 ifanyiwe mabadiliko kuruhusu;

i) uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi itakayosimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Tanzania Bara na Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano. TAMISEMI isisimamie uchaguzi wa serikali za mitaa.

ii) Kuruhusu Mgombea Binafsi asiyedhaminiwa na Chama cha Siasa.

iii) Rais atatangazwa kashinda kama atapata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote halali zilizopigwa. Ikiwa hakuna mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote, Uchaguzi utarudiwa na utakuwa na Wagombea wawili walioongoza kwa kura nyingi.

iv) Uchaguzi wa Rais uweze kuhojiwa Mahakamani.

4. Mfumo wa Tume Huru ya Uchaguzi uliwekwa ndani ya Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba na umefafanunuliwa katika Randama ya Rasimu ya Katiba. Katiba Inayopendekezwa imechukua baadhi ya mambo yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba. Mapendekezo ya Kikosi Kazi yana mfumo bora zaidi wa taratibu za kuunda Tume Huru ya Uchaguzi ukilinganisha na Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba na Katiba Inayopendekezwa. Muswada wa Tume Huru ya Uchaguzi urejee mapendekezo ya Kikosi Kazi na maoni ya wadau wengine yaliyowasilishwa kwa Serikali.

5. Muswada wa Mabadiliko ya Katiba upelekwe pamoja na Muswada wa Tume Huru ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria Mpya ya Uchaguzi katika Bunge lijalo kama ilivyofanyika mwaka 1992, wakati wa kurudisha vyama vingi, kwani muda uliobaki kuelekea uchaguzi ni mfupi. Mkutano wa kitaifa wa Maridhiano, Haki na Amani uliofanyika Aprili, 2022 jijini Dodoma ulijadili na kuwasilisha Serikalini Muswada wa mfano wa Sheria ya Uchaguzi itakayoimarisha uwepo wa uchaguzi huru na wa haki.

6. Mabadiliko ya sheria ya uchaguzi yaondoe gharama za kifedha wanazotakiwa kutoa wagombea ili kuteuliwa kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi.

7. Muda wa Tume Huru ya Uchaguzi kuandaa uchaguzi ni mfupi sana. Serikali ikubali kupokea misaada ya kuimarisha utendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi toka Washirika wa Maendeleo kama vile UNDP na wengine.

8. Serikali na vyama vya siasa kwa upande wa Zanzibar viendeleze utashi wa kisiasa katika utekelezaji na kudumisha dhana ya maridhiano kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.

9. Zanzibar pia inahitaji uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi na Uchaguzi ufanyike siku moja na siyo siku mbili kama ilivyokuwa 2020. Wadau wa demokrasia waandae na kufanya mkutano wa hali ya demokrasia kwa upande wa Zanzibar ili kudumisha dhana ya maridhiano na utatuzi wa changamoto kwa pamoja katika kuelekea uchaguzi wa 2025.

10. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, katika kukuza vyama vya siasa na demokrasia, iendelee kutoa elimu na uhamasishaji juu ya kuzingatia sheria zinazosimamia vyama vya siasa. Hata hivyo kuna umuhimu wa kuifanyia mabadiliko sheria ya Vyama vya Siasa ya 2019 ili kupanua uhuru na demokrasia ya Vyama vya Siasa. Mkutano wa kitaifa wa Maridhiano, Haki na Amani ulijadili na kuwasilisha Serikalini Muswada wa mfano wa Sheria ya Vyama vya Siasa. Muswada huu utarahisisha kazi ya kuandaa Muswada utakaopelekwa Bungeni.

11. Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa yaweke ulazima na kiwango cha uwakilishi wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika nafasi za uongozi na vyombo vya maamuzi ndani ya vyama vya siasa.

12. Mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa na uchaguzi yahakikishe yanaondoa vikwazo kwa asasi za kiraia kutoa elimu ya uraia na mpigakura.

13. Serikali itoe ratiba inayoainisha kila hatua na tarehe za matukio muhimu ya mabadiliko ya Katiba, sheria ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi, na sheria ya Vyama vya Siasa.

14. Wadau wa demokrasia waendelee na kusimamia utolewaji wa elimu ya uraia kwa jamii ili kuweza kujenga utamaduni wa mijadala kwa kujenga hoja. Hii iwe ndiyo msingi wa kuwaandaa Watanzania katika michakato mbalimbali ya kushiriki na kujenga demokrasia nchini.

15. Serikali iwezeshe na kusaidia majadiliano baina ya vyama vya siasa, asasi za kiraia na mashirika ya kiserikali ili kuhakikisha mtazamo wa pamoja katika kujenga dhana ya ushirikiano wa “kushindana kwa hoja bila kupigana” kuelekea chaguzi za 2024 na 2025.

16. Serikali ifanyie marekebisho sheria ya Utumishi wa Umma ambayo inamtaka aliyeteuliwa na Tume ya Uchaguzi kama mgombea kuacha kazi. Sheria hii imekuwa na athari kubwa kwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

17. Serikali ianzishe mchakato wa mabadiliko ya sheria ya Jeshi la Polisi ili iweze kuendana na dhana ya demokraisa ya ushindani kwani limekuwa likilalamikiwa na vyama vya siasa pamoja na wadau wa demokrasia nchini.

18. Serikali iweke mazingira mazuri kuchochea na kulinda uhuru wa kujieleza na kutoa maoni kwa wananchi, viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kiraia.

19. Vyama vya Siasa viwe na kanuni zinazoelezea na kuongoza mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi za viti maalumu vya wanawake zilizoakisi misingi ya uwazi, usawa na demokrasia.

20. Viongozi wa vyama vya siasa wajiepushe kutumia lugha za matusi, ubaguzi,udhalilishaji, upotoshaji na kubeza katika kutimiza malengo yao ya kisiasa. Baadala yake wajikite kunadi sera zao kwa kujenga hoja na kutumia lugha zenye staha.

21. Fedha zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya elimu kuhusu katiba ya mwaka 1977 zipelekwe kwa Asasi za Kiraia na elimu hii iwe endelevu katika mchakato mzima wa mabadiliko ya katiba. Pia taarifa ya Tume ya Jaji Warioba na viambatanisho vyake na hususan Randama ya Katiba zitumiwe katika elimu kuhusu katiba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...