Na Sweetbetter Njige, TMC 

MKUU wa Wilaya ya Temeke Mobhare Matinyi amekabidhi nepi za kisasa (pampers) kwa kina mama waliojifungua na wanaosubiri kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke kwa lengo la "kuwashika mkono" kina mama hao.

Akikabidhi nepi hizo  Matinyi ambaye aliambatana na Mbunge wa Jimbo la Temeke Dorothy Kilave pamoja na viongozi wengine wakiwemo madiwani, ameeleza nia ya dhati ya kuwapongeza wazazi waliojifungua katika hospitali hiyo na kuwatakia heri. 

"Tumekuja mahususi kwa ajili ya kuwaona kina mama waliokwisha jifungua na wanaosubiri kujifungua na tukaona tusije mkono mtupu; kwa hiyo tumeleta zawadi ya nepi za kisasa kwa watoto wachanga," amesema Matinyi.

Aliongeza: "Hii iwe zawadi kwa kina mama hawa kwani mbali ya kufanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo kwa taifa letu lakini wao ndio msingi wa maisha; wanapokuja kujifungua tunapaswa wote kama jamii kuwaunga mkono." 

Matinyi amesema  wananchi wa Temeke wanapaswa kujivunia uwepo wa wataalamu wenye juhudi na utu wanaohudumia katika hospitali hiyo kwa kuthamini jitihada zao. 

"Nitoe shukrani kwa Mganga Mfawidhi Dkt. Kimaro na timu yako kwani hospitali yetu inahudumia wananchi wengi; mnafanya kazi kubwa na tunapaswa kujivunia uwepo wa wataalamu wanaofanya kazi nzuri kwa moyo wa kujitolea," alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa  hospitali hiyo, Dkt. Joseph Kimaro, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa jitihada zake za kufanikisha upatikanaji wa msaada huo na kumuahidi kuwa watumishi wa hospitali hiyo wataendelea kutoa huduma kwa upendo na uaminifu. 

"Nikushukuru kwa jitihada ulizochukua kufanikisha upatikanaji wa msaada huu utakaowasaidia kina mama waliokwishajifungua. Hospitali hii inahudumia wananchi wa Temeke wanaokaribia 1,500,000 lakini pia inahudumia  wanaotoka maeneo ya jirani;  tutaendelea kuwahudumia kwa upendo ili waweze kurudi kulihudumia taifa," alisema Dkt. Kimaro.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke ni moja kati ya hospitali inayopokea na kuhudumia wagonjwa wengi nchini kutoka mikoa na wilaya jirani kama Mkuranga na Kigamboni.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...