Mkuu wa Mkoa wa Iringa akizungumza wakati wa uzinduzi wa Lishe ya Mifugo kutoka Yara.

Mkurugenzi wa Yara Tanzania Winstone Odhiambo akizungumza na wanahabari juu ya uzinduzi wa Lishe ya Mifugo kutoka Yara
Mkurugenzi wa Meja Agrovet Supply Majorino Yangi akizungumza ujio wa Lishe ya Mifugo kutoka Yara.
Baadhi ya wafanyakazi wa Yara wakiwa na wafanyabiashara na wafugaji mkoani Iringa.
Wafugaji na wafanyabiashara wakiwa kwenye uzinduzi huo

NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego ameisifu kampuni ya Utengenezaji na Usambazaji wa mbolea nchini ya Yara Tanzania kwa kuzindua huduma mpya nchini Tanzania ya Lishe ya Mifugo mbalimbali itakaowezesha wafugaji kuwanenepesha Mifugo Yao na kuwa kwenye ubora unaotakiwa kitaifa na kimataifa.

Alisema kuwa kampuni ya Yara ni mdau mkubwa sana wa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini na inafahamika kwa ubora wa bidhaa zake, hususan mbolea mbalimbali za kupandia na kukuzia mazao.

Aliongeza kuwa Ubora huo wa bidhaa kutoka Yara, pamoja na maarifa wanayoyatoa kila wakati kwa wakulima umeifanya kampuni hiyo kupendwa na kujikita katika mioyo ya wadau wa hii sekta muhimu hivyo basi, ni furaha kuona kwamba Yara Tanzania sasa imepanua wigo wake na kuongeza huduma mpya ya uzalishaji na usambazaji wa lishe bora kwa mifugo

."Nawapongeza sana Yara kwa uamuzi huu ambao sio tu muhimu kwa wafugaji kote nchini bali pia kwa uchumi endelevu wa taifa letu.

Dendego alisema kuhusu Lishe Mpya ya Mifugo ni dhamira ya Yara ya kutaka kuleta mageuzi chanya na dhabiti ya sekta ya mifugo.

Alisema kuwa Uzinduzi huu wa lishe mpya na bora ya mifugo ni ishara tosha kwamba Yara wanatambua mchango wa wafugaji na wavuvi katika kuboresha maisha ya watanzania na kuchangia ukuaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Alisema Serikali inatambua nafasi ya kipekee ya wafugaji katika kutekeleza mikakati ya serikali ya kuinua uzalishaji wa maziwa, nyama na mayai humu nchini.

Aidha alisema uzinduzi huu wa leo wa lishe bora ya mifugo kutoka Yara utachangia kwa kiasi kikubwa kuchochea uzalishaji wa bidhaa za ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na hata samaki.Licha ya kwamba Tanzania ni ya Tatu barani Afrika kwa wingi wa mifugo, uzalishaji wetu wa maziwa, nyama na mayai bado ni wa kiwango duni sana kutokana na sababu mbalimbali.

"Uchangiaji wa sekta ya mifugo katika ukuaji wa uchumi wetu kwa kiwango cha 7% ya pato la taifa pia ni wa chini mno. Hivyo basi juhudi za pamoja kati ya sekta ya umma na binafsi zinahitajika kukuza uzalishaji na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni" Alisema

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Yara Tanzania, Winstone Odhiambo alisema kwamba kampuni hiyo inayojihusisha na uagizaji na usambazaji wa mbolea hapa nchini hadi sasa ni kampuni tanzu ya Yara International ASA , ambayo inaongoza katika uzalishaji wa mbolea duniani na katika masuala ya utunzaji wa mazingira na lishe.

Alisema kampuni Ina Lengo la kuwawezesha wafugaji kupitia utoaji wa bidhaa mpya za lishe bora ya wanyama mifugo ambazo zitabadilisha sekta ya mifugo na uvuvi nchini na kuongeza kuwa bidhaa hizi za kulisha wanyama zitakazopatikana kupitia mtandao wa wakala wasambazaji wa Yara Tanzania nchini zitasaidia mamilioni ya wafugaji wa Wanyama kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na samaki ili kuongeza faida zao kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa.

"Yara International inazalisha bidhaa za lishe bora za wanyama ambazo leo tunazindua kwenye soko la Tanzania na Tunajisikia furaha na tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali, wafugaji na wazalishaji wa chakula cha mifugo ili kuboresha wingi na ubora wa uzalishaji wa maziwa, nyama, mayai na Samaki" alisema

Odhiambo alisema kuwa Bidhaa za Yara za lishe za mifugo zinatengenezwa kwa viwango na ubora wa hali ya juu katika kiwanda cha kisasa cha Yara nchini Afrika Kusini ambapo zitapatikana na kusambazwa nchini Tanzania kwa bei ya ushindani.

"Uzinduzi wa leo hapa Iringa ni muhimu kwa Tanzania, ukifuatia mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula la Afrika (AGRF) uliofanyika hivi karibuni Dar es Salaam ili kuhamasisha nchi za Afrika kuchukua hatua za kuhakikisha usalama wa chakula, kumaliza umaskini na kulilitea bara hili mafanikio," alisema

Aliongeza kuwa Tanzania ni nchi ya tatu barani Afrika kuanzisha lishe ya mifugo kutoka Yara International baada ya Afrika Kusini na Kenya. Bidhaa hizi zimekuwa zikitumiwa Ulaya kwa miongo kadhaa ambapo sekta ya mifugo imekua kuwa biashara ya mabilioni ya dola.

Baadhi ya wafanyabiashara walisema huduma hiyo ni muhimu kwa ajili ya kuongeza ubora kwenye Mifugo ya wafugaji.

Mmoja wa wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo Mkoani Iringa, Mkurugenzi wa Meja Agrovet Supply , Majorino Yangi alisema kuwa huduma hiyo hiyo imekuja kwenye wakati mwafaka na kuwaponyeza Yara kwa kuzindua rasmi Lishe ya Mifugo ambayo itasaidia wafugaji kukuza Mifugo Yao katika njia nyingine tofauti na awali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...