Na. Peter Haule, WF, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa Serikali inapunguza athari za changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni kwa kuongeza kiwango cha kuuza fedha hizo katika soko la fedha za kigeni.

Dkt. Nchemba amebainisha hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Mhe. Mhandisi Ezra John Chiwelesa, aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika kunusuru uchumi wa nchi kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni, hususani dola ya Marekani.

Alisema kuwa Serikali inaendeleea kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi, wa kati na muda mrefu katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni, hususani dola ya Marekani ambapo kati ya Machi 2022 na Agosti 2023, Benki Kuu ya Tanzania imeuza katika soko la fedha za kigeni zaidi ya dola za Marekani milioni 500 ili kutatua changamoto hiyo.


“Serikali inaongeza vyanzo vya upatikanaji wa fedha za kigeni ikiwemo ununuzi wa dhahabu na kutekeleza mikakati ya kuongeza mauzo nchi za nje na kuzalisha bidhaa mbadala wa zile zinazoagizwa kutoka nje ya nchi ili kuongeza fedha za kigeni”, alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alisema hatua nyingine ni pamoja na kuendelea kushirikisha benki za biashara, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, pamoja na wadau wengine katika kusimamia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya usimamizi wa fedha za kigeni hapa nchini.


Alizitaja sababu za changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni kuwa ni mgogoro wa vita kati ya Ukraine na Urusi, kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii baada ya UVIKO-19 na mabadiliko ya tabianchi.


“Sababu nyingine ni utekelezaji wa sera za fedha ambayo inalenga kupunguza ukwasi katika uchumi wa nchi mbalimbali ikiwemo Marekani ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei” alisema Dkt. Nchemba


Alisema kuwa kwa ujumla matukio hayo yameathiri mnyororo wa uzalishaji, usambazaji na uhitaji wa bidhaa na huduma katika soko la dunia.

Dkt. Nchemba alisema kuwa pamoja na changamoto zilizojitokeza, hali ya upatikanaji wa fedha za kigeni nchini imeendelea kuwa himilivu ambapo mwezi Julai 2023, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.246, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 4.7 ikilinganishwa na malengo ya miezi minne.

Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini Mhe. Jesca Jonathani Msambatavangu, alieuliza sababu za Serikali kutounganisha kodi ya mapato kwa wachimbaji wadogo wa madini na mfumo wa Mineral Market Management Information System (MMMIS), Dkt. Nchemba alisema kuwa kwa sasa, Mamlaka ya Mapato Tanzania na Tume ya Madini zimeingia makubaliano ya kubadilishana taarifa ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi.


Alisema kuwa kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuzitaka taasisi za umma kuhakikisha mifumo yote ya mapato na matumizi inasomana, Mamlaka ya Mapato Tanzania, inaendelea kuunganisha na kufungamanisha mifumo yake ya usimamizi wa mapato na mifumo ya taasisi nyingine ikiwemo mfumo wa Mineral Market Management Information System.
Aidha, alieleza kuwa kodi ya mapato kwa wachimbaji wadogo wa madini inakusanywa katika masoko ya madini chini ya usimamizi wa Tume ya madini kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akijibu swali bungeni jijini Dodoma kuhusu mpango wa Serikali katika kunusuru uchumi wa nchi kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni, hususani dola ya Marekani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...