*Viongozi wahudhuria sherehe maadhimisho miaka 74 kuanzishwa Jamhuri ya Watu wa China
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, January Makamba amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika sekta zote zitakazowezesha nchi hizo mbili kupata maendeleo kwa kasi kubwa.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 74 ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China Makamba aliyekuwa mgeni rasmi ameelezea kwa kina ushirikiano wa nchi hizo mbili ambao umekuwa na mafanikio makubwa kwa nchi hizo.
Akifafanua zaidi amesema safari ya China kufikia hapa ilipo imechangiwa na viongozi na wananchi wao kujituma na leo hii inasaidia nchi zingine kuendele, ikiwemo Tanzania kwamba kuna la kujifunza ili kufika ambako nchi hiyo imefika.
"China imekuwa ikisaidia nchi nyingi duniani kwenye sekta mbalimbali, hivyo ni vema kila nchi kutamani mafanikio hayo.Kitendo cha China kuwa miongoni mwa nchi zenye nguvu kubwa kiuchumi duniani ni uthibitisho wa ujasiri, dhamira, maono, uongozi, na kufanya kazi kwa bidii na dhamira isiyoyumba.
"Mchango wa serikali ya China katika kupunguza changamoto ya umaskini duniani haupaswi kupuuzwa na kwamba kwa zaidi ya miaka mingi China imetoa mchango mkubwa katika ustawi wa dunia, utulivu na kufufua uchumi wa nchi mbalimbali. Naamini kila anayetaka kujifunza anaweza kufanya kama China,"amesema
Ameongeza maendeleo ya China na watu wake ni hamasa kwetu sote na yanatoa ukumbusho wenye nguvu wa kile kinachoweza kutekelezwa na nchi tunapofanya kazi pamoja kuelekea kutimiza lengo moja.
Pia Makamba Tanzania inaunga mkono kikamilifu mpango kabambe wa Belt and Road Initiative (BRI), ambao umeonesha matokeo chanya kwa nchi husika.
Amesema mwezi ujao kutakuwa na Jukwaa la Tatu la Ukanda na Barabara kwa Ushirikiano wa Kimataifa litakalofanyika Beijing, Tanzania tutashiriki kwani mpango huu wa BRI utawezesha kuongezeka kwa biashara, kukuza uchumi wetu na kuboresha maisha ya watu wetu," amesema.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian akizungumza katika maadhimisho hayo amesema, China imeendelea kuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa Tanzania kwa miaka saba mfululizo ambapo biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia dola za Kimarekani bilioni 8.31 mwaka 2022.
Ameongeza urafiki na uhusiano kati ya China na Tanzania umekuwa ukiendelezwa kizazi hadi kizazi na unaendelea kushamiri na kumpongeza Rais Samia kufuata nyayo za watangulizi wake kuendeleza.
Amesisitiza China na Tanzania wana uhusiano na ushirikiano wa kuigwa na kutolewa mfano , lakini hali hiyo ipo kwa nchi zote ambazo zinasimamia misingi ya haki za binadamu na amani.
Balozi amesema mwaka huu pekee, wanafunzi 160 wa Kitanzania wamepata ufadhili wa kusoma China, huku wakiendelea kutoa fursa za mafunzo kwa Tanzania, yanayojumuisha fani mbalimbali kama vile elimu ya ufundi stadi.
Pia ujenzi wa miundombinu, kuondoa umaskini na uwezeshaji wa wanawake na hivyo kusaidia nchi kuibua vipaji vya taaluma mbalimbali ambavyo vinahitajika kwa haraka kwa maendeleo ya taifa.
Kuhusu hali ya uchumi wa China Balozi Chen amesema ni imara na umekuwa ukiendelea kukua kwa asilimia 5.5 kila mwaka na kufanya pato la Taifa la China kuongezeka zaidi.
"Pato la Taifa la China (GDP) limekuwa likikua kwa asilimia 5.5 mwaka hadi mwaka katika nusu ya kwanza ya 2023, na kufikia Yuan trilioni 59.3 (sawa na USD trilioni 8.24); uagizaji wa bidhaa na mauzo ya nje ulizidi Yuan trilioni 20 (sawa na dola trilioni 2.8) kwa mara ya kwanza," amesema.
Aidha kutokana nakuongezeka kwa GDP pamoja na ukuaji wa uchumi kukukua zaidi, Balozi Chen ameeleza hatua hizo zimesababisha Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kutabiri kuwa China itachangia asilimia 34.9 katika ukuaji wa uchumi wa dunia mwaka huu.
Amesisitiza jambo ambalo lilionesha kikamilifu imani ya ulimwengu katika maendeleo ya ubora wa juu ya China.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...