Na Mwandishi Wetu

WAFANYAKAZI wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) wamejitokeza katika maonesho ya sita ya teknolojia ya madini Geita na kupatiwa elimu pamoja na uchunguzi wa saratani mbalimbali.

Huduma hiyo ya elimu na uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, matiti na tezi dume inatolewa na bure na Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya GGML katika viwanja vya Bombambili vilivyopo kwenye eneo maalumu la ukanda wa uwekezaji (EPZA) mjini Geita.

Akizungumzia utoaji wa huduma hizo, Mratibu wa huduma za Tiba katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Geita, Dk. Pasclates Ijumba amesema wameamua kutoa huduma hizo ili kudhibiti madhara ya saratani hususani kwa wananchi ambao wamekuwa waoga kufanyiwa uchunguzi kutokana na na dhana potofu iliyojengeka ndani ya jamii.

Ametoa mfano kuhusu chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi ambayo hutolewa kwa mabinti wadogo, baadhi ya jamii huwazuia watoto wao kupatiwa chanjo hiyo kutokana na ukosefu sahihi wa elimu kuhusu chanjo hiyo.

“Vivyo hivyo kwa wanaume kuhusu uchunguzi wa tezi dume, wengi hudhani ni mpaka wafanyiwe kipimo kwa mtaalam kupapasa tezi dume, napenda kuwatoa hofu kuhusu hilo kwani sasa kuna kipimo maalumu cha damu badala ya kipimo cha kidole,” amesema na kuongeza baadhi ya wafayakazi hao wa GGML wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya tezi dume.

Mmoja wa wafanyakazi hao Evarist Mwanakatwe amesema wamehamasika kujitokeza kufanyiwa uchunguzi wa saratani pamoja na kupatiwa elimu kuhusu ugonjwa huo ili kuhamasisha jamii ya wana-Geita na washiriki wote wa maonesho hayo kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo kwani ni bure.

Kwa upande wake Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo wa GGML, Dk. Kiva Mvungi amesema saratani ya tezi dume inashika nafasi ya pili kwa aina ya saratani zinazowapata wanaume pia inashika nafasi ya sita kwa kusababisha vifo vitokanavyo na saratani duniani.

Amesema dalili kuu za saratani ya tezi dume kwa wanaume ni kushindwa kupata haja ndogo, kukojoa damu wakati mwingine wanapata maumivu ya mgongo na nyonga.

“Kwa hiyo idara ya afya, usalama na mazingira pamoja na idara ya mahusiano ya jamii kutoka GGML tumeandaa kampeni ya kupima saratani na kuimarisha uelewa wa masuala ya saratani” amesema na kuongeza kuwa;

“Kampeni hiyo imelenga kutoa elimu na kupima saratani kwa wafanyakazi wa GGML na jamii inayozunguka mgodi huo ili kila mtu apime afya yake na iwapo akigundulika kuwa na tatizo hilo aweze kutibiwa mapema.

Katika maonesho hayo ambayo mwaka huu yamejumuisha zaidi ya washiriki 400, yatafanyika kwa muda wa siku 10 kuanzia tarehe 20 hadi 30 Septemba mwaka huu.

Mratibu wa Idara ya Huduma za dharura kutoka GGML, Evarist Mwanakatwe akipatiwa vipimo vya saratani ya tezi dume kutoka kwa mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita. Hospitali hiyo kwa kushirikiana na GGML wanatoa huduma bure za utoaji elimu na uchunguzi wa saratani ya tezi dume, shingo ya kizazi na matiti katika maonesho ya sita ya teknolojia ya madini Geita.
Mmoja wa wanyakazi wa Idara ya Huduma za dharura kutoka GGML, Sande Misenya akipatiwa vipimo vya saratani ya tezi dume kutoka kwa mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita. Hospitali hiyo kwa kushirikiana na GGML wanatoa huduma bure za utoaji elimu na uchunguzi wa saratani ya tezi dume, shingo ya kizazi na matiti katika maonesho ya sita ya teknolojia ya madini Geita.
Mtaalam wa maabara kutoka Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita, Deogratias Keeka (kulia) akimpatia huduma za vipimo vya saratani, Dereva kutoka GGML, Andrew Elias. GGML kwa kushirikiana na hospitali hiyo wanatoa huduma bure za utoaji elimu na uchunguzi wa saratani ya tezi dume, shingo ya kizazi na matiti katika maonesho ya sita ya teknolojia ya madini Geita.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...