Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amezungumzia umuhimu wa Wizara ya Ujenzi kuendeleza miradi ya kimkakakati ya ujenzi wa barabara kwa utaratibu wa uhandisi, manunuzi ujenzi na fedha (EPC+F) na ujenzi wa miradi kwa njia ya ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP) ili kufikia matarajio ya Serikali.

Akizungumza wakati akimkabidhi Ofisi Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, jijini Dodoma, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kazi kubwa ya kuweka misingi ya kuendeleza miradi hiyo imekamilika hivyo kazi iliyobaki ni kuendelea na kasi ya uendelezaji wa miradi hiyo.

“Mheshimiwa Waziri unayo timu nzuri ya kukusaidia kufanya kazi, hivyo itumie na kuwaongezea uzoefu wa kimataifa katika kusimamia miradi ili kuiwezesha Tanzania kuendana na kasi ya mabadiliko ya miundombinu ya kidunia”, amesisitiza Profesa Mbarawa.

Amezungumzia umuhimu wa Wizara kujenga uwezo wa kutayarisha wahandisi washauri wa miradi inayotekelezwa nchini badala ya kutumia wataalamu kutoka nje ya nchi kama ilivyo sasa.

Aidha, Profesa Mbarawa amewashukuru wataalamu na watumishi wa Wizara ya Ujenzi kwa ushirikiano waliompa na kumsisitiza Waziri Bashungwa kuendeleza ushirikiano huo ili kufanikisha malengo ya Sekta.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa,  amemshukuru Profesa Mbarawa kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kutekeleza miradi mikubwa ya barabara, madaraja, nyumba na ujenzi wa wa viwanja vya ndege na kuahidi kuendeleza utamaduni huo ili kuleta tija kwa wananchi.

“Tutahakikisha msingi uliojenga tunauendeleza hususan kuongeza barabara za kisasa, nyumba za viongozi na watumishi wa umma na kuhakikisha vivivuko na utengenezaji wa magari unakuwa wa uhakika”, amesema Waziri Bashungwa.

Katibu Mkuu, Mha. Balozi Aisha Amour, amemshukuru Profesa Mbarawa kwa miongozo yake na kumuahidi kumpa ushirikiano Mheshiwa Bashungwa katika usimamizi wa miradi mbalimbali ili kuweza kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya Sita katika uendelezaji wa miundombinu nchini.

Mheshimiwa Bashungwa leo amekabidhiwa rasmi Ofisi na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Profesa Mbarawa mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Agosti 30, 2023 kuwa Waziri wa Ujenzi kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Manaibu Mawaziri na Makatibu wakuu.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (katikati) akizungumza Menejimenti ya Wizara na Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Wizara ya Ujenzi mara baada ya kukabidhi ofisi kwa Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (kushoto) leo, Septemba 08, 2023 Jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour.

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa akipokea vitendea kazi kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,  Mhe. Prof. Makame Mbarawa ambaye sasa ni Waziri wa Uchukuzi wakati wa makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika leo, Septemba 08, 2023 Jijini Dodoma.

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (katikati) akizungumza Menejimenti ya Wizara na Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Wizara ya Ujenzi mara baada ya kukabidhiwa ofisi na Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (kulia)  leo, Septemba 08, 2023 Jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya Ofisi kati ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (katikati) na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (kulia) yaliyofanyika leo, Septemba 08, 2023 Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya Ofisi kati ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa yaliyofanyika leo, Septemba 08, 2023 Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Bw. Ludovick Nduhiye akiwa Menejimenti na  Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Wizara ya Ujenzi katika hafla ya makabidhiano ya Ofisi kati ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa yaliyofanyika leo, Septemba 08, 2023 Jijini Dodoma.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...