Na Said Mwishehe,Michuzi TV
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imeelezwa kwamb sekta binafsi nchini imekuwa na mchango mkubwa kuinua bunifu kwa kutoa mawazo mazuri ya kuboresha sera.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza kuanza kwa Maonesho ya Wiki ya Sahara Sparks yanayotoa fursa wabunifu kuonesha bunifu zao Mkurugenzi Menejimenti Maarifa Costech Samson Mwela ameeleza kwa kina mchango wa sekta binafsi katika kuibua wabunifu.
Amesema Serikali imekuwa ikitenga fedha na kuingiza kwenye sekta ya kuendeleza ubunifu na ili ziweze kuelekezwa maeneo yenye manufaa na tija wanahitaji zaidi maoni ya wananchi na sekta binafsi huku akisisitiza ili kuendeleza bunifu zinazoibuliwa iko haja kwa wadau kuwa sehemu ya safari hiyo.
Amefafanua kwamba kwa muda muda sekta binafsi ikiwemo ya Sahara Sparks zimekuwa zikiandaa maonesho mbalimbali nchini ambapo wabunifu huonesha bunifu zao na zile zenye tija zimekuwa zikiendelezwa .
"Sekta binafsi katika eneo hili la ubunifu wamekuwa wakitoa mchango mkubwa sana, ziko bunifu nyingi ambazo zimeleta manufaa makubwa na siwezi kuzitaja hapa maana wote tunafahamu.
"Lakini sekta binafsi wamekuwa wanafanya mijadala ambayo imekuwa ikiibua mawazo mazuri yanayokusanywa na Serikali kabla ya kuyachakata na yamekuwa msaada kufanikisha utungaji sera na kuchochea mageuzi ya tasnia ya bunifu nchini na tuko katika mchakato wa kuangalia upya sera zetu kwa lengo la kuendelea kuboresha eneo hili la ubunifu,”amesema
Akifafanua zaidi amesema mawazo hayo mazuri yamekuwa yakiingizwa kwenye program zao na kusisitiza kupitia program zilizoanzishwa kuanzia mwaka jana, jumla ya vijana 83 wamenufaika na mfuko wa kuendeleza bunifu za vijana.
Ameongeza kwamba kati yao vijana 150 wanaotarajia kwenda kushiriki maonesho ya Sahara wameptia kwenye tume hiyo.
Awali Mkurugenzi wa Kampuni ya Sahara Venture, Mussa Kamata amesema kampuni hiyo tangu mwaka tangu mwaka 2016 wamekuwa wakifanya maonesho ya ubunifu na wanajivunia mafanikio yaliyopatikana yakiwemo kuwawezesha vijana 2000 kupata fursa hiyo kuonesha bunifu zao.
Amesisitiza kuwa kati yao kuna walionufaika kupata msaada wa kifedha, kutoka kwa wawekezaji ambao ni zaidi ya vijana 12 kupitia jukwaa hilo na sasa wanaendeleza bunifu zao.
"Tuliamua kuanzisha kuanzisha jukwaa kwa lengo kuu la kuwasaidia vijana wabunifu nchini kuwa na eneo ambalo wataonesha bunifu zao na kutoa maoni yao katika eneo la ubunifu."
Wakati huo huo Meneja wa Sahara Sperks Lead Rose Urassa amefafanua kuhusu maonesho hayo huwa yanafanyika kila mwaka kwa ajili ya kunyanyua jukwaa la sayansi na teknolojia nchini kupitia ubunifu na uwekezaji.
“Tukio hili litafanyika kwa wiki nzima katika viwanda vya makumbusho ya Taifa Posta na wabunifu mbalimbali watakuwa wanaonesha bunifu zao na kutakuwa na wawekezaji watakao hudhuria kuona namna ya kuwaunga mkono,”amesema
Ameongeza kutakuwa na matukio yanayoendelea kuanzia kesho na kuendelea mpaka Oktoba 13, 2023 na maonesho yenyewe yatafanyika Oktoba 13 na Oktoba 14 katika viwanja vya Makumbusho vilivyopo Posta jijini Dar es Salaam .
"Oktoba 13 maonesho yataanza saa 11 jioni kwa wageni kuanza kuingia na litaendelea mpaka saa nne usiku na siku ya pili ambayo ni Oktoba 14 tutaanza maonesho kuanzia saa tano asubuhi mpaka saa nne usiku katika eneo hilo hilo .
"Lakini kabla ya kufika Oktoba 13 , kuanzia kesho Oktoba 10 kutakuwa na matukio mengine yanaendelea kuelekea katika kilele chenyewe cha Sahara, " amefafanua.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Sahara Venture Mussa Kamata( kulia) akifafanua kwa kina kuhusu maonesho ya ubunifu ya Sahara Sparks yanayotarajia kufanyika jijini Dar es Salaam .Katikati ni Mkurugenzi Menejiment maarifa kutoka COSTECH Samson Mwela na kushoto ni Meneja wa Sahara Sparks Rose Urassa
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...