Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Bw. Titus Kaguo akizungumza na waandishi wa habari.

Na.Mwandishi Wetu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imevifungia vituo viwili vya mafuta kwa muda wa miezi miezi sita kwa kosa la kuhodhi mafuta ili kujipatia maslahi haramu ya biashara ikiwemo faida kubwa kutokaba na ongezeko la bei za mafuta jambo ambalo ni kinyume na sheria, kanuni na miongozo inayosimamia biashara ya mafuta nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari  Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano EWURA Bw. Titus Kaguo, amesema kuwa vituo vilivyofungiwa ni Kituo cha Kipenda Roho Investment pamoja na Oilcom vilivyopo Soya, Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma.

Bw. Kaguo amesema kuwa uamuzi huo umekuja baada ya kikao cha Bodi ya Wakurugenzi ya EWURA kilichofanyika Oktoba 9, 2023 na kujiridhisha vituo hivyo vilitenda kosa la kuhodhi mafuta kati ya mwezi Julai na Agosti mwaka huu.

Amesema kuwa uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi hadi sasa utakuwa umegusa vituo tisa, huku akieleza kuwa uchunguzi unaendelea katika vituo vingine.

“EWURA inapenda kuwakumbusha wafanyakazi wote wa biashara ya mafuta nchini kuhakikisha wanaendesha biashara zao kwa mujibu wa sheria, kanuni, na miongozo inayosimamia biashara ya mafuta nchini” amesema Bw. Kaguo.

Bw. Kaguo ametoa onyo kwa OMCs na wamiliki wa vituo vya mafuta kuwa serikali inafuatilia suala hilo kwa ukaribu kupitia vyombo vyake na ikithibitika kuna uvunjaji wa sheria na kanuni umetendeka hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kuwafutia leseni za biashara.

Kwa mujibu wa Sheria ya Petroli, sura Na 392 EWURA ina jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa mafuta wakati wote katika maeneo yote nchini.

Hata hivyo kuanzia mwezi Julai mwaka huu kumekuwepo na matukio kwa baadhi ya maeneo hasa pembezoni mwa nchi kukosa mafuta hasa kipindi bei zinapoelekea kubadilishwa na kusababisha kuwa na usumbufu makubwa kwa wananchi na madhara ya Kiuchumi.

Ili kufikia malengo EWURA inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisheria ikiwemo kuvifungia baadhi ya vituo vilivyothibitika kufichua mafuta kinyume na kanuni na miongozo inayosimamia biashara ya mafuta nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...