Na. Mwandishi Jeshi la Polisi.

Jeshi la Polisi Nchini leo Oktoba 05, 2023 limekabidhiwa msaada wa magari Manne aina ya Nissan Patrol toka Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia mabaki ya shughuli za Mahakama za Makosa ya Jinai - IRMCT yenye ofisi zake Jijini Arusha kwa ajili ya kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi wakati akipokea magari mawili yaliyotolewa kwa Mkoa huo ameishukuru taasisi hiyo kwa kutambua umuhimu wa kazi za Jeshi la Polisi za kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarika.

Sambamba na hilo pia amebainisha kuwa magari hayo yatakua msaada mkubwa na yataongeza ufanisi wa kazi za Polisi katika maeneo mbalimbali na yatatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro ACP Simon Maigwa ambaye naye alipokea magari mawili yaliyotolewa na taasisi hiyo kwa Mkoa huo, amesema magari hayo yatasaidia katika kuimarisha usalama wa watalii hasa kwa kuzingatia mikoa ya Kilimanjaro na Arusha watalii na wageni wengi hufika kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii.

Kwa upande wake Msajili wa Mahakama hiyo ya IRMCT Bwana Abubacarr Tambadou wakati akikabidhi magari hayo, amebainisha kuwa wataendelea kushirikiana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususani Jeshi la Polisi kwa kusaidia kutatua changamoto mbalimballi ili kuhakikisha usalama wa maeneo yote unaendelea kuwa shwari.

Aidha katika tukio lililofanyika katika taasisi hiyo pia imekabidhi gari moja kwa Jeshi la Uhamiaji kwa ajili ya kuimarisha doria, na kufanya jumla ya magari yaliyotolewa kuwa matano ambapo kwa Jeshi Polisi Mkoa wa Arusha limepata magari mawili na Kilimanjaro magari mawili.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...