MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema haina mfumo wowote mwingine inaouendesha wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo wa Forodha wa TANCIS ambao unatumika kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Stephen Kauzeni ameyasema hayo leo Oktoba 12, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu malalamiko ya Emmanuel Gadi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Wintech Tanzania Ltd anayedai kuwa, TRA imetengeneza mfumo wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo halali wa Serikali kinyume na Sheria ya Forodha.
Amesema, Gadi alifikisha malalamiko yake TRA kwa njia ya barua ya Februari 27, 2023 akidai kupewa uthibitisho na TRA wa kuingiza mzigo wa vifurushi 471 vya Toner Cartridges kupitia kampuni ya Tosh Logistics Ltd.
"TRA ilifanya Uchunguzi wa kutosha na kuthibitisha kwamba hapakuwa na mzigo wowote ulioingizwa nchini kwa jina la Wintech Tanzania Ltd wa vifurushi 471 vya Toner Cartridges kupitia kadhia yenye namba TZDL – 22-1382193 ya tarehe 18 Agosti 2022 kama anavyodai,” amesema Kauzeni.
Kauzeni ameendelea kueleza kuwa baada ya uchunguzi huo TRA ilimjibu mhusika kupitia barua yenye kumbukumbu namba CF 8/92/01 ya tarehe 25 Julai 2023 ikimjulisha kuwa, kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa House Bill of Lading na kutoonekana kwa mzigo huo kwenye kadhia iliyowasilishwa na kampuni ya Tosh Logistics Ltd, TRA isingeweza kuthibitisha kuingizwa kwa mzigo huo nchini.
“Kupitia taarifa ya Gadi aliyoitoa kwenye vyombo vya habari, tumebaini kuwepo kwa viashiria vya ukwepaji kodi kwani ni dhahiri kuwa mzigo wake uliingizwa kwa njia za magendo,” ameeleza Meneja Kauzeni.
Meneja huyo wa Elimu kwa Mlipakodi amemtaka mlalamikaji kuwasilisha nyaraka na uthibitisho wa Kampuni yake kuingiza mzigo huo nchini mara moja ili hatua stahiki zichukuliwe.
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Stephen Kauzeni akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu malalamiko ya Bw. Emmanuel Gadi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Wintech Tanzania Ltd anayedai kuwa, TRA imetengeneza mfumo wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo halali wa Serikali kinyume na Sheria ya Forodha (Picha na Mpiga picha wetu).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...