Na. Jacob Kasiri-Ruaha.

Wimbi la uingizaji wa mifugo unaofanywa na wafugaji wasioitakia mema nchi yetu ulioanza kushika kasi hivi karibuni, umegubikwa na siri nzito inayotarajia kuua soko la utalii ulianza kushika kasi ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla.

Doria iliyofanyika tarehe 17.11.2023 kwa kutumia Helikopta ndani ya hifadhi hiyo imekamata mifugo 812 wakiwemo kondoo 759, ngombe 53 na kubaini mifugo mingine mingi ikiwa pembezoni mwa hifadhi ikirandaranda kusubiri kuingia na kwenda kuharibu Ardhi Oevu ya Ihefu ambayo ni lulu na chanzo kikuu cha Mto The Great Ruaha.

Ikumbukwe kuwa ikolojia ya Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa zaidi ya asilimia 75 hutegemea Mto Ruaha Mkuu, hivyo madhara yoyote yanayosababishwa na mifugo pamoja na kilimo huathiri utiririshaji wa maji, athari hizo huenda sambamba na kutoweka kwa wanyamapori. Na wanyamapori wakitoweka hakutakuwa na utalii.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Godwell Meing’ataki - Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha alisema, "Mifugo inapoingia hifadhini husababisha mnyang’anyano wa malisho na maji kati mifugo hiyo na wanyamapori, matokeo ya ushindani huo ni uhaba wa malisho unaopelekea baadhi ya wanyamapori kufa na wengine wenye nguvu na uwezo wa kutembea umbali mrefu kutafuta eneo mbadala na kujikuta wakivamia makazi ya watu".

"Mifugo jamii ya kondoo,ng'ombe na mbuzi wanatabia ya kula eneo moja kwa muda mrefu tofauti na wanyamapori, wao wana tabia ya kuhamahama. Tabia hii ya kukaa sehemu moja kwa muda mrefu huathiri ukuaji wa mimea, huleta mmomonyoko wa udongo, ardhi kukosa rutuba na mvua kubwa zikinyesha hutokea mafuriko. Madhara hayo yote huathiri Uhifadhi na Utalii", aliongeza Kamishna Meing’ataki.

Mtaalamu wa tiba za wanyamapori, Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi, Isaya Kiwele kutoka Hifadhi ya Taifa Ruaha, alisema kuwa mifugo inapoingia hifadhini kuna uwezekano mkubwa wa wanyama hao kuambukizana magonjwa.

"Magonjwa kama Kimeta na Mafua ya ndege huingizwa hifadhini na mifugo na pia huweza kutolewa hifadhini na kupelekwa kijijini na mifugo hiyo hiyo iliyotoka hifadhini na kuleta madhara na vifo kwa jamii", mara nyingi mlipuko wa magonjwa haya huua sana wanyama na binadamu na kusababisha watalii kutokuja kutalii nchini na kulikosesha Taifa mapato, alisema Kiwele.

Ikumbukwe kuwa hili ni tukio la pili ndani ya mwezi huu Novemba la kukamatwa kwa mifugo mingi kiasi hicho, tukio la kwanza lilitokea tarehe 13 na 14 Novemba, 2023 ambapo ng’ombe 345 walikamatwa wakichunga kinyume cha sheria na trekta moja iliyokuwa ikiendesha shughuli za kilimo kinyume cha sheria.
Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...