Na Imani Mtumwa , Maelezo
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa, amesema, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kitaendelea kutoa taaluma za fani mbalimbali ili kuhakikisha kinazalisha Wataalam walio bora Nchini.
Ameyasema hayo wakati akizindua Baraza la Nane la Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA ) katika ukumbi wa Mikutano Skuli ya Utalii Maruhubi.
Amesema, Wajumbe wote walioteuliwa ni watendaji wa Serikali hivyo ni matumaini yake wajumbe hao wanaweza kufanya maamuzi mazuri ya kuendelea kufanikisha mipango na mikakati ya chuo hicho.
Amesema, Zanzibar imekua na ufaulu mkubwa kwa wanafunzi wa Sekondari hivyo SUZA inahitaji kuendelea kuwa na mipango ya kuandaa programu mbalimbali ziatakazopelekea wanafunzi hao kuweza kujifunza kupitia chuo hicho.
Pia aliwataka wajumbe hao kutumia tafiti mbalimbali juu ya miradi mikubwa ili kuleta mageuzi yanayoendana na wakati na kuisaidia Serikali kuweza kukuza Uchumi wa Taifa.
Aidha Waziri Lela amewasisitiza Wajumbe hao kuhakikisha wanaendelea kutatua changamoto za kutanua miundombinu ya upatikananji wa fani ili kuhakikisha wataalamu wanaozalishwa Sekondari wanapata fursa ndani ya Chuo hicho.
Hata Hivyo amewataka wajumbe hao kufanya kazi kwa kushirikiana na wajumbe waliopita ili kuhakikisha wanaiendeleza vyema sekta ya Elimu na kuhakikisha SUZA inatoa vipaombele vya ufundi kwa upande wa Zanzibar.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo la Nane Bi. Hamida Ahmad Muhammed amempongeza Waziri wa Elimu kwa kuharakishaa kuchagua baraza jengine mara baada ya kumaliza muda kwa Baraza la saba ili kuhakikisha chuo hicho kinaendelea kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali.
Nae Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar (SUZA) Profesa Mohammed Makame Haji amewasisitiza Wajumbe Wapya kutumia utaalamu uliyobora katika utekelezaji wa kazi zao ili kuweza kuisadia Serikali kufikia malengo yake ya Uchumi wa Buluu.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Muhammed Mussa akitoa nasaha kwa wajumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar SUZA wakati akizindua Baraza la nane la chuo hicho na kuwaaga wajumbe waliomaliza muda huko Ukumbi wa Skuli ya Utalii Maruhubi Mjini Unguja.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar SUZA Profesa Muhammed Makame Haji akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa baraza la nane la Chuo hicho lilifanyika Ukumbi wa Skuli ya Utalii Maruhubi Mjini Unguja.
Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la nane la Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar SUZA wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa baraza hilo na kuwaaga wajumbe waliomaliza muda huko Ukumbi wa Skuli ya Utalii Maruhubi Mjini Unguja.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Muhammed Mussa akiwatunuku vyeti vya shukurani baadhi ya wajumbe wa Baraza la saba la Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar SUZA wakati wa uzinduzi wa Baraza la nane la chuo hicho na kuwaaga wajumbe waliomaliza muda .
PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...