KATIBU Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius. Kahyarara ameiagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutangaza mafanikio ya Taasisi yanayopatikana kikanda, kimataifa pamoja na mafanikio yanayopatikana katika utekelezaji wa majukumu yake.
Prof. Kahyarara ameyasema hayo leo Desemba 5, 2023 alipotembelea banda la maonesho la TMA katika mkutano wa 16 wa Wadau wa Sekta ya Uchukuzi kuhusu Ufuatiliaji na Tathmini (16th JTSR) unaofanyika jijini Arusha.
Pia ameisifu TMA kuwa ni taasisi inayofanya kazi nzuri na yenye mafanikio kitaifa na kimataifa.
“Ni wakati sasa, jamii ikatambua mafanikio ya TMA kikanda na kimataifa, natambua kuwa taasisi hii inafanya kazi nzuri inayoonekana, ni vyema kujipanga kuwa na vipindi katika televisheni na kueleza mafanikio hayo” amesisitiza
Aidha, Prof. Kahyarara ameitaka Wizara kusimamia programu ya kutangaza mafanikio ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi kwa kuanza na TMA.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TMA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Miundombinu na Ufundi, Dkt. Pascal Waniha, amesema TMA imekuwa ni kielelezo bora katika ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na nje ya Kanda.
“Kazi kubwa imeendelea kufanyika katika kuiwakilisha vizuri nchi kwenye masuala ya hali ya hewa kimataifa na kueleza kuwa imeteuliwa na WMO kuwa muandaaji wa mafunzo ya rada katika Kanda ya Afrika yanayoratibiwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)". Amesema Dkt. Waniha
Ameendelea kusema kuwa fursa hiyo imepatikana kutokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya hali ya hewa unaoendelea kufanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mafanikio mengine yaliyoelezwa mbele ya Katibu Mkuu kupitia mabango ni pamoja na maendeleo katika shughuli za uangazi, ununuzi wa vifaa na mitambo ya hali ya hewa, udhibiti wa huduma za hali ya hewa pamoja na njia mbalimbali zinazotumika katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa jamii na kwa sekta mahsusi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...