Na Mwandishi Wetu – Pemba

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Ofisi ya Zanzibar imetoa elimu kuhusu Uanzishwaji na Uendeshaji wa Klabu za Kidijiti kwa Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar (JUWASEZA) kwenye kikao-kazi kilichofanyika Jumatano hii, Pemba.

 

Meneja wa Mamlaka hiyo Ofisi ya Zanzibar, Bi. Esuvatie Masinga akizungumza mara baada ya semina hiyo alisema Wakuu wa Skuli za Sekondari ni msingi muhimu katika kuhakikisha Klabu za Kidijiti zinaanzishwa kwenye skuli na kuendeshwa ili ziwanufaishe wanafunzi kuwa washiriki kamili katika kujenga uchumi wa kidijiti na buluu. 

 

“Ushiriki wa vijana kwenye uchumi wa kidijiti na buluu ni wa msingi sana; hii ndiyo sababu tumeazimia kuwafikia wanafunzi kupitia wakuu wa skuli kwa kuwa wanayo nguvu ya ushawishi kama Viongozi watakaochagiza Uanzishaji wa klabu hizi muhimu,” alisema.

 

Masinga alibainisha kuwa ili kujenga uchumi wa kisasa unaoegemea zaidi matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ushiriki wa vijana ni muhimu sana.

 

“Vijana ndiyo nguzo muhimu ya kuimarisha na kujenga uchumi wa kidijiti, lengo letu ni kuhakikisha vijana wanajiunga na kuwa washiriki wa Klabu za Kidijiti zitakazowapatia maarifa ya teknolojia kupitia masomo ya STEM yaani Hisabati, Sayansi, Teknolojia na Uhandisi,” 

 

Alisema TCRA itaendelea kuhamasisha ubunifu na uvumbuzi katika klabu za kidijiti zilizoanzishwa na zitakazoanzishwa ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo waratibu wa klabu za kidijiti ili waweze kuzisimamia vyema ziweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.

 

“TCRA tunaamini Wakuu wa Skuli mtasaidia uanzishwaji wa klabu za kidijiti katika skuli zenu. Ikumbukwe kuwa klabu hizi hazina tofauti na klabu nyingine za masomo kama klabu za Hisabati, Kiingereza nakadhalika. Ili tujenge uchumi wa kidijiti na buluu matumizi ya TEHAMA hayaepukiki hivyo ni tunapaswa tuwaandae vijana wetu” alisema Masinga. 

 

Aliwaasa wanafunzi pamoja na walimu ambao ni walezi kujiunga kwenye klabu za kidijiti kwa kujisajili moja kwa moja kupitia tovuti ya https://digitalclubs.tz au kuzianzisha moja kwa moja katika skuli zao kwa kupata utaratibu wa uanzishaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa JUWASEZA Khatibu Rashidi aliishukuru Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Ofisi ya Zanzibar kwa kuona umuhimu wa kuwapa walimu wakuu Elimu ya Uanzishaji wa Klabu za Kidijiti akisema zitakuwa zenye mchango mkubwa katika kuwahamasisha wanafunzi kuifahamu zaidi Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

 

“Hakika tumefaidi sana kwa semina ambayo mmetupatia, huu ni msingi mzuri wa kuwajengea uwezo wanafunzi wetu hasa tutakapoanzisha klabu hizi kwenye skuli zetu,” alisisitiza.

Mkutano huo wa 11 wa JUWASEZA ulifunguliwa na Waziri wa Elimu ya Mafunzo ya Amali Mheshimiwa Lela Muhammed Mussa ambae aliwasisitiza walimu kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Meneja wa TCRA Ofisi ya Zanzibar Bi. Esuvatie Masinga akitoa elimu kuhusu uanzishwaji wa Klabu za Kidijiti katika Skuli za Sekondari Zanzibar wakati akizungumza na Wakuu wa Shule kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar (JUWASEZA) uliofanyika kisiwa cha Pemba kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni. Picha na TCRA.
Picha ya pamoja kati ya Meneja wa TCRA Ofisi ya Zanzibar Bi. Esuvatie Masinga(aliejifunga mtandio mweupe), Maafisa wa TCRA na Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar muda mfupi baada ya kuhitimishwa Mkutano wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar (JUWASEZA) uliofanyika kisiwa cha Pemba kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni. Katika Mkutano huo TCRA ilitoa elimu kuhusu uanzishwaji wa Klabu za Kidijiti katika Skuli za Sekondari Zanzibar. Picha na TCRA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...