Na Muhidin Amri,Kilwa

WAKAZI 59,983 wa mji wa Masoko
na Kivinje pamoja na wanaoishi katika vijiji vya Singino,Nanguruku,Mavuji,Mchakama na Mpara wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, wanatarajia kuondokana na adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Ni kufuatia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilayani humo, kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji wa miji 28 utakaogharimu Dola za Marekani milioni 18,976,499.41 sawa na Sh.bilioni 44,000,000,000 za Kitanzania.

Mradi huo utatumia chanzo cha mto Mavuji,unatekelezwa na Ruwasa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji hivyo.


Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Kilwa Mhandisi Lunyilija Msomi alisema,mradi huo utakapokamilika utaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji katika wilaya hiyo.


Aidha alisema,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wametengewa Sh.bilioni 2,473,751,779.00 ili kukamilisha ujenzi wa miradi sita katika vijiji vya Hotelitatu,Nakiu,Kipindimbi,Kinjumbi,Marendego na Kilwa Kisiwani.


Pia alisema,serikali imetoa fedha Sh.bilioni 1,036,451,050.00 zitakazotumika kujenga miradi mitano mipya katika vijiji vya Kisimamkika,Zingakibaoni,Mbwemkuru,Nainokwe na Pandeplot-Mtangashari-Nang’ookiwa.


Katika hatua nyingine Msomi alieleza kuwa, kwa mwaka 2022/2023 walipokea Sh.bilioni 2,981,502,492.69 ambazo zilitumika kwa ajili ya kutekeleza miradi 9 katika vijijiji Nakiu,Chumo,Chapita,Likawage,Hotelitatu,Kinjumbi,Marendego,Kilwa Kisiwani,Kipindimbi,na Mji wa Masoko.


Alisema,baadhi ya miradi katika vijiji hivyo imekamilika na kuanza kutoa huduma na mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na itakapokamilika itawezesha kuongeza kiwango cha huduya maji kutoka asilimia 63.7 ya sasa hadi asilimia 72.

Miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa maji Marendego,ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 95 na tayari umeanza kutoa huduma ya maji kwa wakazi wa kijiji hicho wapatao 2,151.

Alitaja kazi zilizotekelezwa ni ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000,nyumba ya mashine ya kusukuma maji na kufunga umeme,kujenga vituo vya kuchotea maji 10.


Kwa mujibu wa Msomi,kazi nyingine zilizofanyika ni kuchimba mitaro ya kulaza mabomba urefu wa kilomita 2.5,kujenga ofisi ya jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO) kununua na kufunga pampu ya kuvuta maji kwenye kisima.

Alieleza kuwa,chanzo cha mradi huo ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 11,000 kwa saa na fedha zilizotumika kutekeleza zimetoka mfuko wa maji wa Taifa.

Mkazi wa kijiji cha Marendego Hadija Ali,ameishukuru serikali kukamilisha mradi huo uliowaondolea kero iliyokuwepo kwa zaidi ya miaka 40 ambapo walitegemea kupata maji kupitia chanzo cha asili cha Kilengalonga ambacho maji yake hayakuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Alisema,wakati mwingine walilazimika kutembea umbali wa kilomita 2 kila siku kwenda kutafuta maji hivyo kukosa muda wa kufanya shughuli za maendeleo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Mohamed Mpongo alisema,mradi huo umesaidia sana kupunguza malalamiko hasa kwa wanandoa pindi wanawake wanapochelewa kurudi nyumbani wanapokwenda kutafuta maji kwa matumizi ya familia zao.


Alisema,tangu kijiji hicho kilipoanzishwa zaidi ya miaka 40 iliyopita wananchi wake hawajawahi kuona maji ya bomba,hivyo ameipongeza serikali kwa kutoa fedha na Ruwasa kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji ya bomba.

Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Kilwa mkoani Lindi Mhandisi Msomi Lunjilija kushoto,akiwaelekeza baadhi ya wakazi wa kijiji cha Marendego wilayani humo namna ya matumizi ya koki za maji alipotembelea kituo cha kuchotea maji (DPS) kilichojengwa katika kijiji hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...