Jengo la Mama na Mtoto Njombe.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Njombe (Kibena) Hellen Masese, akizungumza na wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari nchini, wakati wa ziara ya wahariri hao mkoani Njombe iliyoandaliwa na mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibilango, Winfred Kayombo akizungumza na wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari nchini, wakati wa ziara ya wahariri hao mkoani Njombe iliyoandaliwa na mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MGANGA Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Kibena iliyopo mkoani Njombe, Helena Msese amesema kabla ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuwasaidia kujenga jengo jipya la kuhifadhia watoto njiti, walikuwa wanalaza watoto hao wawili hadi watatu kwenye kitanda kimoja hivyo kuhatarisha usalama wao.

Amesema hali hiyo imetokana na kuwepo kwa chumba kidogo cha kuhifadhi watoto hao kilichokuwa na uwezo wa kutunza watoto wawili pekee hata hivyo, kilitunza watoto 10 hadi 15.

Akizungumza wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari nchini, mkoani Njombe iliyoandaliwa na Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF),
Dkt. Msese amesema "Inapofika wakati unawalaza watoto wale wawili hadi watatu kwenye kitanda kimoja, usalama ni mdogo kwani unapowahudumia wanaweza kupata magonjwa ya kuambukizana."

Dkt. Msese amesema wapo watoto waliozaliwa kabla ya umri lakini afya zao ni njema, wale ambao hawakuwa vizuri kiafya na wanaozaliwa majumbani wote wanatakiwa kuhifadhiwa hospitalini hapo.

Ameeleza kuwa "Kutokana na changamoto hii, nilichukua hatua ya kuomba msaada kwa viongozi mbalimbali nilishiriki hadi kwenye mikutano ya Kijiji na kueleza changamoto hii kwani hata tukifanya mambo mengi na huku tukipoteza watoto, taifa la kesho hakuna."

Daktari huyo ameongeza kuwa ni lazima kuwe na mazingira mazuri kwa ajili ya kuwatunza watoto njiti.

"Sauti yetu ilisikika na TASAF ikawa tayari kutusaidia. Mpaka sasa tunahudumia kwa mwezi watoto 30, jengo hili limefanyika baraka kwani tunavyo vyumba vitano vya watoto njiti ambapo tunaweza kuwatunza kwa nafasi watoto 40," amesisitiza

Pia amesema wamepata chumba cha kuwaweka wazazi waliotoka kwenye upasuaji kwani kwa sasa wanaweka wanawake watano pekee.

"Bado tunahitaji vyumba zaidi kwani nikiwa na operesheni sita au saba sitaweza kufanya kwani hakuna pakuwaweka, wapo wanawake wengi wanasubiri. Kwa kupata jengo hili, ni kitu cha thamani," amesema.

Pia ameishukuru serikali kwa hatua walizochukua kupata jengo hilo kwani watawasaidia watoto kufikia umri unaotakiwa pamoja na kuongeza kufanya upasuaji kwa wanawake.

"Jengo hili linauwezo wa kuhifadhi wanawake 25 na watoto 40 hivyo ni hatua kubwa sana kwani hospitali hiyo ni mama na hupokea wagonjwa wengi wa Mkoa huo," amesema.

Ameongeza kuwa mwaka 2022/23 wamefanya upasuaji kwa wanawake 1,980 wakati hospitali nyingine ni chini ya hapo na ni kutokana na huduma wanazotoa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibilango, Winfred Kayombo amesema mwaka 2022 katika vikao vyao vya Kijiji waliibua wazo la kuwa na jengo la watoto njiti na kuamua kuomba msaada TASAF wawasaidie kujenga jengo hilo.

Amesema kuwa wakazi wa eneo hilo hutumia hupata huduma za afya katika kituo hicho na kutokana na changamoto waliona washirikiane na wananchi.

"Walikubaliana wananchi kushiriki kama nguvu kazi kwa kuchimba eneo la kujenga jengo hili, na hospitali wasaidie kuandaa malighafi za awali matofali na mawe na gharama ni Sh milioni 160 na mpaka sasa tumetumia zaidi ya Sh 154," amesema Kayombo.

Ameeleza kuwa zaidi ya cha Sh milioni saba imebaki baada ya kukamilisha shughuli za ujenzi huo.

Kayombo amesema wananchi walikuwa na muitikio mzuri katika kuhakikisha jengo hilo linajengwa na kukamilika.

"Tunaishukuru serikali na TASAF kwa kutusaidia kukamilisha jengo hilo. Kama wazazi tuliona changamoto ya watoto hawa ndio maana tuliona kuna umuhimu wa kujenga jengo hili,"

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Irene Vwiha ameeleza kuwa changamoto aliyoiona kama mwanamke ni mazingira yasiyoridhisha yaliyokuwa yanatumika kuhifadhi watoto waliozaliwa kabla ya umri (njiti) na wale ambao wametimiza umri lakini hali zao si nzuri.

Amesema kuwa chumba cha awali kilikuwa kidogo kiasi ambacho uhifadhi wa watoto zaidi ya 10 kwa kubanana.

"Wapo wengine ambao wanaumwa na wengine wamezaliwa siku bado hivyo tuliona tuwe na mradi wa mama na mtoto kupata chumba kikubwa ili tuwahidumie mama na watoto," amesema Vivaha.

Amesema jengo la sasa linauwezo wa kuhudumia watoto wengi kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo nje ya Halmashauri ya Njombe tofauti na awali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...