Na Said Mwishehe, Michuzi TV

KABLA ya kwenda mbali zaidi naomba nieleze mapema umefika wakati kwa Watanzania na hasa wakulima kuhakikisha wanaendelea kutumia mbegu za asili katika kuzalisha mazao ya vyakula.

Ndio lazima tutumie mbegu asili kwa lugha nyingine mbegu za kienyeji.Ni mbegu ambazo tumekuwa nazo tangu enzi na enzi, mbegu ambazo walizitumia wazee wetu na kuvuna mazao ya uhakika, bora, yenye lishe na kubwa zaidi kuwa na uhakika wa chakula.

Nafahamu dunia inakwenda kasi sana, teknolojia nayo imeendelea kupewa nafasi kubwa hata katika shughuli za kilimo.

Kukua kwa teknolojia kumesababisha wanasayansi kuingia maabara kufanya tafiti za mbegu gani zinapaswa kutumiwa na wakulima hasa katika kipindi hiki ambacho kuna changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Naheshimu jitihada zao, nathamini na kutambua shughuli wanazofanya, siku hizi ni jambo la kawaida kusikia ukinunua mbegu fulani utavuna mazao mengi lakini kwa muda mfupi.

Sawa utavuna kwa muda mfupi na mazao yatakuwa mengi.Swali la kujiuliza ninaweza kutumia mbegu ya msimu huu kwa kilimo cha msimu unaokuja, jibu ni hapa.

Kwanini? Ni kwasababu mbegu za kisasa kila mwaka unabidi ununue nyingine ndio upande na sio tu kupanda na dawa za kuua wa wadudu lazima zitumike.Na hapa lazima nieleweke sio kwamba napinga uwepo wa mbegu za kisasa, lazima ziwepo na anayetaka atumie.

Hakuna anayeweza kumzua mkulima kununua mbegu ya kisasa, ni haki yake na ni uamuzi wake .Tunafahamu mahitaji ya chakula duniani ni makubwa kulingana na idadi ya watu, hivyo kinachoangaliwa kwa sasa ni kuzalisha kwa wingi ili kukidhi mahitaji.

Kwa mtazamo wangu , pamoja na mahitaji ya dunia katika upatikanaji wa chakula lakini usalama wetu wa vyakula tunavyokula ni muhimu lakini ni muhimu zaidi kuwa na uhakika wa mbegu na kwa hakika hadi sasa mbegu yenye uhakika ni mbegu ya asili.

Kwa Tanzania kumekuwa na njia mbalimbali za kutunza na kuhifadhi mbegu za asili kutoka msimu mmoja hadi mwingine.Na mbegu hizo zimeendelea kutoa mazao bora , salama na yanayofaa kwa chakula. Hakuna mwenye shaka na mbegu asili maana inavyopatikana tunajua.

Mbegu ya asili haikufanyi uwe mtumwa kwamba kila msimu lazima uende dukani kununua mbegu.Ukifika wakati wa kilimo unachukua mbegu yako uliyoihifadhi vizuri aidha kwa kuweka juu ya chanja au kwenye benki ya mbegu asili kisha unaipanda.

Binafsi ninaamini katika mbegu asili zaidi kuliko mbegu za kisasa. Zipo sababu nyingi za kuamini mbegu ya asili bado inanafasi kubwa katika nchi yetu, unajua kwanini inatupa uhakika wa chakula safi na salama kwa mazingira.

Kuna wakati huwa natafakari iwapo Tanzania hatutakuwa na mbegu zetu za asili, je wakulima wetu wote wanaweza kumudu gharama za kununua mbegu kuwahi msimu wa kilimo? Je huko ambako mbegu za kisasa zitakuwa zinatoka hakutakuwa na masharti mengine magumu?

Kwa hali ilivyo na tusipochukua hatua ya kuendeleza mbegu zetu za asili, tutakuwa watumwa katika chakula. Ndio kama huna mbegu kwanini usiwe mtumwa?Jaribu tu kuwaza hata sasa mbegu ya kisasa ambayo utatumia mwaka huu, katika msimu mwingine wa kilimo ukipanda haioti na ikiota haitakupa mazao mazuri.

Kwa lugha rahisi tumeshaanza kuwa watumwa wa mbegu bila kujua. Kama nchi kuna haja ya kujitafakari mapema kabla ya kuzama kwa asilimia 100 kutumia mbegu za kisasa.

Nikiri nafahamu jitihada ambazo serikali inaendelea kuchukua kuhakikisha mbegu zetu za asili zinaendelea kutunzwa, kuhifadhiwa na kutumiwa na wakulima kuzalisha mazao. Katika hilo naipongeza Serikali yangu, mbegu za kisasa inazihitaji lakini za asili nazo zimeendelea kupewa nafasi.

Hata hivyo wakati Serikali ikiweka juhudi katika mbegu za asili, pia kumekuwepo na wadau mbalimbali ambao nao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mbegu za asili zinaendelea kupewa nafasi nchini Tanzania kutokana na kutambua faida zake na umuhimu wake kwa usalama na uhakika wa chakula.

Miongoni mwa wadau hao ni Mtandao wa Bionuai Tanzania (TABIO), Envirocare, Taasisi ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM) na wengine wengi ambao wameendelea kuelezea faida za mbegu asili.

Katika kuhakikisha wanafanikiwa kuizungumzia mbegu ya asili wamekuwa na miradi mbalimbali ambayo inajengea uwezo wakulima kuzalisha mbegu asili na kuzitumia katika kila msimu.

Hivi karibuni TABIO kwa kushirikiana na Envirocare wameandaa semina kwa waandishi wa vyombo vya habari nchini ambako wametumia nafasi hiyo kuomba vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele kuufahamisha umma wa Watanzani umuhimu wa kuendelea kutumia mbegu asili.

Akielezea sababu za kuandaa semina hiyo kwa waandishi wa habari Abdallah Ramadhan Mkindi ambaye ni Mratibu wa TABIO amesema lengo la kuimarisha uwezo wao wa namna ya kuandika kuhusu masuala yanayohusiana na masuala ya mbegu za asili.

"Kwa kushirkiana na Envirocare tunateke katika mradi ambao unapaza sauti kuhusu mbegu za asili au mbegu za wakulima ambazo zinaonesha zinachangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa chakula nchini.

Kwa hiyo tunaona kunahitajio la kuendelea kuimarisha uwezo wa waandishi wa habari katika kutoa taarifa sahihi kuhusu mbegu za asili ili taifa kwa ujumla liweze kupata taarifa sahihi kuhusu mbegu hizi," anasema.

"Tunaamini baada ya waandishi kupitishwa kwenye mada kadhaa zinazohusiana na mbegu za asili faraja yetu ni kwamba wamepata uelewa mzuri zaidi na hatimaye tunategemea uwezo huo utasaidia katika kuelimisha jamii kuhusu mchango wa mbegu za asili katika kuzalisha chakula na kilimo kwa ujumla."

Hata hivyo swali mojawapo lilikuwa kwanini za asili, ambapo Mkindi amejibu kwamb mbegu za asili kwanza ndizo ambao wamerithi kutoka kwa babu na bibi zao na vizazi vingi tu vimetumia mbegu za asili huku akifafanua kwa Tanzania bado mbegu za asili zinatumika katika uzalishaji wa chakula kuanzia mazao mbalimbali mahindi kama muhogo, mpunga na mazao mengine.

"Kwa hiyo mbegu hizi zina mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula ambacho kinatumika hapa Tanzania na hata nje ya nchi, ambapo wafanyabiashara wanapeleka vyakula hivyo vinavyotokana na mbegu za asili

Swali lingine lilikuwa tafiti zinaonesha mbegu za asili zinalimwa kwa kiwango gani na katika mikoa gani? Amejibu tafiti zinaonesha mchango wa mbegu za asili katika kilimo ni zaidi ya asilimia 70 na takwimu ambazo zimepatikana kutoka Wizara ya Kilimo mwaka 2019/2020 zinaonesha eneo kubwa la ardhi lilimwa kwa kutumia mbegu za asili

"Kwa hiyo kama eneo kubwa lililimwa kwa kutumia mbegu za asili inamaanisha kwamba mbegu hizi zinamchango mkubwa kwa ajili ya uzalishaji chakula hapa nchini hata kama sio kwaa asilimia 100."

Kwa upnde wake Mtaalam wa Mbegu katika kitengo cha Sera , Ushawishi , Utetezi na Uzalishaji wa TABIO, Daud Manongi anaeleza kwa miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa mbegu za asili kwenye maeneo mengi lakini kwa sasa mbegu za asili zinapatikana kwa wingi.

"Kulingana na uendelevu wa program mbalimbali zinazohusika na uendelezaji wa mbegu zinazosimamiwa na wakulima hasa ujenzi wa benki mbalimbali ambazo ziko kwenye jamii imerahisisha upatikaji wa mbegu asili katika jamii husika...

Na hii imetokana na wananchi kuelewa nini maana ya benki za mbegu lakini imekuza uwanda mpana wa upatikanaji wa mbegu kwani katika benki hizi unaweza kupata mbegu tofauti tofauti ambazo zinapatikana kwenye jamii husika.

Zaidi ya yote hizi benki za mbegu zinakuwa kama darasa ili watu kujifunza kwa namna gani wanaweza kuendeleza mazao asili kwa kuzingatia kilimo ikilojia na mbinu za kilimo hai.

Kuhusu upatikanaji wa mbegu asili, anasema kwa sasa kuna zaidi ya benki za mbegu 22 zinazosimamiwa na wakulima kuzunguka Tanzania nzima ambapo benki hizo zinaweza kuhudumia wakulima 200 mpaka 300."Kwa hiyo ukiangalia wa uwiano utaona watu wengi wanaweza kuhudumiwa na hizi benki."

Amefafanua kwa sasa kuna kamati za kusimamia benki za mbegu za asili, kuna wazalishaji na waendelezaji wa mbegu asili ambao hao wanawaita wazalishaji na watunzaji mbegu asili.

Pia anasema kwa sasa kuna kiasi kikubwa cha mbegu asili ambacho kinahifadhiwa katika benki za mbegu za asili na kwamba watu wengi wanaweza kutupata mbegu hizo kupitia mitandao yao lakini na maeneo ambako wako. Kuna benki 22 za mbegu asili na matarajio yetu ni kuongeza benki nyingine."

Alipoulizwa vipi kuhusu mbegu za asili zinazongezeka au zinapungua? Amejibu kuwa kwa bahati mbaya utafiti unaonesha mazao yanayotokana na mbegu asili yanaendelea kudorora na kupotea na hiyo inatokana na mchanganyiko wa mbegu za kisasa na asili.

Aidha pamoja na tafiti ambazo mara nyingi zimekuwa hazina tija ya moja kwa moja katika kuendeleza mbegu za asili ikiwa tafiti nyingi zimejikita katika kuongeza uzalishaji na sio katika kuangalia suala zima la lishe na namna gani tunaweza kutunza na kuendelea baionua ya mbegu

"Kiuhalisia kwa sasa tunachoomba tafiti nyingi zisiangalie katika uzalishaji bali namna gani ya kuboresha mazao ya asili, kuyatunza na kuyahifadhi kutoka kizazi kimoja mpaka kingine lakini zaidi ya yote vinasaba za hizi mbegu zinaweza kuwa sehemu ya jamii husika ambayo inazalisha mbegu wa muda mrefu ili tusiwanyime haki ya kumiliki na kuendeleza mazao yao ya kiasili na mwisho wa siku mazao haya yakachukuliwa na kuendelezwa kwa njia kiuhandisi jeni na wakulima hawa kuwa watumwa wa kununua mbegu.

Vipi kuhusu faida za mbegu za asili. Amejibu mbegu ya asili inampa mkulima uhuru wa kuzalisha kila mwaka kwa sababu ni endelevu kwa hiyo kile kizazi ambacho ni jeni asilia, jeni mama ya kizazi cha mbegu inakuwa imehifadhiwa kutoka miaka na miaka na mkulima husika kwa hiyo inaweza kurithiwa na vizazi na kuendelea. Inaweza kupunguza ubora wake lakini haiwezi kupotea kwa hiyo bado anakuwa na haki ya kuendeleza ile mbegu.

"Faida nyingine unapotumia mbegu za asili unarudi kwenye uasilia wa kiuzalishaji mbinu za kiasialia za kuzalisha mazao, kwa hiyo unatunza udongo unaozalisha, unahakikisha unatumia viuatilifu rafiki katika kuua wadudu lakini unaweka usawa wa kiikolojia kwasababu hata madawa ya kiasili unayotumia kwenye kudhibiti wadudu kwenye uzalishaji wa mbegu za asili haziui , lakini inafukuza .

Ule mfumo wa kiikolojia wa kuhifadhi na kuendeleza wadudu unaendelea kuwepo kwenye eneo husika kwa hiyo ndio sehemu muhimu ya kuhakikisha kwamba lazima tuilinde na kuiendeleza kuhakikisha mazao ya asili yanaleta tija" anasema.

Lakini zaidi ya yote hizi mbegu zinapatikana kwa urahisi. Zinapatikana kwenye jamii ambayo wakulima wapo na mbegu za asili mchakato wake wa kuzipata sio mgumu kwasababu wakulima wake wanaweza kubadilishana, wakulima wanaweza kulizalisha kwa urahisi, kwa hiyo mazingira ambayo yanapatikana hayaleti ugumu kwa mkulima kuendeleza

Alipoulizwa kuhusu nafasi ya waandishi wa habari kuzipigia debe mbegu za asili. Manongi amesema kama habari njema inaweza kuleta uzima, afya na kicheko na furaha ni kuandika kuhusiana na habari zinazohusu uhuru wa mbegu na uhakika na usalama wa chakula kupitia mbegu za asili.

"Ni muhimu sana kutenga muda wa kujifunza zaidi kwanini mbegu za asili na kurejea kwenye asilia. Mwito wangu kwa waandishi wa habari ni kuangalia ni nafasi gani iliyopo kwa wakulima wadogo ambapo kwa asilmia 76 wanatumia mbegu za asili na wanaweza kusema kuanzia mwaka 2014 hadi 2022 nchi yetu imekuwa utoshelevu wa chakula kwa zaidi ya asilimia 100 na kati ya hao asilimia 76 ni wakulima wadogo ambao wanalima mazao ya asili.
















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...