Na Muhidin Amri, Mtama

ZAIDI ya wakazi 1,100 wa kijiji cha Tulieni na Moka Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi,wameondokana na adha ya kukosa maji safi na salama baada ya mradi wa maji Tulieni wenye thamani ya Sh.milioni 416,589.12 kukamilika.


Mradi huo uliotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),umemaliza kero ya muda mrefu ya wananchi wa vijiji hivyo kutembea umbali wa kilomita 2 kila siku kwenda kuchota maji kwenye mito na vyanzo vingine vya asili.


Mkazi wa kijiji hicho Salma Milanzi alisema,walikuwa wanachota maji kwenye mito na madimbwi ambayo hujaa maji wakati wa masika tu na wakati wa kiangazi vyanzo hivyo vinapokauka wanalazimika kuingia gharama ya kununua ndoo moja ya lita 20 kwa Sh.800.


“tulikuwa na maisha magumu katika kijiji chetu,tunaishukuru sana serikali kwa kutuondolea tatizo kubwa la maji safi na salama”alisema Milanzi.


Alisema,katika umri wake wa miaka 68 hajawahi kuona maji ya bomba katika kijiji chao,badala yake alikuwa anayaona na kuyatumia anapofika Hospitali ya misheni Ndanda na Nyangao.


Mkazi mwingine Moza Mtani alisema,mradi huo ni mkombozi mkubwa kwani umetoa nafasi ya kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo miradi ya huduma za afya na elimu na kwenye shughuli za kijamii kama ndoa na misiba.


Mwenyekiti wa kijiji cha Tulieni Mikidad Likwati alisema,awali wananchi wa kijiji walitegemea maji yanayotoka kwenye milima na mabonde hali iliyosababisha baadhi yao kupatwa na ugonjwa wa kifua na magonjwa ya milipuko ikiwemo kuhara na matumbo.


Mtendaji wa kijiji hicho Dafrosa Chilumba alisema,kabla ya ujenzi wa mradi huo haujakamilika ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo hasa za kujitolea ulikuwa mdogo na hali hiyo ilitokana na wananchi kutumia muda wao mwingi kwenda kutafuta maji.


Chilumba,ameipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kutekeleza mradi wa maji Tulieni ambao umesaidia kuchochea na kuharakisha maendeleo katika kijiji hicho.


Kwa upande wake meneja wa Ruwasa wilaya ya Lindi Mhandisi Idd Pazi alisema,mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 416,589,589.12 fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uvico-19 na umekamilika kwa asilimia 100.


Aidha alisema,upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa wilaya ya Lindi kwa sasa imefikia wastani wa asilimia 76 ambapo kwa Halmashauri ya Mtama ni asilimia 75 na katika jimbo la Mchinga ni asilimia 77.


Kwa mujibu wa Pazi ni kwamba,kabla ya kuanzishwa kwa Ruwasa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo ilikuwa chini ya asilimia 50 kwa maeneo yote ya vijijini.


Pia alisema,Ruwasa wilaya ya Lindi inaendelea kutekeleza jumla ya miradi 9 ambayo ni mradi wa maji Navanga Corridor,mradi wa Nyangao-Mtama,mradi wa Namunda-Mnolela,mradi wa Mawilo,mradi wa Kilangala,mradi wa Milola,mradi wa Moka-Matimba na mradi wa Mputwa.


Pazi alitaja gharama za miradi hiyo ni Sh.bilioni 13,241,717,532.44 na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na baadhi ya miradi hiyo imeanza kutoa huduma ya maji kwa jamii.

Alieleza kuwa,kwa ujumla miradi hiyo itakapokamilika itawezesha kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 10.6 hivyo kufikia asilimia 86.6 kiwilaya ifikapo mwaka 2025.

 

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Tulieni Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi wakichota maji katika kituo mojawapo kinachotoa huduma hiyo.
 

Mwenyekiti wa kijiji cha Tulieni Halmashauri ya Mtama wilayani Lindi Mikidad Likwati kulia,akizungumza na wakazi wa kijiji hicho kuhusu umuhimu wa kutunza na kulinda miundombinu ya maji baada ya mradi wa maji Tulieni unaohudumia kijiji hicho na kijiji cha Moka kukamilika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...