Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kampeni ya Kitaifa ya Kuhamasisha Uwekezaji wa ndani, mwaka 2024 imeendelea kushika kasi katika mikoa mbalimbali nchini, ambapo watumishi wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) wapo bega kwa bega kutembea mikoani humo kuhamasisha uwekezaji huo kuanzia Januari 8 hadi Februari 9, 2024.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema Kampeni hiyo ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani ni lengo la Serikali kuongeza na kukuza shughuli za uchumi wa nchi.
“Matokeo ya uwekezaji katika nchi, hujitokeza katika kuongeza ajira, kuongeza mapato ya Kodi, kupunguza uagizwaji wa bidhaa kutoka nje na kuongeza mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi,” amesema Prof. Kitila
Aidha, Prof. Kitila amesema Serikali imeendelea kupata mafanikio mbalimbali katika kuhasisha, kuvutia na kuwezesha uwekezaji nchini. Amesema mwaka 2023, TIC ilifanikiwa kusajili jumla ya miradi 504 yenye thamani ya Dola za kimarekani 5.6 Bilioni na inayotarajiwa kuzalisha ajira 230,000. “Lengo la Serikali ni kuvutia uwekezaji wenye thamani ya dola za kimarekani Bilioni 15 ifikapo mwaka 2025.”
Vile vile, Prof. Kitila amesema Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji Uwekezaji (National Investment Promotion Campaign), iliyozinduliwa na Waziri Mkuu, Tarehe 25 Septemba 2023, Kampeni hiyo ina lengo la kutoa msukumo maalum kwa Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini.
Pia, Serikali imetoa ombi kwa Viongozi wote wa umma na sekta binafsi katika ngazi za mikoa na wilaya kutoa ushirikiano katika Kampeni hiyo muhimu ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani mwaka huu wa 2024.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akizungumza na Waandishi wa Habari (Hawapo pichani) wakati akizungumzia Kampeni ya Kitaifa ya Kuhamasisha Uwekezaji wa ndani, mwaka 2024 inayoendelea mikoa mbalimbali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akizungumzia Kampeni ya Kitaifa ya Kuhamasisha Uwekezaji wa ndani, mwaka 2024 inayoendelea mikoa mbalimbali. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...