Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda (katikati) akikata utepe pamoja na Mkuu wa Masoko na Mauzo wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Neema Patrick (wa pili kushoto) wakati wa uzinduzi rasmi wa Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2024 katika hoteli ya Salinero Mjini Moshi. Wengine kutoka kushoto ni Meneja Masoko wa Gee Soseji, Magreth Karua, kaimu Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Daniel Mainoya na Mkurugenzi wa Salinero Hotels, Ben Mengi.
Mkurugenzi wa Sal Salinero Hotel, Ben Mengi.
Kaimu Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Daniel Mainoya.
Meneja Masoko wa Gee Soseji, Magreth Karua.
Meneja Masoko wa Kanda ya Kaskazini wa Kampuni ya Bia Tanzania, Neema Patrick.

TOLEO la 22 la Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2024 limezinduliwa Ijumaa katika Hoteli ya Salinero iliyoko Moshi, mkoani Kilimanjaro, jambo ambalo linaashiria wazi kwamba siku ya tukio hilo linalotarajiwa kufanyika la Februari 25, 2024 imekaribia.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Katibu Tawala wa Mkoa huo Tixon Nzunda, aliwapongeza waandaji wa mbio hizo kwa hatua iliyofikia hadi sasa tangu kuanzishwa kwake hasa kwa mchango wake katika kukuza utalii wa michezo na uchumi wa Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.

“Tunajivunia mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon kwani zimeonekana kuwa moja ya matukio makubwa ya kimataifa katika ukanda huu kwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 12,000 na idadi kama hiyo ya watazamaji kutoka zaidi ya nchi 56 ambao wote hawa ni watalii watarajiwa”, amesema na kuongeza, hili ni tukio kubwa sana na muhimu kwa Taifa letu.

Nzunda aliendelea kusema kuwa hakuna mashindano mengine yanayoweza kufikia Kilimanjaro Marathon kwa maana ya matokeo yake katika kukuza uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuna haja kubwa kwa wadau wote wa michezo na wale wanaohusika na maswala ya biashara kufanya kazi kwa karibu katika kuhakikisha mashindano hayo makubwa yanaendelea kuweko kwa mstakabali mzuri wa kukuza michezo pamoja na uchumi wa Taifa na watu wake.

 "Tumekuwa tukiandaa mbio za marathon kwa miaka 22 sasa na jumuiya ya wafanyabiashara itakubaliana nami kwamba kwa kawaida wakati wa mbio hizi ni msimu wa biashara aina mbalimbali mkoani hapa kukua ikiwa ni pamoja na hoteli zote na nyumba za kulala wageni kufanya biashara kubwa”, alisema.

Aliongeza, “Nitoe wito kwa wafanyabiashara wote kuzingatia ubora wa bidhaa zao pamoja na huduma watakazotoa ili kuhakikisha wageni wanapata thamani ya fedha watakazotumia”.

“Nichukue fursa hii kuwapongeza wadhamini wote wa mbio hizi wakiongozwa na Kilimanjaro Premium Lager (mdhamini mkuu) na Tigo-21km Half Marathon, Gee Soseji wanaodhamini 5 km Fun Run kwa mchango wenu mkubwa”, alisema na pamoja na wadhamini wenza ambao ni Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies, CRDB Bank na TPC Sugar, pamoja na Washirika rasmi ambao ni pamoja na Garda World, CMC Automobiles, Salinero Hotels na wasambazaji - Kibo Palace Hotel na Keys Hotel; bila ya nyinyi isingekuwa rahisi kufanikisha mbio hizi,” alisema, ambapo alitoa wito kwa washiriki wa Kitanzania kujiandaa vyema ili kuhakikisha zawadi nyingi zinabaki nyumbani.

Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya Bia Tanzania, Kanda ya Kaskazini Mashariki, Neema Patrick amesema wanajivunia kupitia Kilimanjaro Premium lager, kudhamini hafla hiyo kwa miaka 22 iliyopita na kuwa miongoni mwa udhamini wa muda mrefu nchini Tanzania, ambapo alisema mbio hizo zimeendelea kuchangia utalii na utamaduni wa Mtanzania kwa ujumla.

Amesema TBL imetenga Tsh milioni 28 ikiwa ni zawadi ya fedha huku washindi wa kwanza katika kitengo cha wanaume na wanawake wakitarajiwa kupata zawadi ya Tsh milioni 4 kila mmoja.

Alitoa wito kwa wanaotarajia kushiriki mbio hizo kujiandikisha kwa wakati kwani usajili tayari unaendelea kupitia www.kilimanjaromarathon.com.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Daniel Mainoya amesema,“Tunayo furaha kubwa kuwa wadhamini wa mbio za Tigo Half Marathon kwa mwaka wa tisa mfululizo; Tigo Half Marathon inawahusisha washiriki zaidi ya 6,000 kwa wakati mmoja wakiwemo wanariadha wa daraja la juu Barani Afrika; napenda kuwajulisha ya kuwa zawadi katika kitengo hiki zimeongezeka”, amesema.

Aliongeza, “Dirisha la usajili katika kitengo hiki linaendelea na washiriki wanaweza kupiga *150*01#, kisha bonyeza 5 LKS, kisha bonyeza 5 (Tiketi) na kufuata maelekezo ili kukamilisha usajili wao. 

Meneja wa Biashara na Masoko wa Gee Soseji, Margaret Karua, ambaye kampuni yake ndiyo wadhamini wapya wa 5 KM Fun Run amesema, mashindnao hayo ni jukwaa sahihi la kutangazia bidhaa za kampuni hiyo.

“Kwa kushiriki mbio hizi, tutashirikiana na watumiaji wa bidhaa yetu kwa njia ya kujifurahisha na kuelimishana juu ya faida za kutumia bidhaa yetu kwa ajili ya kujenga afya kwa ujumla”, amesema na kuongeza, dhamira yetu ni kufanya mapinduzi katika soko la soseji kwani tumekuja na soseji zenye ubora, zilizoandaliwa kwa usafi, za gharama nafuu na zenye ladha nzuri zitakazovutia watu wengi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Salinero Hotels ambao ndiyo walikuwa wenyeji wakati wa uzinduzi huo, Ben Mengi amesema mashindano hayo yamekuwa chachu kubwa katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro ikiwemo sekta ya utalii kupitia michezo.

“Sisi tunayo fahari kubwa kuwa sehemu ya mashindano haya maarufu ulimwenguni kwa sasa; katika kuhamasisha washiriki wa mbio hizi Salinero inaahidi kutoa ofa kwa washindi wa kwanza wa 42 km na 21 km katika vitengo vyote vya wanaume na wanawake ya kulala usiku mmoja katika Serengeti Lodge”, alisema.

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon zitakazofanyika Jumapili Februari 25, 2024 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), zimeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...