Na Lusajo Mwakabuku – WKS Njombe

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema serikali imedhamiria kuhakikisha mradi huu unatekelezwa mapema iwezekanavyo ndio maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha malipo ya fidia kwa wananchi wote waliopisha eneo la utekelezaji wa mradi mkubwa wa Liganga na Mchuchuma Wilayani Ludewa Mkoani Njombe.

Waziri Chana ameyasema hayo tarehe 05/01/2023 akiwa katika Kijiji cha Nkomang’ombe kilichopo katika wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani humo akitekeleza jukumu lake la kusimamia misingi iliyowekwa na Sheria Sura 449 na 450 yenye lengo la kuhakikisha uwekezaji katika uvunaji na matumizi ya utajiri asili na maliasilia za nchi unatekelezwa kwa namna ambayo inainua hali ya wananchi kiuchumi na kuongeza pato la Taifa.

“Lengo la ziara hii ni kufuatilia utekelezaji wa Sheria hizi katika miradi ya Liganga na Mchuchuma. Aidha, Sheria hizi zinaweka misingi ya kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Ludewa na waliopo karibu na maeneo ya miradi hii wananufaika na fursa zinazopatikana katika uwekezaji wa rasilimali za Taifa. Kwa mfano, ni matarajio ya Serikali kuwa, uwekezaji wa namna hii itatoa ajira kwa watanzania, itatoa fursa ya watanzania kusambaza zabuni kwa watanzania na kuwapa mafunzo yanayolenga kuhuwisha teknolojia kwani kwa kufanya hivyo ndiyo utekelezaji wa misingi iliyowekwa na Sheria zetu.”alisema Waziri Chana.

Aidha Waziri Chana amesema kuwa pamoja na kwamba mradi huu una historia ndefu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha nia ya wazi ya kutekeleza mradi huu kwa kutoa kiasi hicho cha fedha ili mradi huu wa Liganga na Mchuchuma unaojumuisha uchimbaji wa chuma cha Liganga pamoja na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma uanze kazi mara moja baada ya maafikiano ya kimikataba kufikiwa.

Waziri Chana pia akatumia nafasi ya ziara yake ya siku mbili hii kuongea na wananchi wa vijiji vya Nkomang’ombe na Mundindi ambapo miradi hii inatekelezwa na kuwataka wawaandae vijana wao katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kielimu, uwekezaji mdogo mdogo na ujuzi ili mradi utapoanza basi waitumie nafasi hiyo vizuri kuhakikisha wanufaika wa kwanza wanakuwa wananchi wa maeneo husika.

Akiongelea hatua mbalimbali za kitaalam ambazo mradi huu umepitia, Meneja wa Mradi wa Liganga na Mchuchuma kutoka NDC Dkt. Witness Ishuza alisema “Mwaka 2013 Tafiti ya Makaa za Mawe pamoja na Chuma zilifanyika, kwa kipindi hicho na kugundua kwamba kuna tani milioni 428 za Makaa ya mawe katika eneo la ukubwa wa mraba 30 ambazo zinaweza kuchimbwa kwa miaka zaidi ya 140 na Chuma ambacho ni zaidi ya tani milioni 126 ambacho kinaweza kuchimbwa kwa miaka 58 “amesema Dkt. Ishuza.

Naye Mwenyekiti wa CCM katika Wilaya ya Ludewa amesema Rais Samia amefanya jambo kubwa kwani ametekeleza jambo ambalo ni kiu kubwa ya wananchi na kwamba Taifa na litakwenda kusonga mbele kwani mradi huu unaokwenda kubadilisha uchumi wa taifa letu, na kupunguza gharama kubwa zinazotumika katika kuagiza chuma kutoka nje tena kwa kutumia fedha za kigeni, hivi viwanda vyote vya nondo, viwanda vya umeme, viwanda vya mabati, vitatumia chuma chetu.

Rafael Memba ni mmoja wa wanufaika wa fidia ya kupisha mradi wa Liganga na Mchuchuma na mkazi wa Kijiji cha Nkomangombe alimshukuru Mhe.Rais Samia kwa kutimiza ahadi yake ya kulipa fidia licha ya kusubiri muda mrefu na pia akaiomba serikali kuhakikisha taratibu mbalimbali zinazokwamisha mradi huu kuanza zimalizike kwa haraka ili mradi huu uweze kufanyika kwa haraka na kuleta mafanikio kwao binafsi na kwa Taifa kwa ujumla.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Njombe alipowasili mkoani humo kwa ajili ya ziara ya siku mbili kwenye mradi wa Liganga na Mchuchuma 05/01/2024
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiongea na wananchi wa kijiji cha Nkomang’ombe wilayani Ludewa ambapo mradi wa Mchuchuma unatekelezwa.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana na viongozi pamoja na wananchi wa kijiji cha Nkomamanga wakiimba na kumfurahia Rais Samia baada ya kupata taarifa za mradi wa Liganga na Mchuchuma.
Mkurugezi wa kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asili na Maliasilia za Nchi Kamishna Neema Mwanga akitoa taarifa ya kisheria juu ya utekelezwaji wa mradi huu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...