Wanaume wameaswa kuweka kipaumbele katika kushiriki kwenye masuala mazima ya uzazi wa mpango ikiwemo kutumia njia za Uzazi wa Mpango katika kupanga uzazi ili kutoa nafasi kati ya mtoto na mtoto.
Hali hii itaimarisha Afya ya mama na mtoto na familia itapata muda wa kushiriki kwenye shughuli za kujitafutia kipato pia itaupunguza idadi kubwa ya Watoto ambao wanazaliwa na kukosa matunzo ipasavyo.
Akiongea na Michuzi Media, Mratibu wa Huduma za Uzazi wa Mpango Kitaifa kutokea Wizara ya Afya Dodoma, Zuhura Mbuguni amesema kuwa zipo njia mbalimbali za Uzazi wa Mpango kwa ajili ya Wanaume ambazo ni rahisi zaidi na kuwa elimu ikitolewa vizuri basi itasaidia kwa kiwango kikubwa matumizi ya Uzazi wa Mpango kwa Wanaume.
Amezitaja njia za Uzazi wa Mpango ambazo zinawagusa Wanaume moja kwa moja kuwa ni matumizi ya kondomu, pamoja na kufunga mirija ya uzazi ingawa mpaka sasa watumiaji ni wachache kutokana na ‘mfumo dume’.
Aidha, Mbuguni ameongeza kuwa baada ya kutolewa elimu hiyo Wanaume katika Kanda ya Magharibi wameonesha muitikio mkubwa katika kutumia njia hizi za Uzazi wa Mpango hasa njia ya kufunga mirija.
“Tuna kazi ya ziada kufanya kwa Wanaume, lakini tuna imani kama elimu itafika vizuri na wataelewa umuhimu wa hii huduma nafikiri wataungana na wenza wao kuhakikisha kwamba wenza wao wanatumia au wenyewe wanatumia.
“Kama mama alizaa labda alizaa kwa operesheni, baada ya idadi yenu ya Watoto kufika unaonaje wewe ukafunga ili muendelee kulea familia yenu,” anaeleza Mbuguni.
Kulingana na takwimu ya viashiria vya Afya ya Uzazi na Malaria, Mbuguni aliutaja Mkoa wa Simiyu kuwa ni mkoa ambao upo chini katika matumizi ya njia za Uzazi wa Mpango, hivyo kufanya kiwango cha uzazi kuwa juu huku Mkoa wa Mtwara ukiwa na kiwango kidogo zaidi cha uzazi yaani Mwanamke mmoja kuzaa watoto wachache.
Ameongeza kuwa Mila na Desturi ambazo zinakinzana na matumizi ya uzazi wa mpango zimekuwa ni changamoto kubwa ambapo wataalamu wanakutana nazo wakati wa kutoa elimu juu ya uzazi wa mpango.
Home
HABARI
Wanaume washauriwa kushiriki kwenye masuala ya Uzazi wa Mpango ili kuimarisha Afya ya Mama na Mtoto
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...