Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb.) na Balozi wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian wakionesha mikataba mara baada ya kusaini leo Januari 18, 2024 jijini Dar es Salaam.msaada wa kugharamia ununuzi wa zana na vifaa vya kijeshi wenye thamani ya Chinese Yuan RMB milioni 100 sawa takriban Shilingi za Kitanzania 35,030,000,000.
WAZIRI wa Ulinzi na JKT,
Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb.) na Balozi wa China nchini
Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian kwa pamoja wametiliana saini mikataba miwili
baina ya Wizara ya Ulinzi na JKT ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara
ya Ulinzi ya Jamhuri ya Watu wa China kuhusu msaada wa kugharamia ununuzi wa zana
na vifaa vya kijeshi wenye thamani ya Chinese Yuan RMB milioni 100 sawa takriban
Shilingi za Kitanzania 35,030,000,000.
Akiongea maneno ya utangulizi
kabla ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, kwa niaba ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla,
ametoa shukurani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na
Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (Peoples Liberation Army), kwa msaada wa
zana na vifaa vya kijeshi kupitia mpango maalum wa Jumuiya ya Afrika (AU),
ambapo China iliridhia kuipatia msaada Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kupitia JWTZ.
Aidha, Mheshimiwa Waziri
ameongeza kusema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini
misaada isiyo na ukomo, inayoendelea kutolewa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China kupitia sekta ya ulinzi hususan JWTZ.
Jitihada zote na kujitoa huko kunaziwezesha Serikali hizi mbili
kushirikiana na kufanya kazi kwa Karibu. Akitoa mfano wa tukio la leo, ambalo ni
kielelezo tosha katika kukuza na kuendeleza ushirikiano wa kihistoria uliodumu
kwa muda mrefu baina ya mataifa haya.
Vile vile, Dkt. Stergomena
amebainisha kuwa kusainiwa kwa mikataba hii, kunaashiria ni kwa namna gani
mataifa haya mawili, yalivyo na dhamira ya dhati katika kudumisha ushirikiano, kuendelea
kusaidiana na kuimarisha urafiki wa kindugu.
Waziri Stergomena
amemhakikishia Mheshimiwa mingjian pia, kuwa Wizara ya Ulinzi na JKT,
itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China katika
kuendeleza ushirikiano baina mataifa haya mawili, lengo likiwa kuimarisha
majeshi haya mawili (PLA na JWTZ), na ni imani yake kuwa kwa kufanya kazi
pamoja na kwa umoja wao wataweza kukabiliana na changamoto za kiulinzi zilizopo
na zitakazoibuka siku za usoni.
Mheshimiwa Dkt. Stergomena pia,
amemshukuru na kumpongeza Balozi Mingjian na timu yake pamoja na timu ya Wizara
ya Ulinzi na JKT, kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya. Ushirikiano wa dhati baina
ya mataifa ya Tanzania na China ni hatua muhimu katika kudumisha na kuimarisha mahusiano,
katika kujenga umoja wenye nguvu na wa kina, na wenye undugu baina ya mataifa
haya mawili.
Kwa upande wake, Balozi
anayeiwakilisha Jamhuri ya Watu wa China hapa nchini, Mheshimiwa Chen Mingjian
amebainisha kuwa uhusiano baina ya Jeshi la Ukombozi la Watu wa China na JWTZ ulianza
tangu mwaka 1964, mara tu baada ya kuundwa kwa JWTZ. Aidha, ameainisha maeneo
mbalimbali ya ushirikiano baina majeshi ya nchi hizi mbili. Ameyataja maeneo
hayo kuwa ni pamoja na misaada ya kijeshi, zana na vifaa, mafunzo ya pamoja,
tiba, na viwanda vya kijeshi.
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
nchini, Jenerali Jacob John Mkunda akitoa neno la shukrani, amemhakikishia
Balozi Chen kuwa JWTZ litatumia msaada uliotolewa na Serikali yake kwa Jeshi,
utatumika ipasavyo na kwa ufanisi mkubwa, ili kuleta matokea chanya katika
kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...