Na. Farida Ramadhani na Saidina Msangi, WF, Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, amekabidhi kadi 100 za Bima ya Afya za Mfuko wa Bima ya Taifa (NHIF) kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Maalum ya Wasioona, Buigiri, iliyoko Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi kadi hizo iliyofanyika katika shule hiyo, Bi. Omolo alisema kadi hizo sehemu ya kutekeleza ahadi iliyotolewa na watumishi wanawake wa Wizara hiyo mwaka 2023.

“Sisi kama jamii ya watumishi wanawake wa Wizara ya Fedha, kwa niaba ya Katibu Mkuu wetu, Dkt. Natu El – maamry Mwamba, tumeleta Kadi hizi ili kuwarahishia matibabu watoto wetu, tunaamini hatua hii itarudisha tabasamu kwa watoto wetu ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu na kuongeza ari ya kufanya vizuri zaidi katika masomo yao ili kufikia malengo wanayoyatarajia”, alisema Bi. Omolo.

Alisema kadi hizo zina vifurushi vya mwaka mmoja na kuahidi kuwa Wizara itaendelea kuwalipia vifurushi kila mwaka.

Alitoa wito kwa taasisi na watu binafsi nchini kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao.

Aidha, aliupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kuendelea kuwalea watoto hao katika maadili mema.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Samwel Jonathan, aliishukuru kwa msaada huo muhimu kwa afya za Watoto na kuomba Wizara iendelee kuwakumbuka kila wakati.

Naye Mwanafunzi wa Shule hiyo, Stanley Keneth, aliishukuru Wizara kwa kuwapatia kadi hizo na kubainisha kuwa bima hizo zitawasaidia kupata matibabu watakapopata changamoto za kiafya..

Bi Lucy Assay, ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Chamwino, aliishukuru Wizara ya Fedha kwa msaada huo na kutoa rai kwa jamii kutowaficha Watoto wenye mahitaji maalumu majumbani ili wapate elimu kwa kuwa shule zipo kulingana na namna ya ulemavu.

‘‘Niwashukuru sana kwa msaada mliotoa kwa kuwa sasa watoto wetu wataweza kupata huduma za afya na nitoe rai kwa jamii kuwa na moyo wa kusaidia watu wenye mahitaji maalumu’’alisema Bi. Lucy.

Shule ya Msingi Buigiri ni ya pekee mkoani Dodoma inayotoa elimu ya makundi maalum na ilianzishwa Aprili 30, 1950, inafundisha Watoto wenye uoni hafifu, wasioona pamoja na wenye ulemavu wa ngozi kuanzia shule ya awali hadi darasa la saba.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi.Jenifa Christian Omolo, akizungumza na wanafunzi pamoja na uongozi wa Shule ya Msingi Maaluum ya Wasioona Buigiri iliyopo Chamwino mkoani Dodoma baada ya kuwakabidhi kadi 100 za bima ya afya za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), mkoani Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi.Jenifa Christian Omolo (wapili kushoto) na wawakilishi wa viongozi wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE tawi la Wizara hiyo, wakifurahia nyimbo mbalimbali zilizoimbwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Maaluum ya Wasioona Buigiri iliyopo Chamwino mkoani Dodoma baada ya kuwakabidhi kadi 100 za bima ya afya za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), mkoani Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi.Jenifa Christian Omolo (wa kwanza kushoto) akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Maaluum ya Wasioona Buigiri, Bw. Samwel Jonathan (wa kwanza kulia) kadi 100 za bima ya afya za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo, mkoani Dodoma. Kulia kwake ni wawakilishi wa viongozi wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE tawi la Wizara hiyo, Bi. Scholastica Okudo, Bi. Halima Juma, Bi. Mariam Kiangi na Afisa Elimu Kata ya Buigiri, Mwalimu Emmanuel Otta.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi.Jenifa Christian Omolo na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Maaluum ya Wasioona Buigiri, Bw. Samwel Jonathan wakimkabishi Mwanafunzi wa Darasa la Awali wa Shule hiyo, Zulfat Ibrahimu,  kadi ya bima ya afya za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani Dodoma. Wakishuhudiwa na wawakilishi wa viongozi na wajumbe wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE tawi la Wizara hiyo, Bi. Hilda Segele, Bi. Scholastica Okudo, Bi. Halima Juma, Bi. Mariam Kiangi na Mwalimu wa Shule hiyo, Wakati Joseph.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi.Jenifa Christian Omolo, akiwa katika picha na wanafunzi wa Shule ya Msingi Maaluum ya Wasioona Buigiri, iliyopo Chamwino mkoani Dodoma, baada ya kuwakabidhi kadi 100 za bima ya afya za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kurahisisha matibabu.
 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...