Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ulaya, Wilayani Mikumi mara baada ya kukagua barabara ya Dumila-Kilosa-Ulaya-Mikumi (Km 142) kwa kiwango cha lami, Mkoani Morogoro
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akikagua moja ya Daraja katika Barabara ya Dumila-Kilosa, Mkoani Morogoro.
Muonekano wa Barabara ya Rudewa-kilosa (Km 24 ) kwa kiwango cha lami, Mkoani Morogoro.

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kuipandisha hadhi barabara ya Tanga - Kilosa - Mikumi - Lupembe kuwa barabara kuu 'Trunk Road' ili kuinua uchumi wa mikoa ya Tanga, Morogoro na Njombe.

Bashungwa, ameyasema hayo mkoani Morogoro wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Dumila-Kilosa-Ulaya-Mikumi (km 142) kwa kiwango cha lami sehemu ya pili, Rudewa-Kilosa (km 24), ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 98.

“Barabara inayoanzia Tanga bandarini kupitita Handeni - Mziha - Dumira - Kilosa - Mikumi - Ifakara mpaka Lupembe mkoani Njombe lazima tuitangaze iwe ni mojawapo ya barabara kuu ‘Trunk road’ ili iweze kuipatiwa bajeti ya kutosha na kuweza kuihudumia wakati wote”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amemtaka Mkandarasi M/s Umoja - Kilosa Jv anayetekeleza mradi huo kufanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha barabara na madaraja yanakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa kwenye mkataba kwani fedha zote zimeshalipwa na ifakapo mwezi wa nne mwishoni waikabidhi barabara hiyo kwa wananchi.

Bashungwa akijibu ombi la Mbunge wa Kilosa, Prof. Palamagamba Kabudi la uwekaji wa taa, amesema Wizara itatenga bajeti ya ufungaji wa taa 120 katika kipande cha kilometa tatu katika barabara ya Rudewa - Kilosa.

Aidha, Waziri Bashungwa amemuelekeza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Morogoro kuhakikisha wanatenga bajeti za matengenezo ya upanuzi wa njia ya maji katika mito yote ili mvua zitakaponyesha zisilete athari kwenye miundombinu ya barabara.

Akitoa taarifa ya mradi kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Miradi, Mhandisi Malima Kusesa, amesema mradi wa ujenzi wa barabara ya Dumila-Kilosa-Ulaya-Mikumi (km 142) kwa kiwango cha lami sehemu ya pili, Rudewa-Kilosa (Km 24) umefikia asilimia 98.3 na sehemu iliyobaki ni ujenzi wa madaraja matatu ambayo yanaunganisha barabara hiyo.

Vilevile ameongeza kwa kusema kuwa mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.

Kwa upande wake Mbunge wa Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani muhimu katika uchumi wa wana Kilosa.

Utekelezaji wa mradi huo ni moja ya mkakati wa Serikali katika kukuza uchumi na kuunganisha mikoa ya kaskazini (Tanga, Kilimanjaro na Arusha) na Mikoa ya Kusini (Iringa, Mbeya na Ruvuma) kupitia Turiani na Mziha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...