NA BALTAZAR MASHAKA,NYAMAGANA

SERIKALI ya Wilaya ya Nyamagana imesema sh.milioni 800 zitatumika kutatua changamoto ya elimu katika Kata ya Igoma na kuwaepusha wanafunzi kusafiri umbali mrefu kupata huduma ya elimu ya sekondari nje ya kata hiyo.
Akizungumza na wananchi wa mitaa ya Shamaliwa A na Kilimo B katika mkutano wa hadhara leo,Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi,amesema dhamira ya serikali ni kuleta maendeleo ya wananchi kwa usawa katika sekta mbalimbali bila kujali itikadi za vyama.

Amesema serikali inaendelea kuboresha sekta ya elimu na kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)inatekeleza mradi wa bwalo la chakula,madarasa matatu na matundu sita ya vyoo katika shule ya sekondari Shamaliwa kwa sh. milioni 401 utakaoiwezesha kuchukua wanafunzi wa kidato cha tano na sita wanaolazimika kwenda kusoma nje ya kata hiyo.

Makilagi amesema mradi huo ulioibuliwa na wananchi wenyewe watachangia asilimia 10 (nguvu kazi) na TASAF asilimia 90 fedha ambazo zimetolewa na wadau wa maendeleo wakishirikiana na serikali.

Pia,kutokana na mahitaji ya shule kwa wananchi wa Igoma serikali imeridhia kutoa sh.milioni 400 za kujenga sekondari mpya isaidiane na Shamaliwa watoto wasiende umbali mrefu hivyo imewekeza jumla ya sh.milioni 801 zikatatue changamoto ya elimu katika Kata ya Igoma.

“Maendeleo ni kujinyima na mradi huu msiuache,wakati wengine wanaandamana sisi tunajenga shule.Je,mnahitaji shule au maandamano (akijibiwa,tunataka shule).Basi kazi imekwisha,mjitoe kuchangia kwa ajili ya watoto wetu wakiwemo waliooa na wasioolewa mradi ukamilike tupate mingine,”amesema Makilagi na kuongeza kuwa hata Roma haikujengwa siku moja,tuko kazi na Mama yuko kazini,Kazi Iendelee.

Naye Diwani wa Igoma (CCM),Mussa Ngollo na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Uchumi,Elimu,Afya na Mazingira Jiji la Mwanza,amesema shule ya Shamaliwa mwaka huu imesajili wanafunzi 1,100 wa kidato cha kwanza,imeelewa zaidi na haiwezi kuwa na ufanisi mzuri wa elimu.

“Tuna jumla ya shule za msingi 16 kati ya hizo za serikali ni 8 ambapo wastani kila mwaka watoto 2,000 wanahitimu na wanaokosa nafasi Shamaliwa wanapangiwa shule zingine za sekondari Pamba,Mwanza,Mabatini na Mirongo ambazo ziko mbali,”amesema.

Ngollo ameeleza kuwa changamoto ya umbali watoto wanalazimika kuamka alfajiri kuwahi usafiri,huko njiani wasichana wanakumbana na madhila ya kukabwa na kuporwa,hivyo hitaji la shule nyingine ya sekondari Kata ya Igoma halikwepeki.

“Igoma tumenufaika kwa mradi huu wa elimu ambao ni nadra kuupata,ni fursa tukiukamilisha tutakuwa tumejenga daraja la kupata miradi mingine maana bado Shamaliwa tunahitaji jengo la utawala na nyumba ya mwalimu,”amesema.

Kwa mujibu wa diwani huyo kwa miaka mitatu mfululizo shule hiyo ya Shamaliwa katika matokeo ya kidato cha nne imeendelea kufanya vizuri na mwaka huu imeshika nafasi ya kwanza mkoani Mwanza na kuiheshimisha Wilaya ya Nyamagana.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, akiwahamasisha  wananchi wa mitaa ya Shamaliwa A na Kilimo B, Kata ya Igoma  kuchangia ujenzi wa mradi wa  bwalo la chakula, madarasa matatu na matundu sita ya vyoo katika shule ye sekondari Shamaliwa , leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mtaa wa Shamaliwa A.  
 

Wananchi wa mitaa ya Kilimo B na Shamaliwa A wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (kulia) alipohutubia mkutano wa hadhara leo, akihamasisha wananchi hao kuchangia asilimia 10 ya mradi wa bwalo la chakula, madarasa matatu na matundu sita ya vyoo, unaotekelezwa na TASAF kwa sh. milioni 401 katika  shule ye sekondari Shamaliwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...