ZANZIBAR
MKURUGENZI wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt. Mzuri Issa, amehimiza vyombo vya habari kuripoti kwa kina mapungufu ya sheria za habari za Zanzibar ili zifanyiwe marekebisho na kutoa fursa kwa wananchi kupata habari bila vikwazo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kikao cha uzinduzi wa ripoti ya mapitio ya sheria za habari zenye vifungu vinavyokwaza uhuru wa habari Zanzibar alisema, iwapo vyombo vya habari vitapaza sauti kwa pamoja kushawishi mabadiliko itachochea kasi ya marekebisho ya sheria hizo.

"Waandishi wa habari tutumie nafasi kupaza sauti zetu juu ya mapungufu ya kisheria yaliyopo ili zifanyiwe marekebisho, hii itawapa watu furaha na kujisikia kuwa ni sehemu ya nchi kwa kutoa maoni yao bila hofu," alieleza Dkt. Mzuri.

Alibainisha kuwa waandishi wa habari wakiwa na uwezo wa kutoa maoni yao bila hofu itarahisisha upatikanaji wa taarifa na kuongeza uwajibikaji katika nyanja mbalimbali.

"Kukiwa na uhuru wa habari itasaidia kupunguza madhaifu yaliyopo kwenye sekta ya habari kwa kudhibiti waandishi holela wanaotoa taarifa feki na kuifanya sekta ya habari kuwa imara na kutoa taarifa ambazo zinakidhi misingi ya uandishi." Alieleza.

Akiwasilisha ripoti hiyo, Said Suleiman ambaye ni mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar alisema uchambuzi wa sheria hizo umebaini kuwepo baadhi ya vifungu vinavyokwaza uhuru wa habari.

Aliongeza kuwa ripoti hiyo imepitia jumla ya sheria nane (8) ambazo ni Sheria ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria no.8 ya 1997, Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 iliyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010.

Nyengine ni sheria ya Adhabu ya Mwaka 2004 (Sheria Na. 6) iliyorekebishwa mwaka 2018, Sheria ya kufuta Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya mwaka 1984 na kutungwa kwa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2017 na mambo mengine yanayohusiana na hayo pamoja na Sheria ya Baraza la Wawakilishi Na 4 ya mwaka 2007 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Alieleza kuwa Sheria ya Tume ya Utangazaji Na. 7 ya 1997 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria Na. 1, 2010 inahitaji kufanyiwa marekebisho kifungu cha 27 (2) kutokana na kutoa mamlaka zaidi kwa viongozi.

"Sheria ya Tume ya Utangazaji No. 7 ya 1997 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria No. 1, 2010 viongozi wamepewa mamlaka makubwa sana mfano kifungu cha 27 (2). Waziri amepewa mamlaka makubwa sana ya kuchukua maamuzi yoyote," alieleza mkufunzi huyo.

Alipendekeza sheria na sera kuwekewa vifungu vinavyoweka mazingira ya usalama wa waandishi wa habari ili kuwalinda dhidi ya uvunjifu wa uhuru wa kujieleza.

Alisema, "Sera na sheria lazima zihusishe vifungu vinavyohakikisha usalama wa waandishi wa habari, wanaharakati na wasomaji ili kuwaweka katika mazingira salama."

Jabir Idrissa, ambaye ni mdau wa habari alisema, uwepo wa sheria zinazokwaza uhuru wa habari imepelekea Zanzibar kukosekana kwa vyombo vya habari binafsi kwa upande wa magazeti kutokana na urasimu katika utekelezaji wa sheria hizo.

"Mpaka leo Zanzibar hakuna Gazeti binafsi, ambapo kabla ya Mapinduzi kulikuwa na magazeti mengi Zanzibar, historia ya uandishi wa habari Zanzibar ni ya muda mrefu lakini imekufa kutokana na uwepo wa sheria zisizo rafiki," alieleza mdau huyo.

Kikao hicho ni muendelezo wa juhudi za TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na wadau na waandishi wa habari Zanzibar katika kufanya ushawishi na utetezi wa mabadiliko ya sheria zenye vifungu vinavyokwaza uhuru wa habari kwa lengo la kupata sheria zilizohuru na zinazoendana na wakati katika tasnia ya habari nchini.Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...