Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu (kulia) akipokea tsheti ya kukimbia kutoka kwa Meneja Matukio wa Kilimanjaro Premium Lager International Marathon, David Marealle (kushoto) huku Meneja wa Itifaki wa mbio hizo, Nurdin Saggafu akishuhudia. Hafla hiyo ilifanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Moshi.
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu ametoa rai kwa wakazi wa mkoa huo hususan wafanyabiashara kutumia fursa za kibiashara zinazotokana na mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon.

Babu ametoa rai hiyo leo Februari 21,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maandalizi ya mbio hizo kwa upande wa serikali ya Mkoa.

“Mbio hizi zinatarajiwa kuhusisha zaidi ya washiriki 10,000 na idadi kama hiyo ya watu wengine watakaokuja mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kufuatilia mbio hizo muhimu Afrika Mashariki”, amesema na kuongeza idadi hiyo pia inahusisha washiriki na watu wengine kutoka nje ya nchi.

“Taarifa nilizonazo ni kuwa tayari nyumba za kulala wageni zote zimejaa hapa Moshi mjini na maeneo mengine yaliyoko nje ya Moshi Mjini na wengine wamechukua vyumba mkoa wa jirani wa Arusha”.

“Niendelee kutoa rai kwa wafanyabiashara kutumia fursa zingine za kibiashara mbali na za nyumba za kulala wageni kwani wakati wa tukio hili muhimu fursa zinakuwa ziko nyingi”, amesema.

Aidha Babu amewapongeza waandaaji wa mbio hizo ambapo amesema mbali na kuinua vipaji vya wanamichezo kwenye tasnia ya riadha, pamoja na kukuza uchumi wa koa na ule wa Taifa, pia mbio hizo zinaunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan zinazolenga kukuza sekta ya michezo hapa nchini.

Kuhusu maandalizi kwa ngazi ya Mkoa, Babu amesema yote yanaenda vizuri ikiwemo kuhakikisha usalama wa uhakika kwa washiriki na wananchi wengine watakaoshiriki kwenye tukio hilo la kimataifa.

“Sisi kwenye ngazi ya Mkoa tumejiandaa vizuri kwa ajili ya tukio hili muhimu na pia katika kuhakikisha usalama unakuwa ni wa uhakika kabla na baada ya mbio hizo”, amesema.

Aidha Babu ametoa rai kwa wale watakaotembelea Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa mbio hizo pia kuitumia fursa hiyo kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko mkoani humo, ambavyo ni pamoja na Mlima Kilimanjaro ambao una hadhi ya kipekee kimataifa.

Mkuu wa Mkoa Babu pia ameushukuru uongozi wa Kilimanjaro marathon kwa kutoa fursa kwa uongozi wa Mkoa huo kuandaa jogging maalum Feburuari 24, mwaka huu, ambayo mbali na kutumika kama kipasha moto kwa ajili ya mbio zinazotarajiwa kufanyika februari 25, mwaka huu, pia zitatumika kuwakumbusha wananchi tukio la kuwashwa Mwenge wa Uhuru kitaifa linalotarajiwa kufanyika mkoani Kilimanjaro Aprili 2, mwaka huu.

Kwa upande wake, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Catherine Lyakurwa amesema maandalizi yamefikia pazuri na washiriki wajiandae Kwa burudani ya aina yake kabla na siku ya mbio ambapo kutakuwa na matamasha mbalimbali uwanja wa Ushirika na Moshi Club.

"Mwaka huu tumeboresha zaidi ikiwemo kupanua eneo, safu kubwa zaidi ya wasanii na sehemu kubwa ya kuegesha magari,"amesema.

Naye, Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo amesema udhamini wao Kwa miaka tisa umekuwa na tija kubwa sana.

"safari hii tutafunga WIFI katika vituo mbalimbali Mjini Moshi na itakuwa bure kwa kila mtu,"ameeleza.

Meneja Masoko wa Gee Soseji, Margret Karua amesema wanakuja na mambo ya kusisimua hasa ikizingatiwa ni mara yao ya kwanza kudhamini mbio hizi.

Wadhamini wengine ni Mexa za maji- Simba Cement, TPC Sugar, CRDB Bank, Kilimanjaro Water, wabia wakuu- GardaWorld Tanzania, Salinero Hotel naCMC Automobiles na Wasambazaji wakuu Keys Hotel na Kibo Palace Hotel.

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon zinaandaliwa na kampuni ya Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...