SHAHIDI ambaye ni fundi Seremala, Dominic Mpakani (43) ameileza mahakama jinsi mtuhumiwa Bharat Nathwan (57) alivyomshambulia jirani yake, Lalit Ratilal kwa kumpiga kichwa kifuani kisha akadondoka chini na nakupoteza fahamu kwa muda.

Aidha, amedai kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya mke wa Bharat (Sangita Bharat) na mke wa Lalit, (Kiran) ambao walikuwa wakirushiana maneno kwa ukali kwa lugha ya kihindi huku, baada ya muda kidogo waume zao walifika kwa pamoja na kuingilia ugomvi huo.


Mpakani alidai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati alipokuwa akitoa ushahidi dhidi ya washitakiwa hao.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga aliyekuwa akisaidiana na Wakili Frank Michael, shahidi Mpakani amedai kuwa Julai 21,2023 alikuwa nyumbani kwa Lalit Ratilal maeneo ya mtaa wa Mrima katika jengo la Lohana ambapo alimuita kwa ajili ya kumfanyia kazi zinazohusiana na mbao na kazi zingine ndogo ndogo.


Amedai kuwa alifika katika jengo hilo saa tatu asubuhi ambapo bosi wake huyo anakaa floor ya tatu, wakati anaendelea na kazi alidai kuwa Sangita alikuwa amesimama kwenye dirisha lake na Kiran alikuwa amesimama kwenye mlango wake, kila mmoja alianza kuzungumza kwa ukali na kwa jaziba wakitumia lugha ya kihindi.

"Lakini nilimsikia mke wa Bharat, Sangita akimwambia mke wa Lalit kwamba uchafu wake apeleke huko ambapo vitu vyote vilikuwa vimewekwa katika eneo la Lalit na hakuna kitu chochote kilichokuwa katika eneo la Sangita. Baada ya dakika kadhaa sijui walipiga simu au vipi waume zao walikuja kwa wakati mmoja na malumbano yakaendelea kwa wote wanne," amedai Fundi Mpakani

Shahidi huyo ameendelea kudai kuwa, wakati malumbano hayo yanaendelea wote walikuwa wamesimama kwenye mlango wa Lalit, baada ya muda Bharat akampiga kichwa Lalit na Lalit akadondoka chini na kupoteza fahamu.

"Wakati Lalit yupo chini, Bharat alikuwa akiendelea kumpiga mateke, mke wa Lalit, Kiran akawa anazuia akiwa chini ndipo tukaachia kazi zetu kwenda kuamulia ugomvi, lakini Bharat alimsukuma mama huyo na kuzamisha kichwa chake ndani ya ndoo ya saruji iliyochanganywa na mchanga."

Alidai kuwa kuna fundi wa vigae ambae ndiye aliyekuwa amechanganya mchanganyiko huo kwa ajili ya kuweka vigae nyumbani kwa Lalit. Baada ya kumtoa Bharat ndipo alipoanza kutoa lugha ya matusi ikiambatana na maneno kwamba atamuonesha Lalit kuwa yeye ni nani.

"Tulipomtoa Bharat, Lalit alikuwa kama amepoteza fahamu kwa sababu alikuwa hatikisiki, ndipo tukambeba kumsusha floor ya chini tukamfungua vifungo vya shati na kuanza kumfuta futa ndipo akaamka akaitisha simu zake aka akapiga simu polisi na hospitali,"

"Gari la hospitali likafika likamchukua Lalit na mke wake na polisi wakamchukua Bharat, lakini walinihoji nikatoa maelezo yangu wakaondoka,"alidai.

Shahidi mwingine ambae ni Dkt. Lucia Augustino (52) wa Hospitali ya Mnanzi Mmoja amedai kuwa Julai 21,2023 alikuwa Idara ya Dharura chumba namba  20 muda wa mchana alipokea wateja wawili wenye asili ya kiashia walikuwa wamechafuka kuanzia kichwani hadi miguuni , mama alichafuka sana kuliko baba.

Alidai kuwa alianza kumuhudumia mama (Kiran) kwa kumnawisha na maji ya dripu kwa sababu macho yake yalikuwa yanatoa machozi na pia alikuwa akilalamika kwamba ana maumivu makali ya kichwa na alikuwa akilalamika kuhusina na kichwa alimuuita daktari wa macho ili aweze kumuangalia.

"Daktari alibaini kwamba jicho la upande wake wa kushoto limepata madhara sana ,mgonjwa aliandikiwa rufaa ya kwenda hospitali ya Regency ilkiyokuwa karibu na hospitali ya Mnazi Mmoja ili aweze kupata matibabu kutokana na kwamba hapo hakuna vifaa vyakufanya uchunguzi. Baada ya hapo tulimrudisha chumba namba 20, akachomwa sindano ya maumivu,"alidai Dkt. Augustino.

Dkt. Augustino amedai kuwa alimuangalia mwili mzima, alikuwa ana mamumivu kwenye masikio, macho na kichwa ndipo akamuandikia rufaa, akaondoka nikaanza kumuhudumia baba (Lalit) ambapo alikuwa akilalamika kuwa anaumwa sana kichwa, kizunguzungu na anaona maluwe luwe baada ya kushambuliwa.

Amedai kuwa alimchunguza hadi kwenye miguu, alibaini kwamba alikuwa amevimba kichwani upande wa kulia, kifuani na pia magoti yake yalikuwa yamechubuka, nilimuandikia sindano za kupunguza maumivu na pia nilimuandikia akafanye vipimo vya CT Scan.

"Licha ya kumchoma sindano ya maumivu bado alikuwa anajisikia muamivu makali, ndiyo nae akaandikiwa rufaa ya kwenda Regency kwa ajili ya uchunguzi zaidi,"Amedai.

Baada ya kumaliza kuwapa huduma zote, walienda kufanya vipimo wakamletea ripoti mbili. Lalit alirudisha ripoti ya CT Scan kutoka kitengo cha koo, masikio na macho.

Dkt Lucia alidai kuwa ripoti ya Kiran ilionesha kuwa kutokana na kemikali aliyopata katika macho alipata ugonjwa wa jicho na ubongo wake umepata mtikisiko, baada ya hapo alijaza fomu ya polisi Pf3.

Alidai kuwa madhara ambayo anaweza kuyapata ni kupata upofu na pia kidonda chake kinachukua muda mefu kupona sio wiki wala mwezi kwa sababu kina pona taratibu.

Pia, wagonjwa hao walipata maumivu ya  nyama laini, tatizo hilo walitibiwa Mnanzi Mmoja, baada ya hapo alijaza Julai 21,2023.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 12,2024 kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa mashahidi upande wa mashitaka.
 
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao ambao ni raia wa Tanzania wenye asili  ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jingo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023.

Katika shitaka la kwanza la kujeruhi linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jingo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.

Pia, katika shitaka la pili la shambulio la mwili linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo tarehe hiyo na eneo hilo alimsababishia madhara Lalit Ratilal katika mwili wake kwa kumpiga kichwa, ngumi na mateke kichwani.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu na la nne linalomkabili Sangita peke yake, ambapo anatuhumiwa kutoa matusi makubwa dhidi ya Lalit na Kiran kitendo ambacho kilileta fujo kwa namna ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.

Mtuhumiwa wa shambulio la kudhuru mwili, Bharat Nathwan (kulia) na mke wake, Sangita Bharat (kushoto) anayetuhumiwa kutoa matusi dhidi ya Lalit Ratilal wakiwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kusikiliza kesi inayowakabili. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...