Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini, TMA Dkt. Ladislous Chang'a akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuto utabiri wa mvua msimu wa Masika 2024

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imesema katika msimu wa masika, vipindi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi na kupelekea uharibifu wa miundombinu, mazingira, upotevu wa mali na hata maisha.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Chang'a amesema hayo leo Februari 22,2024 wakati akitangaza utabiri wa mvua za masika zinazotarajia kuanza wiki ya nne ya mwezi Februari, 2024 katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei 2024 katika maeneo mengi.

Kufuatia utabiri huo, TMA imeziasa mamlaka husika katika sekta mbalimbali na idara ya Menejimenti ya Maafa nchini kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza


Aidha, sekta, mamlaka husika na Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji/Mitaa zinashauriwa kushirikiana na kuchukua hatua stahiki ikiwemo kutoa elimu na miongozo itakayohamasisha kuzuia au kupunguza madhara, kujiandaa, kukabiliana na maafa na kurejesha hali endapo maafa yatatokea.

Mapema leo TMA imetoa tahadhari ya uwepo wa mvua za wastani hadi juu ya wastani kwa msimu wa Masika, 2024 zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Msimu wa mvua za Masika ni mahususi kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka katika mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Dkt. Chang'a ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, amesema mvua hizo za masika zinatarajiwa kuwa na ongezeko kubwa katika kipindi cha mwezi Machi, 2024.

"Kutokana na kuwa na matarajio ya uwepo wa mvua hizo kubwa kutakuwa na vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo," amesema Dkt. Chang'a.

Dkt. Chang'a alisema athari nyingine zinazotarajiwa kuongezeka kwa kina cha maji katika mito na mabwawa, magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji.

Aidha vyombo vya habari, vimeshauriwa kupata, kufuatilia na kusambaza taarifa za utabiri na tahadhari, pindi tu zinapotoka ili jamii iweze kuzipata kwa wakati.

"Tunawashauri kutafuta ushauri wa kitaalamu kutoka katika sekta husika wakati wa kuandaa, kutayarisha na kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji. Pia, inapendekezwa kutumia lugha nyepesi wakati wa kuhabarisha jamii," amesema Dkt. Chang'a.

Pia Dkt. Chang'a anaendelea kuwashauri watumiaji wote wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyamapori, wasafirishaji, mamlaka za maji, afya, shughuli za ujenzi (Makandarasi), uchimbaji madini, upakuaji na ushushaji mizigo bandarini kuendelea kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa wataalam katika sekta husika.

Pia amesema TMA itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua na hali ya hewa kwa ujumla nchini kadri inavyohitajika huku pia akiwashsuri wadau kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za mwelekeo na utabiri wa hali ya hewa ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...